Mbele ya mvua kubwa, upepo mkali, baridi kali na radi za kutisha, miguu yangu imechagua kusimama juu ya kilele cha mlima mrefu. Mboni zangu zimefanikiwa kupenya katikati ya wingu zito na kutua Jangwani. Sehemu ambayo mboni zangu zinaona rangi mbili tu, rangi za njano na kijani.
Sehemu ambayo Yanga ilichagua kuishi. Klabu pekee ambayo kwa miaka mingi ilikuwa ngumu kutofautisha masika na kiangazi kwao. Walifundishwa umoja na kupeana moyo na ndiyo maana hawaamini katika kurudi nyuma hata siku moja.
Haijalishi dhoruba gani wanakutana nalo kurudi nyuma kwao ni mwiko. Hatua za kwenda mbele kufikia mafanikio ndiyo hatua ambazo wanaziamini siku zote. Kwenye akili zao wanaamini mwisho wa dhoruba kuna wingu la dhahabu inavyovutia.
Radi zinapiga. Macho yangu yanagoma kuzifumba mboni zangu kwa sababu mbele yangu kuna filamu ya soka naitazama, filamu ambayo inarudisha miaka 26 iliyopita kwenye uwanja wa zamani wa Taifa maarufu kwa jina la “shamba la bibi”.
Mwaka 1998. Mwaka ambao Yanga walifanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Ilihitajika miaka 25 tena Yanga kufuzu tena hatua ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Huu ndiyo mwaka ambao Yanga walicheza na Ethiopia Coffee ya Ethiopia na Yanga kushinda goli 6-1.
Yanga hakufanikiwa kufanya vizuri kwenye michuano hiyo baada ya kufuzu hatua ya makundi, dhoruba kubwa lilitanda kwenye safari yao. Walizidi kwenda mbele daima na neno kurudi nyuma halikuwepo kwenye kamusi yao ya mafanikio.
Waliamini kuna siku watafanikiwa kufanya vyema. Ukame ulizidi kwenye ardhi yao, hakuna mmea uliofanikiwa kumea kwenye ardhi yao. Hakukuwepo na chakula cha kuwatosheleza tena, njaa iliwakamata sana.
Miili yao ilidhoofu lakini matumaini yao yalinawiri kila uchwao. Kila jua lilipokuwa linachomoza ilikuwa ishara ya wao kupata mwanga kwenye giza lao. Walihitaji mwanga maana hawakuwa na uwezo wa kuona tena kamusi yao ya mafanikio.
Licha ya kukosa malisho mazuri, kudhoofika mwili fikira zao ziliamini katika kuyakimbilia mafanikio. Katikati ya giza totoro ghafla mwanga ulionekana tena mwaka 2015.
Mwaka huu ulipokelewa na tabasamu pana la wananchi wa jangwani. Kwenye vifua vyao wakabeba vitu viwili, moyo na matumaini wakawa na moyo wenye matumaini makubwa sana. Moyo huu ulijengwa na Yusuph Manji.
Binadamu ambaye alikuja kubadilisha biashara ya mpira wa miguu hapa Tanzania. Binadamu ambaye hakuogopa kufungua pochi lake nene kutoa kiasi chochote cha fedha ili kumchukua mchezaji yoyote bora.
Rasmi Yanga ikawa nyumba ya wachezaji bora hapa Tanzania. Kila kipaji kilichokuwa bora kilitakiwa kucheza Yanga. Yanga iliweka utawala wake ikawa timu ya kuogofya. Hata ile ndoto yao kubwa ya kufanya vyema kimataifa ikawa na matumaini.
Walifika hatua ya makundi ya kombe la shirikisho. Wananchi wakawa wanaamini wapo kwenye njia sahihi ya kuelekea walipo kina TP Mazembe kwa wakati huo na timu zingine kubwa barani Afrika.
Ghafla mwanga ukazima tena, nuru ikatoweka kwenye mji wa jangwani. Ukame ukajenga makazi rasmi kwao, njaa ikawa na urafiki mkubwa na wao. Waliinamisha vichwa chini kutafakari, kipi sahihi kwao? Kurudi nyuma au kwenda mbele?
Wakati wakiwa wanatafakari sauti ikawajia kichwani kwao ikisema , Daima mbele mwiko nyuma. Sauti ambao iliwafanya wasimame na kuendelea na safari yao. Walifanya kila wanachoweza ili wafanikiwe kwenda mbele.
Kuna nyakati walishika bakuli ili waombe barabarani ili tu waendelee na safari yao. Kwao wao walikubali fedhea kuliko kurudi nyuma au kuishia njiani. Katikati ya safari yao walikutana na mtu ambaye walijenga uswahiba naye.
Mtu ambaye aliwaaminisha anaweza kuifanya Yanga kuwa “Club Above All” fundo la mate ya tamaa lilipita katikati ya koo la wana Yanga, fundo ambalo lilisindikiwa na utulivu wa kumsikiliza swahiba wao mpya.
Ilikuwa lazima watulie na kumsikiliza. Ilikuwa lazima wameze fundo la mate la tamaa kwa sababu watani wao kipindi hicho walikuwa wanafanya vyema kimataifa. Kwa watani wao ilikuwa ni habari ya kawaida kufika hatua ya robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
Kelele za mafanikio za watani wao ziliwaumiza sana Yanga. Wakawa wanaamini kabisa na wao wanastahili kufika hatua ile. Swahiba wao mpya aliwahakikishia kuwa wanaweza kufika hatua kubwa zaidi na hatua wanazofika watani wao.
Wakatabasamu, wakatazamana kisha wakamfungulia mlango ili aweze kuingia kwenye nyumba yao, rasmi kukafungwa ndoa ya mafanikio kati ya Yanga na GSM.
Ndoa ambayo lengo kubwa ni kuifanya Yanga kuwa kubwa kuliko, kuifanya Yanga iwe moja ya klabu tishio balani Afrika. Pochi la GSM likafunguka rasmi ili kuijenga Yanga.
Chini ya GSM , Yanga ikafanikiwa kufika hatua ya fainali ya kombe la shirikisho barani Afrika. Chini ya GSM, Yanga ilifanikiwa kufika hatua ya makundi ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa mara baada ya miaka 25.
Chini ya GSM, Yanga imefanikiwa kutengeneza timu bora na yenye wachezaji bora ambao wanauwezo mkubwa wa kuifikisha timu katika hatua kubwa kwenye michuano ya vilabu barani Afrika.
Wakati naitazama Yanga jana kwenye mechi dhidi ya CBE ya Ethiopia nilibaki na maswali mengi sana kichwani kwangu. Lakini swali kubwa ambalo linatakiwa kujibiwa na GSM ni kuwa Yanga hii inaweza kuwa ile TP Mazembe tishio ?