KANUNI za shirikisho la Soka Duniani, FIFA zinazuia serikali yoyote kuingilia masuala ya soka. Ikumbukwe wakati wa uongozi wa Muhidin Ndolanga Tanzania imewahi kupitia kipindi kigumu kiasi kwamba masuala ya soka yaliingiliwa na serikali pamoja na mifumo ya Mahakama kwa maana ya kesi za michezo kupelekwa mahakamani.
Mchezo wa soka unasimamiwa na taasisi zinazotambulika na Mataifa yetu. Bahati mbaya siasa inapochukua nafasi kwenye masuala ya kimichezo ni mwanzo wa kuharibu mwenendo mzuri ama hata kile kitu kidogo kilichotengenezwa. Majirani zetu Kenya ni wazoefu wazuri kwenye suala la kufungiwa na shirikisho la soka.
Mara nyingi serikali inapoingilia masuala ya soka huwa inaweza kuigharimu nchi husika kama ambavyo imewahi kutokea kwingineko ama hapa kwetu. Utaratibu huu wa siasa kuingilia masuala ya utawala wa mpira ni miongoni mwa sababu za maendeleo hafifu ya michezo yenyewe. Siasa kama ilivyo si mbaya lakini wanayofanya wanasiasa kwa hulka binafsi iwe moja kwa moja au kwa kupitia mlango wa nyuma huwa inaleta matokeo hasi.
Mchezo wa soka unapendwa sana Tanzania lakini tukubali kuwa masuala ya kisiasa yanachangia kiasi kikubwa kuvunjwa kwa kanuni zinaozowekwa ili kuendesha mchezo huo. Mara nyingi kwenye suala la kikanuni huwa tunasema iingizwe busara, kana kwamba wakati tunatunga kanuni hizo tulikubaliana kuweka busara.
Mchezo wa soka ni kama biashara nyingine, washabiki ni wateja ambao wanatakiwa kuthaminiwa. Katika uendeshaji wa soka washabiki wanahitajika kuamsha ari ya wachezaji, kupata burudani, kuchangia mapato na maendeleo ya mchezo wenyewe lakini kama hawapewi heshima ni wazi idadi yao itaanza kupungua viwanjani. Katika hali hiyo lazima tujiulize madhumuni ya kutunga kanuni za Ligi Kuu ni pamoja na kutambua utaratibu wa kuendesha ligi na wadau wanatakiwa kuzifuata.
Tangu machi 8, 2025 kumekuwa na mijadala mingi kuhusiana na taratibu za mchezo wa watani wa jadi, Yanga na Simba. Mchezo huo haukufanyika kwa sababu ambazo sote tunazijua na mbaya zaidi tunaona video zikisambaa kuonesha hali halisi. Madai ya Simba yaliwekwa bayana, na Yanga nao wanayo sababu yao katikamazingira ya sasa. Katika pande hizi mbili ni lazima tukubali suala la kanuni tulizoweka ni muhimu kutumika kuliko kuingiza masuala ya siasa.
Ligi Kuu inayopanda ngazi na kupendwa na maelfu ya watu barani Afrika inataka kuingia kwenye mtego wa kisiasa. Hapakuwa na sababu zozote za wenye mamlaka kuonana na Waziri wa Michezo kama njia ya kuzungumza kutafuta suluhu. Swali linaloulizwa ni suluhu ya aina gani ambayo haiwezi kupatikana kikanuni? Sababu za kuahirishwa mchezo zilitajwa, lakini kila zikichambuliwa bado zinaleta mashaka. Video zinaonesha ni watu aina gani waliozuia Basi la Simba lisiingie usikue ule.
Kila kitu kipo bayana, lakini kutumia njia hiyo kama sababu ya kuahirisha mchezo saa chache kabla haujaanza ni dhahiri hatuwatendei haki mashabiki wa Ligi Kuu. Tunapoanza kuingiza wanasiasa kwenye uendeshaji wa Ligi Kuu maana yake tunakaribisha vurugu. Hakuna sababu ya kuingiza siasa kwenye kamati ya saa 72 ambayo inawajibika kutoa taarifa ya kile kinachotokea. Hakuna sababu ya kuingiza siasa kwenye Bodi ya Ligi Kuu kwa sababu inakuwa chanzo cha kuvuruga Ligi Kuu.
Miongoni mwa sababu za ugomvi kati ya KFF (sasa ni FKF) ilikuwa siasa. Ni siasa ilisababisha Kenya ipokonywe uenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1996 na zikapelekwa nchini Afrika kusini. Siasa za aliyekuwa Rais wa Kenya na mwanasiasa aliyekuwa akiongoza KFF wakati huo walikuwa wanatoka vyama tofauti hivyo walihisi yule wa upande wa michezo angelipata umaarufu na sifa nyingi kuliko Rais Moi.
Tukio hili lilitia doa soka la Kenya na linaonesha namna wanasiasa walivyo virusi vibaya kwenye uendeshaji wa soka. Tanzania haitakiwi kufuata nyayo za kutegemea maamuzi ya wanasiasa kuendesha Ligi Kuu. Tanzania haitakiwi kutegemea busara kuendesha Ligi Kuu badala yake utaratibu usemwe kikanuni. Mfani kwenye mkanganyiko wa kuahirishwa mechi ya Machi 8, 2025 kati ay Simba na Yanga Bodi ya Ligi imejikanganya sana. kwenye barua ya Machi 8 walilaumu Simba kutowashirikisha wahusika wa uwnaja, timu mwenyeji, maafisa wa mchezo na kadhalika. Lakini kwenye barua ya ufafanuzi,
Bodi ya Ligi hiyo hiyo ilileta hoja mpya kudai kuwa kanuni hazisemi Simba au timu mgeni apewe uwanja muda gani ama kuwasiliana na wahusika wa uwanja, timu mwenyeji na maafisa wa mchezo. Mkanganyiko huu ndiyo unasababisha malumbano kisha tunajikuta tunaingia kwenye siasa za mpira. Mpira wetu ambao tunaupigania uwe ‘brand’ muhimu na kubwa barani Afrika tumeanza kuingiza makando kando.
Wakati taasisi za utafiti zikihangaika kuitafiti Ligi Kuu, sisi wenyewe tunahangika kutofuata kanuni zilizowekwa na badala yake. Hatua tuliyofikia inanikumbusha jinsi aliyekuwa Afisa mtendaji wa Simba na Yanga, Senzo Msingiza ambapo pamoja namambo mengine kwenye mahojiano na vyombo vya habari amewahi kutamka kuwa mpira wa Tanzania unategemea busara za wanasiasa, jambo ambalo halifai kwa maendeleo ya mchezo wenyewe. Kwamba sekta ya michezo haina uamuzi wa mwisho kuendesha masuala hayo kwa mujibu wa sheria zinazowapa mamlaka lakini busara za wanasiasa ndizo zinapewa nafasi.
Mambo ya kamati au vikao vya kusuluhisha ni vitu visivyo na tija na vinaonesha jinsi gani kwetu kanuni zetu ni geresha huku tukiwa na dhamira tofauti. Tutambue kuwa siasa huwa ni kero kubwa linapofika suala la uendeshaji wa mpira wa miguu na wanaojua hilo waliamua kuiweka kando serikali na wanasiasa wake. tunaweza kushirikiana kwenye mendeleo ya mpira wa miguu lakini si kutegemea siasa kuongoza mpira huo.