HAKUNA ubishi kwamba, angalau dunia yote ya soka kwa sasa inaijua Tanzania.
Si kwa kupitia timu ya taifa ya wakubwa `Taifa Stars’ walioigomea Cameroon na baadaye kukubali kulala kwa 2-1 ugenini huko Yaounde, bali kupitia soka ya vijana.
Ndiyo. Ni vijana wenye 16 umri wa chini ya miaka 17 waliopatikana kupitia michuano ya Copa Coca Cola na baadaye kwenda Brazil kwa mafunzo maalumu katika chuo cha mkongwe Carlos Alberto Parreira huko Rio de Janeiro.
Wakishiriki kwa mara ya kwanza, vijana wa Tanzania walionyesha maajabu ya soka, wakiipangua timu moja baada ya nyingine na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano maalumu iliyopewa jina la Coca Cola International Tournament. Imetoa pia kipa bora wa michuano hiyo, Mohammed Aziz.
Walianza kwa kuirarua Peru kwa mabao 5-0 na baadaye ikashuka dimbani kuivaa Chile iliyogangamala na kulazimisha suluhu.
Kutoka kwa Chile, kiama kiliwakuta Argentina, moja ya nchi zinazoheshimika sana kisoka duniani.
Nchi hii iliyowahi kutoa nyota halisi wa soka tangu enzi za Mario Kempes na wengine na baadaye akina Diego Armando Maradona, Diego Simeone, Hernan Crespo, akina Roberto Ayala, Gabriel Heinze, Juan Pablo Sorin, Gabriel Milito, Esteban Cambiasso, Pablo Aimar, Javier Mascherano, Carlos Tevez, Hernan Crespo, Lionel Messi, Javier Saviola, Julio Cruz, Rodrigo Palacio na wengine wengi, likaushwa na Tanzania kwa mabao 2-0 katika mchezo wa robo fainali.
Katika nusu fainali, Paraguay ilizamishwa kwa 3-1, kabla ya kufanya kufuru kwa kutwaa ubingwa baada ya kuizamisha Chile kwa 1-0 katika mchezo wa fainali.
Kocha Msaidizi, Sylvester Marsh, akiwa mwenye furaha alikaririwa akisema: “Hata Wabrazil hawakuamini kwamba ni timu ya Tanzania, nchi isiofahamika sana kisoka duniani. Tumewaduwaza.”
Kwa hakika, yatosha kujiridhisha kwamba, soka ya Tanzania imeweza kujipambanua kuwa kama kukiwa na mikakati thabiti, mambo yanaweza kuwa mazuri zaidi katika siku za usoni.
Hii inaweza kuanzia kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kuwa na mikakati ya kutovtpa vipaji vyao, kama ilivyojitokeza siku za nyuma.
Ndiyo, nathubutu kusema TFF ni wauaji wa vipaji kwa sababu miaka nenda miaka rudi, nyota wanaoibuka wanaishia kusikojulikana ama wakiachwa wajitafutie malisho, bila programu maalum.
Leo hii na kiongozi gani wa TFF anayeweza kusimama kidete na kueleza waliko nyota wa timu ya taifa ya vijana wenye umri wa miaka 17 `Serengeti Boys’ walioipeleka nchi katika fainali za Afrika huko Gambia, ingawa kosa la kiufundi la Nurdin Bakari lilitukwamisha?
Ni wazi kwamba wengi watashindwa na kigugumizi, kwani wanaosikika mpaka leo, ni wale waliojitafutia malisho, lakini kuna waliokozikwa kabisa.
Sitaki kuzama katika hili, lakini cha msingi ni kwamba, kwa kuwa vijana hawa wameonyesha mwelekeo, ni wakati sasa wa kuwaweka pamoja, wakaunda timu ya taifa na kukomazwa kimataifa.
Hivi ndivyo wanavyofanya wenzetu wa nchi zilizopiga hatua kikosi, wani mara nyingi mastaa wao hupikwa kuanzia utotoni na kushirikishwa katika michuano ya vijana wa umri mbalimbali kabla ya kuanza kuogelea katika lindi la utajiri katika klabu kubwa za Ulaya.
Ndiko walikopitia akina Maradona, Tevez, David Beckham, Nwankwo Kanu na wengine waliovuma na wanaoendelea kuvuma. Walipitia katika tanuru la timu za watoto, wakalelewa vizuri na hatimaye kuiva kwa soka ya kimataifa.
Kwa kujua mbinu hizo, haitashangaza baada ya miaka miwili kusikia moja ya klabu kubwa duniani ikimwaga mabilioni ya shilingi kumnunua mmoja wa wachezaji wa Argentina, Paraguay au Chile kutokana katika kundi la hawa hawa waliohenyeshwa na watoto wa Tanzania.
Ndiyo maana nashauri hivi; Serikali, TFF na wadau wa soka kwa ujumla wasiishie kuwapokea kifahari watoto hawa, bali huu uwe mwanzo wa kuwalea ili katika miaka michache ijayo, kundi hili lianze kutoka nyota wa kucheza soka ya kulipwa Ulaya ambao kimsingi ndio watakaoifanya Taifa Stars kuwa imara.
Hali kadhalika, kwa utajiri watakaovuna barani Ulaya na kwingineko, hakuna shaka utarudi nchini kuimarisha uchumi kupitia vitegauchumi mbalimbali, huku wengi wakinufaika kutokana na ajira zitakazotengenezwa na vitegauchumo husika.
Na tuanze sasa kuwalea vijana hawa, vinginevyo miaka michache ijayo tutajikuta tukiyashangaa mafanikio na makinda wenzao waliowatoa nishai huko Brazil.
Kamwe tusirudie makosa ya siku za nyuma, hasa kwa wakati huu ambao tayari tuna mawakala wa soka wanaotambuliwa na FIFA kama Mehdi Remtullah.