Ukijadili mastraika bora na hodari wa soka kwa sasa katika kuzifumania nyavu nchini Uingereza basi hauwezi ukakaa bila ya kumtaja Jamie Vardy. Straika huyu wa timu ya Leicester City kwa misimu 5 amekuwa ni mwiba mkali kwa mabeki na makipa wa vilabu vinayoshiriki katika ligi kuu nchini England. Straika huyu ndiye mfungaji mkubwa kwa wakati wote wa timu ya Leicester city. Mchezaji huyu alikulia katika timu ya watoto ya Sheffield United. Timu ambayo inapatikana katika mji ambao yeye alizaliwa na kukulia hapo.. katika msimu wa mwaka 2019-2020 alishinda tuzo ya kiatu cha dhahabu nchini katika ligi kuu ya nchini Uingereza na kujiwekea rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa kushinda tuzo hiyo. Alipata bahati ya kuchaguliwa katika timu ya taifa ya England mnamo juni 2015 na alichaguliwa kushiriki katika kikosi kilichoshiriki mashindano ya mataifa ya ulaya ya mwaka 2016 na kilichoshiriki kombe la dunia mnamo mwaka 2018.
Jamie Vardy kwa sasa ana umri wa miaka 34. Alivuma msimu wa mwaka 2015-2016 baada ya kuiwezesha timu hiyo kubeba ubingwa wa ligi kuu nchini England. Ubingwa huo uliushangaza dunia baada ya ubingwa huo kwani timu hiyo iliubeba huku ikiwa haina mastaa na timu ambayo wachezaji wake walinunuliwa kwa bajeti ndogo sana ukilinganisha na timu karibia zote katika ligi hiyo ya England. Msimu uliofuata kiwango chake kiliongezeka na alikuwa ni chachu ya kuisaidia timu yake kuweza kuvuka na hatimaye kuingia ligi kuu
Vardy kwa kipindi kirefu alizunguka katika timu ambazo zinashiriki ligi za chini huko nchiniUingereza kabla ya kupata nafasi ya kucheza katika ligi kuu. Alipita katika timu kama Stockbridge park steels, FC Halifax Town, Fleetwood Town. Mnamo mwaka 2012 alisajiliwa na timu ya Leicester City ambayo katika kipindi hicho ilikuwa katika ligi daraja la kwanza nchini Uingereza. Msimu wake wa kwanza haukuwa mzuri na kuna nyakati mashabiki wengi walimchukia na aliwahi kufikiria kuacha kucheza mpira ni mpaka meneja wa wakati huo Nigel Pearson alipozungumza naye kwa kina na kisha kumshawishi asichukue maamuzi hayo.
Wachezaji wengi wa ndondo huwa wanapitia hali kama Vardy yaani kutumia mda mrefu sana kuzunguka katika timu ndogo. Changamoto ya wengi ambao nimekutana nao hapa Tanzania ni kukata tamaa mapema. Wengi huwa wakishazunguka sana huona kama hawawezi kufanikiwa kisoka. Tulimuangalia Vardy umaarufu wake aliupata akiwa ana umri wa miaka 29 umri ambao wengi wao wanakuwa wameshachoka na kukata tama ila yeye katika umri huo ndio akabeba ligi kuu Uingereza na kuwa mfungaji mkubwa wa kilabu hicho na kukifanya kilabu hicho kuandika historia duniani. Mwaka uliofuata timu kadhaa zilimtaka asajili katika zao ikiwemo Arsenal chini ya Arsene Wenger. Vardy alijibu moja ambalo ni kumbukumbu kwa klabu hiyo aliwaambia hata kwa pesa ya kiasi gani hawezi kuhama Leicester kwani kilabu hicho kilimnunua na kumthamini katika nyakati ambapo hakuna timu yoyote kubwa barani ulaya ambayo ilimtaka na aliamua kusalia kilabuni hapo mpaka hivi leo.
Yatarajiwa siku moja Vardy atajengewa sanamu katika klabu hiyo. Wachezaji wa ndondo wasikate tama wajitahidi kwenye mazoezi na huku watulize akili zao ipo siku yawezekana tukapata mafanikio ya kisoka kupitia wao. Kama ilivyo kwa wachezaji wa ndondo hufikia kipindi wanaacha mpira na kuanza kufanya shughuli nyingine basi hata Vardy aliwahi kufikia hatua hiyo kwani nyakati aliamua kuanza kujishughulisha na shughuli nyingine ndogo ndogo kwa ajili ya kuisaidia familia yake kwani hakuwa na mkataba wenye kipato kikubwa katika nyakati ambapo alikuwa katika hizo timu za madaraja ya chini.