Taarifa rasmi ya Barcelona kumpa mkataba wa miaka miwili aliyekuwa kocha wa Athletic Bilbao imewashangaza wengi. Yalitarajiwa majina makubwa kama Jorge Sampaoli, Jurgen Klopp, Mauricio Pochettino au Ronald Koeman kuchukua mikoba ya Luis Enrique. Ni Ernesto Valverde aliyepata nafasi ya kuwa meneja wa Lionel Messi, Neymar, Gerard Pique, Luis Suarez na nyota wakubwa wengine ndani ya kikosi cha Barcelona.
Imewezekanaje kocha ambaye ameshindwa kuiwezesha Bilbao angalau kukata tiketi ya kushiriki Europa League msimu ujao apewe mikoba ya kuifundisha klabu yenye mafanikio zaidi duniani kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita? Inawashangaza wengi. Wengi wanashangaa kocha aliyemaliza katika nafasi ya 7 kwenye msimamo wa La Liga kwenye msimu uliomalizika apewe nafasi ya kufundisha klabu yenye mengi zaidi ya La Liga ndani ya misimu 10 ya nyuma.
Kocha huyu aliyefundisha timu kama, Espanyol, Villarreal, Athletic Bilbao na Valencia ndani ya soka la Hispania kwa zaidi ya miaka kumi kwa vipindi tofauti ameshinda kombe moja tu kwenye soka la Hispania. Ana jina dogo na rekodi ndogo ya mafanikio ya maana ndani ya soka la Hispania. Washabiki wanashindwa kuwaelewa Barcelona kumkabidhi timu kocha wa namna hiyo.
Tangu alipoteuliwa kuwa kocha wa Bilbao Julai 2013 mshambuliaji huyo wa zamani wa Barcelona ameiongoza Bilbao kwenye michezo 212 huku akipata ushindi kwenye michezo 102 pekee kati ya hiyo. Uwiano huo wa ushindi ni asilimia 48 ya michezo yote.
Pengine klabu kama Bilbao ambayo sambamba na Barcelona na Real Madrid pekee hazikuwahi kushuka daraja kwenye Ligi Kuu ya Hispania inatosha sana kwa kocha bora kuwa na uwiano mzuri wa ushindi zaidi ya huo. Huyu anawezaje kuwa kocha wa Barcelona?
Kwanini sio Sampaoli aliyeiwezesha Sevilla kukamata nafasi ya nne kwenye msimu wa La Liga uliokwisha? Barcelona hawakumuona kocha huyu aliyeiwezesha Chile kutwaa taji la Copa America mwaka 2015? Kwa maoni ya wengi huyu ndiye alipaswa kuwa kocha wa Barcelona. Alistahili kuwa kocha wa Lionel Messi. Lakini Barca wanamuacha na inaripotiwa kuwa ameshaingia makubaliano na chama cha soka cha Argentina ili kuinoa timu hiyo ya taifa.
Lakini tukifikiri vizuri tunaweza kuacha kuwashangaa Barcelona na tukajigeukia na kujishangaa wenyewe. Hivi Pep Guardiola alikuwa na rekodi gani ya maana wakati anapewa mikoba ya kuinoa Barcelona mwaka 2008? Uzoefu pekee aliokuwa nao kwenye ukocha ni kuinoa Barcelona B kwa mwaka mmoja pekee. Joan Laporta akamtangaza kuwa kocha wa Barca mwaka 2008. Kwenye msimu wake wa kwanza alishinda kila taji aliloshiriki.
Pep alikuja kushinda jumla ya mataji 14 akiwa kocha wa Barca ndani ya misimu minne. Tuzo binafsi pia zilimiminika. Anazo tuzo kubwa kadhaa ikiwemo ile ya Kocha Bora wa Mwaka wa FIFA ya mwaka 2011. Jose Mourinho aliyekuwa na uzoefu mkubwa na rekodi kubwa akiwahi kufundisha kwa mafanikio timu kama FC Porto, Chelsea na Inter Milan kwa ujumla alizidiwa kimafanikio na Pep walipokuwa Hispania kwa misimu kadhaa.
Luis Enrique pia alikabidhiwa kibarua cha Barcelona akitokea Celta Vigo akiwa na jina dogo na rekodi za kawaida kabisa kuhusiana na ukocha. Katika michezo 40 aliyoiongoza Celta Vigo kwenye msimu wake pekee aliokuwepo alishinda michezo 15 tu. Hizo ni sawa na asilimia 37.5 za uwiano wa ushindi. Valverde ana uwiano mzuri zaidi wa ushindi kwenye michezo aliyoiongoza Bilbao kwa kipindi cha miaka minne.
Luis Enrique alishinda mataji yote matatu aliyoshiriki kwenye msimu wake wa kwanza. Ameipa Barca jumla ya mataji 9 kwa misimu mitatu. Anakumbukwa zaidi kwa taji la Ligi ya Mabingwa alilotwaa baada ya kuwafunga Juventus 3-1 kwenye mchezo wa fainali jijini Berlin 2015. Alitwaa pia tuzo ya Kocha Bora wa mwaka ya FIFA 2015. Valverde hatashindwa kufanya makubwa kama haya iwapo Messi na wenzie watakuwa kwenye ubora wao tunaoufahamu. Inashangaza kushangaa Valverde kuwa kocha wa Barcelona.