Kwa sasa Yanga iko mabegani mwake ameibeba huku akiwa anatembea nayo katikati ya jangwa, kulia kwake hakuna maji, kushoto kwake hakuna chakula na kibaya zaidi mbele yake hakuna wa kumsaidia na yeye hatamani kurudi nyuma.
Nyuma ni sehemu ambayo anaichukia sana, kwa ugumu wote anatembea taratibu kuelekea mbele, yeye ndiye mchezaji pekee ndani ya kikosi cha Yanga anayeonesha kutamani kwenda mbele.
Anapigana sana sehemu ambayo wenzake wanaonekana kupigana kidogo. Kila mchezo kwake ni fainali anajituma sana, sijui kipi kinachomfanya ajitume kiasi hicho.
Na sijui lengo lake ni lipi mpaka aamue kujituma kiasi hicho? ni mchezaji wa kulipwa? au bado anawaza kujiuza zaidi ili asajiliwe na timu nyingine kwa pesa ndefu?. Maswali ambayo kichwa changu hakina majibu sahihi.
Mechi nane ndani ya kikosi cha Yanga, mechi ambazo amehusika katika magoli 6, amefunga magoli 3 na kutoa pasi tatu za mwisho za magoli. Wastani wa kuhusika na goli 0.8 kwenye kila mechi.
Huyu ni Bernad Morrison, mchezaji ambaye kwa sasa ndiye lulu kwenye kikosi cha Yanga. Anatengeneza nafasi vizuri sana za kufunga magoli ndani ya mechi.
Anawapa mitihani mabeki wa timu pinzani, mara nyingi huwa wanatumia muda mwingi kufikiria namna ya kumzuia na siyo namna ya kuisaidia timu yao kushambulia kwenda mbele.
Huyu ndiye anayepiga krosi nyingi, anapiga pasi nyingi kwenye eneo la mwisho (final third ) Lakini tatizo linakuja Moja tu, washambuliaji ambao anawapa hizo pasi hawana uwezo mkubwa wa kuzifanya hizo pasi kuwa magoli.
Hapa ndipo ninapoanza kumkumbuka Juma Balinya mtu ambaye aliachwa na Yanga bila kujua kwanini kaachwa. Mshambuliaji mzuri ambaye hakupewa nafasi kwenye kikosi cha Yanga, nafasi ambayo amekuja kupewa Yikpe .
Juma Balinya alikuwa na uwezo wa kufunga, achana na hilo. Siku hizi mpira ni mchezo wa uwazi (spaces) unapotengeneza spaces kwenye mpira ndiyo unakuwa na nafasi kubwa ya kushinda mechi husika.
Tatizo moja wapo katika kikosi cha Yanga kwa sasa washambuliaji wake hawatengenezi uwazi (spaces), uwazi ambao ungewawezesha viungo washambuliaji kuutumia kufunga.
Mfano muda mwingi Yikpe huwa anakuwa katika eneo lake, huwa hatoki kwenye eneo lake. Faida moja wapo ya kutoka kwenye eneo lako, kila unapotokka lazima utoke na beki wa Kati, unapotoka na beki wa Kati lazima nyuma kuwe wazi, uwazi ambao wachezaji wenzako watautumia.
Hiki kitu hakipo, ndiyo maana Bernard Morrison kuna wakati hapati uwazi katika eneo la mbele, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, Balama Mapinduzi pia hawapati uwazi eneo la mbele, eneo la mbele la Yanga huwa linakuwa gumu sana kwa sababu hakuna uwazi unaotengenezwa katika eneo hilo.
Hapa ndipo ninapomkumbuka Juma Balinya, Juma Balinya ambaye alikuwa na uwezo wa kwenda kushoto mwa uwanja, kulia na kushuka katikati ya uwanja, kila alivyokuwa anaenda lazima alikuwa anaenda na beki mmoja wa Kati kitu ambacho kilikuwa kinatengeneza uwazi eneo la mbele.
Pamoja na kwamba Juma Balinya alikuwa na uwezo wa kufunga kuzidi kina Yikpe, Molinga Lakini pia anauwezo mkubwa wa kutengeneza uwazi eneo la nyuma kitu ambacho hakipo kwa sasa kwenye kikosi cha Yanga .