Fedha bila shaka inatawala suala la michezo na wachezaji wa kimataifa. Iwe riadha, ngumi au soka. Fedha ndiyo motisha unaomfanya kijana mdogo wa miaka kumi adamkie viwanjani siku ambazo hakuna shule Jumamosi na Jumapili badala ya kupumzika na wenzake na kuchezea kompyuta.
Fedha ndiyo inayosukuma mabosi wa kampuni za masumbwi kukutanisha wapiganaji. Fedha ndiyo inayowafanya wanariadha wa Kenya na Ethiopia kuminyana na vilima vya Afrika Mashariki. Mwanariadha wa zamani aliposhinda aliambulia tu vikombe na sifa.
Leo mwanariadha anapotwaa medali yeyote huvamiwa na makampuni ya matangazo ya biashara. Fulana atakayovaa, viatu atakavyokimbia navyo, vyote hatimaye huwa na nembo mbalimbali za kibiashara. Mbali na sifa kwa nchi yake, mchezaji ni kama duka. Sura yake ina utajiri mkubwa kutokana na ushindi alioupata.
Pale mchezaji anapoanguka kwa tabia mbaya uwekezaji wa makampuni ya biashara pia huanguka naye. Katika miaka ya karibuni vilabu vya mpira vilivyojulikana zamani vimepitwa na vipya vilivyovumbuliwa au kununuliwa na matajiri. Tanzania tunayo Azam ambayo ukilinganisha na Simba na Yanga ni kama babu na kijukuu. Lakini Azam imekuja juu kutokana na nguvu za fedha na mipango mizuri ya mmiliki wake.
Uingereza klabu mbalimbali za zamani kama Liverpool ambayo iliyoshika taji miaka thelathini iliyopita sasa imepitwa na Chelsea na Manchester City. Wiki iliyopita mathalani tetesi za Lionel Messi kuja Chelsea zilienea London. Bei ya Messi hakuna atakayeiweza kama si klabu hizi mbili zinazomilikiwa na Warusi na Waarabu.
Hapo hapo gumzo kuu la waandishi wa michezo Uingereza limekuwa tabia za wachezaji wenye vipaji. Zamani mchezaji angeweza kuwa na fujo kwa kupiga wenzake ngumi au kumtukana marefa, lakini yalikwisha baada ya mechi.
Leo kuna wachezaji wanaong’ata wenzao meno – kama Luis Suarez- nyota ya Uruguay, Liverpool na sasa Barcelona. Ingawa Suarez anauma wenzake na kufunga bao kwa mkono kama alivyofanya wakati wa kombe la dunia la 2010, timu ziko tayari kumnunua na utukutu wake mradi anafunga mabao.
Mwingine aliyezungumziwa karibuni ni Saido Berahino. Berahino alizaliwa Burundi mwaka 1993 akahamia Uingereza na wazazi kutokana na machafuko ya eneo alilokuwa akiishi akiwa mtoto. Baada ya kusoma na kuanza kuchezea klabu kadhaa aliwika aliponunuliwa na West Bromwich. Hadi sasa anashika nafasi ya tatu kwa idadi ya mabao mengi kati ya vijana walio chini ya miaka 21.
Sifa hiyo inaongozwa na Alan Shearar na Francis Jeffers. Kutokana na ufungaji huu Berahino alichaguliwa timu ya taifa ya England mwisho wa mwaka jana. Mbali na ufungaji , Berahino ni mpiga chenga, mtoa pasi mzuri na ni mtulivu, hababaiki akiwa mbele ya goli. Mchezaji wa zamani wa England na Arsenal, Martin Keown amemlinganisha Berahino na mshambuliaji maarufu wa zamani Ian Wright aliyeichezea Arsenal na England miaka ya 1990.
Uamuzi wa Berahino kuwa mchezaji wa nchi isiyo yake, kumemjengea jina Uingereza ingawa ana vitimbi vyake. Juma lililopita alifikishwa mahakamani kwa kosa la kuendesha gari wakati amelewa. Mahakama imempa adhabu ya kufungiwa leseni ya udereva kwa mwaka mmoja.
Berahino na Suarez ni mfano wa vijana wenye tabia zisizo nzuri lakini vipaji vyao vinawafanya wananunuliwe na kupiganiwa . Mwingine ni Mario Balotelli aliyenunuliwa na Liverpool.