UONGOZI wa klabu ya soka Yanga ya jijini Dar es Salaam imezidi kujiimarisha baada ya jana kumpokea mshambuliaji mpya kutoka Brazil, Genlison Santos Santana ‘ Jaja’.
Jaja aliwasili nchini jana saa nane mchana na kupokelewa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Mohammed Bhinda, na anatarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi hicho ambacho hivi karibuni itapeperusha bendera ya Tanzania Bara katika mashindano ya Kombe la Kagame.
Hata hivyo mshambuliaji huyo kutoka katika klabu ya Itabaina ya Brazil bado hajasaini mkataba wowote na Yanga mpaka atakapokutana na viongozi wengine wa timu hiyo.
Inaelezwa kuwa endapo Jaja atapewa mkataba basi huenda Yanga ikaachana na Mganda, Emmanuel Okwi, ambaye abaonekana kuisumbua klabu hiyo.
Bhinda alisema kuwa kuwasili kwa nyota huyo ni kutaka kuziba mapengo yaliyoachwa na nyota wao wawili, Frank Domayo na Didier Kavumbagu waliohamia Azam.
“Ametoka Domayo na sasa tumemleta Jaja…Yanga oyeeee”, alisema kiongozi huyo akiwaambia wanachama wachache waliofika katika makao makuu ya klabu hiyo.
Jaja alishindwa kuzungumza chochote kutokana na kufahamu lugha ya kireno tu na hakukuwa na mkalimani aliyeandaliwa.
Mshambuliaji huyo aliwapungia mkono mashabiki wa Yanga kama ishara ya kuwasalimia baada ya kujitokeza kumlaki.
Jaja alizaliwa Septemba 21 mwaka 1985 na hii ni mara ya kwanza kuja Afrika.
Endapo Jaja atapewa mkataba mpya wa kuichezea Yanga iliyoko chini ya Kocha Mkuu, Mbrazil, Marcio Maximo, itabidi nyota mmoja wa kimataifa aondolewe.
Nyota wa kigeni ambao wana mikataba ya kuichezea Yanga ni pamoja na Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite kutoka Rwanda, Hamisi Kiiza, Emmanuel Okwi (Uganda) na Andrey Coutinho wa Brazil.