Hatimaye Ivory Coast wamemaliza kazi ngumu waliyoanza kwa kutwaa ubingwa wa Afrika.
Katika mechi kali baina yao na Ghana, Tembo wa Afrika walithibitisha ukubwa wao kwenye mikwaju ya penati baada ya kumaliza dakika 120 wakiwa sare.
Alikuwa ni kipa Boubacar Barry aliyeibuka shujaa wa mchezo baada ya kumzidi mwenzake ujanja kwa kukwamisha nyavuni penati iliyotoa uamuzi wa mwisho.
Tembo waliwashinda Black Stars kwa penati 9-8, ambapo Barry baada ya kuzuia mkwaju wa Ghana, Brimah Razak alikwenda kutia mpira kwenye eneo la penati na kufunga, ikiwa ni marejeo ya mwaka 1992 ambapo ushindi ulikuwa wa penati 11-10 baina ya timu hizo mbili.
Hili ni kombe la pili kwa Tembo hao katika michuano hiyo, ambapo mwaka 2006 na 2012 walikaribia kulitwaa lakini wakazuiwa na Zambia waliokuwa wakinolewa na Kocha Herve Renard, Mfaransa ambaye sasa yupo na Ivory Coast.
Kocha wa Ghana, Mwisraeli Avram Grant alipokea kwa masikitiko matokeo hayo, ambapo sasa amepoteza kwa mikwaju ya penati katika mashindano makubwa mawil, ya kwanza akiwa bosi wa Chelsea dhidi ya Manchester United katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ivory Coast walipoteza penati zao mbili za kwanza kupitia kwa mshambuliaji mpya wa Manchester City, Wilfried Bony aliyegonga mwamba na Junior Tallo aliyepiga nje, lakini
Afriyie Acquah na Frank Acheampong wa Ghana nao walikosa zao, hivyo kuweka mambo sawa.
Ghana walikuwa na nafasi nzuri zaidi za kufunga mabao katika dakika 120 za mchezo lakini walishindwa kuzitumia.
Fainali hizo zilihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Sepp Blatter.