ALIYEKUWA katibu mkuu wa klabu ya Yanga, Jamal Malinzi, ambaye anawania nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Nchini (TFF), amesema kuwa endapo atafanikiwa kuchaguliwa katika nafasi hiyo atahakikisha Tanzania inakuwa mwenyeji wa fainali za mashindano ya Afrika ya vijana kwa umri chini ya miaka 17 (U17) zinazotarajiwa kufanyika mwaka 2019.
Pia Malinzi alisema kuwa endapo atafanikiwa kushinda katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Jumapili atarejesha mashindano ya Kombe la Taifa, Kombe la Shirikisho na Ligi za madaraja ya chini ili kutoa nafasi kwa wachezaji wa hapa nchini kucheza mechi nyingi kwenye msimu mmoja.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Malinzi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kagera (KRFA) Tanzania ikifanikiwa kuwa mwenyeji wa michuano hiyo, timu yake ya vijana (Serengeti) itapata tiketi ya kushiriki fainali hizo na kuandaliwa kwa muda wa miaka mitano.
Malinzi alisema kuwa ili soka la hapa nchini liweze kuendelea ni lazima mambo manne yazingatiwe ambayo ni kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi, makocha, upatikanaji wa vifaa vya michezo na kuboreshwa kwa viwanja.
“Ni lazima tuwe na watu maalumu wa kusaka vipaji na vipaji bila walimu ni sawa na bure…kuna baadhi ya wachezaji wanacheza peku, hii nitaliangalia pia kwa kuzungumza na serikali ili kupunguza kodi katika vifaa vya michezo kwa sababu gharama zake ziko juu, mfano mpira wenye ubora unauzwa Sh. 300,000/=, hivi kuna shule ngapi zinaweza kumudu?,” alisema mgombea huyo.
Malinzi alisema pia akifanikiwa kuingia madarakani atahakikisha anaboresha Idara ya Ufundi kwa kuongeza wakurugenzi watatu wasaidizi ambao watakuwa wanashirikiana kubuni na kusimamia shughuli zote zinazohusu maendeleo ya timu za Taifa kuanzia za vijana hadi za wakubwa kwa upande wa wanawake na wanaume (Taifa Stars na Twiga Stars).
Alisema pia atabadili mfumo wa mgawanyo wa fedha za mapato ya milangoni na kueleza kwamba anasikitishwa kuona timu zinapata mgawo chini ya nusu ya mapato yanayopatikana katika kila mechi huku pia mikoa mingine ikikosa kuangaliwa kama Dar es Salaam inavyonufaika na faida ya mechi za Taifa Stars.
Alieleza pia atahakikisha wanawekeza katika kuendeleza waamuzi wa soka hapa nchini kwa sababu ni aibu Tanzania kutotoa mwamuzi kuchezesha mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 1998 kwa Omar Abdulkadir (mwamuzi mstaafu) kuchezesha fainali hizo.
“Wanafamilia ya mpira lazima tugeuke, tuwe wanaharakati tujenge mpira…nimejipima nimeona nina uwezo wa kutosha kumaliza tatizo hili,” alisema Malinzi ambaye katika nafasi hiyo anachuana na Makamu wa Rais anayemaliza muda wake, Athumani Nyamlani.
Mfumo wa timu kupanda daraja, Malinzi alisema atauendeleza lakini akaongeza kwamba kila mkoa uachiwe kuandaa mfumo wake wa kupata bingwa na si kucheza mechi za nyumbani na ugenini kama ilivyo hivi sasa.
Mgombea huyo alisema pia atahakikisha soka la wanawake linachezwa nchi nzima na kujipanga kuweka utaratibu na si kama ilivyo sasa hakuna mfumo imara.
Pia alisema atakakikisha anaunda kamati maalumu ya wanasheria watakaosaidia kuiboresha katiba ya TFF ikiwemo kuziangalia upya kamati zilizoundwa.