Menu
in

Je, ni wakati wa makipa kutoka Brazil kutamba Ulaya?

Edersson

WIKIENDI iliyopita licha ya kuwatazama vigogo wa EPL, Manchester City dhidi ya  Liverpool, tulikuwa na mjadala mzito juu ya nafasi ya golikipa. Katika kundi Sogozi la  World Soccer, hoja ilikuwa ni namna gani Brazil imefika kuzalisha makipa bora nyakati  hizi na kwanini kimewafikisha hapo.  

Katika mchezo wa EPL kati ya Man City na Liverpool kulikuwa na tukio moja ambalo  lilivutia machoni na akilini. Kuwaona makipa wawili wazaliwa wa Brazil wakiwa kwenye  vikosi vya kwanza vya timu zao lilikuwa tukio la kufikirisha. Alisson Becker alisimama  kwenye milingoti ya lango la mabingwa watetezi wa EPL Liverpool. Edersson Moreno  alikuwa amesimama katika lango la Manchester City. 

Swali letu kuu kwenye makala haya ni je, lini Brazil iliwahi kuibua vipaji vya makipa  abao walizichezea timu kubwa? Je, nini kimewafikisha Wabrazil hao kutamba katika  kandanda kwa sasa? 

Inafahamika kuwa Brazil ndiye bingwa wa Kombe la Dunia ambaye amelitwaa mara  tano. Inafahamu Brazil ndiyo nchi ambayo imekuwa ikizalisha vipaji vingi vya soka  duniani. Takwimu kutoka taasisi mbalimbali za kimichezo zinasema kuna wanasoka  takribani 3,000 wa Brazil waliozagaa nc hi mbalimbali duniani. 

Historia ya Brazil inaonesha kuwa imewahi kuwa na makipa hodari kama Claudio  Tafarrel, Nelson Dida na Julio Cesar. Dida alikuwa kwenye kikosi cha dhahabu cha AC  Milan nchini Italia chini ya kocha Carlo Ancelotti na kikiwa na mastaa kama vile Paolo  Maldini, Mauro Camoranesi, Gennaro Gattuso, Richardo Kaka, Ambrosini, Clarence  Seedorf na wengineo.  

Kwa upande wa Julio Cesar alikuwa nyanda hodari wa Inter Milan ya Italia pia ambako  amefanya mambo makubwa. Katika kipindi chake amecheza na mastaa kama vile Javier  Zanneti,Samuel Eto’o, Zlatan Ibrahimovic na wengineo. 

Rekodi zinaonesha kuwa makipa wa Brazil wamepata mafanikio zaidi katika Ligi Kuu  Italia maarufu kama Serie A, ambako Julio na Dida kwa nyakati tofauti walitwaa mataji  ya UEFA. Nje ya hapo makipa wa Brazil hawaonekani kutikisa dunia katika Ligi kama  vile BundesLiga(Ujerumani),EPL(England), Ligue 1(Ufaransa), Ereviside (Uholanzi), La  Liga (Hispania). 

Kwa mtazamo wangu tangu kumalizika fainali za Kombe la dunia mwaka 2014 Brazil  ambayo ilizabwa mabao 7 na waliokuja kuwa mabingwa Ujerumani inaonesha wanasuka  nafasi za makipa kwa nguvu. 

Kitendo cha makipa wao wawili Edersson na Allison Becker kutamba katika vikosi vya  Manchester City na Liverpool kinapeleka ujumbe kuwa Brazil imeleta kizazi kingine cha  walinda milango mahiri. 

Tanzania Sports
Allison Becker

Kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 kipigo walichokipata nchini humo  kwenye mchezo wa nusu fainali kiliwakosesha kucheza fainali dhidi ya Argentina  kwenye dimba la Maracana.  

Kwa kawaida uwanja wa Maracana umekuwa ukiwaliza Wabrazil wengi, ni maarufu kwa  msemo wa Maracanazo kutokana na vipigo vya dimba. Uwanja huo umekuwa ukiwaliza  mno Wabrazil linapofika suala la kutwaa taji.  

Ukiangalia rekodi zao za washambuliaji Brazil wametikisa dunia. Nafasi ya kiungo  wakabaji wametikisa dunia, ambapo mmojawapo wa viungo hao ni Gilberto Silva  ambaye mara kadhaa huwa nachati naye katika ukurasa wa Instagram masuala  mbalimbali kuhusu soka, hususani Fainali za Kombe la dunia mwaka 2002 na maisha  baada ya fainali hizo kipindi anachezea Arsenal.  

Kwenye nafasi ya mabeki Brazil nao wamebahatika kuwa na miamba iliyotikisa kwa  wakati wake. Katika kizazi hiki cha mwisho wapo Thiago Silva na David Luis ambao  wamecheza pamoja tangu timu za vijana za Taifa. Wana mastaa wa kutosha katika  nafasi mbalimbali lakini eneo la golikipa halikuwa na nyanda wengine waliotikisa nje ya  Dida na Julio Cesar. 

Turudi kwenye hoja ya msingi, kuanzia mwaka 2014 ingawa ni miaka 6 imepita, lakini  mwelekeo wa Brazil unaonesha kuwapika makipa. Kuibuka kwa makipa hawa na  kutamba EPL ni wazi Brazil inaendelea kurekebisha makosa yao ya miaka mingi kuwa  na makipa ambao wengi walikuwa wanacheza Ligi za ndani. Dida na Julio Cesar  kutamba ulaya ni kumetengeneza taswira chanya kwa makipa wa Brazil.  

Hivyo ujio wa Allison Becker na Edersson ambao wamekuwa wakichuana kupata namba  moja timu ya taifa Selecao, wamekuwa wababe ulaya. Liverpool aimetwaa taji la Ulaya  ikiwa na Alisson Becker, kisha Edersson amekuwa mhimili wa mafanikio yote ya  Manchester City chini ya Pep Guardiola. 

Ni halali kusema makipa hawa wanawakilisha kizazi kipya cha makipa ambacho  kinajaribu kupenya na kutamba kama wanavyofanya wachezaji wengine katika nafasi za  mabeki wa kati,pembeni, viungo na kadhalika. 

Wakati makipa wakiwa kwenye kiwnago bora na wanatamba Ulaya, bado kikosi cha  Brazil hakionekani kuwa na makali. Baada ya fainali za Kombe la dunia mwaka 2002,  Brazil ilikotwaa taji, haikuweza kutetea kwenye fainali za mwaka 2006. Katika fainali za  mwaka 2010 Afrika kusini ikiwa chini ya Caralos Dunga haikuwa na maajabu. Kisha  ikaja kuambulia taji la Olimpiki iliyofanyika jijini Rio De Janeiro.

Brazil imesua sua kiuwezo lakini imebahatika kuwa na makipa mahiri. Makipa ambao  wamekuwa vinara EPL. Ni zama mpya, na wanaonekana kupikwa makipa zaidi wa  Kibrazil.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version