Menu
in , ,

Ivory Coast fainali AFCON

Ivory Coast wamezidisha makali na tamaa yao ya kutwaa ubingwa wa Afrika, baada ya kufika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Tembo wa Afrika walifanikiwa kuwachapa Kongo Kinshasa 3-1 kwenye pambano kali ambalo wote walitawala sawa mchezo, lakini Ivory Coast wakawazidi maarifa, bao la kwanza likitiwa kimiani na nyota wa Manchester City, Yaya Toure dakika ya 20.

Kiungo huyo alifunga kwa shuti kali kutoka yadi 20 lakini dakika nne baadaye Dieumerci Mbokani akawasawazishia Chui kwa penati baada ya Eric Bailly kuunawa mpira. Dakika nne kabla ya mapumziko Gervinho aliyevuma sana kwenye mechi hiyo alipachika bao la pili na kuwapa nguvu wenzake.

Ivory Coast walijihakikishia ushindi baada ya Wilfried Kanon kufunga la tatu dakika ya 68 baada ya mpira wa kichwa wa beki Serge Aurier kuokolewa wakati ukiwa wazi kuelekea nyavuni. Nusura Gervinho afunge bao jingine, lakini kipa matata wa Kongo, Robert Kidiaba aliokoa.

Ivory Coast walifika hainali 2006 na 2012 lakini walipoteza mechi zote hizo, katika jitihada zao kupata tena kombe hilo walilolitwaa mara moja tu, 1992. Licha ya kustaafu kwa mchezaji wao nyota Didier Drogba, Ivory Coast wameendelea kuwa hatari, hali inayomridhisha Kocha Herve Renard anayechanganya wakongwe na chipukizi, huku akisema wanaweza kucheza vizuri kuliko wanavyofanya.

Alhamisi hii wenyeji Guinea ya Ikweta wanacheza na Ghana kwenye nusu fainali nyingine, mchezo unaotarajiwa kuwa kivutio kikubwa, kutokana na jinsi wenyeji walivyofanikiwa kuvuka vizingiti, japokuwa kulikuwa na utata.

Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limemfungia kuchezesha na kuingia uwanjani kwa miezi sita, mwamuzi Rajindraparsad Seechurn aliyewapa Guinea penati tata dakika za lala salama za mechi ya robo fainali dhidi ya Tunisia.

Shirikisho la Soka la Tunisia, ambalo wachezaji wake walimzonga na kumkimbiza mwamuzi huyo, nalo limetozwa faini ya pauni 33,000. CAF wamesema kwamba mwamuzi huyo alishindwa kumudu mchezo na kuhakikisha utulivu unakuwapo.

Licha ya hayo, Tunisia wametakiwa kulipa pia gharama za mlango na jokofu walivyoharibu kwenye chumba chao cha kubadili nguo katika Uwanja wa Bata.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version