Timu ya Mkoa wa soka ya Ilala jana ilikata tiketi ya kucheza nusu fainali katika mashindano ya Kombe la Taifa baada ya kuichapa Pwani 2-0 katika mchezo wa kiporo ulioahirishwa juzi kufuatia giza kutanda uwanjani.
Ilala inaendelea kupeta katika `Jumba la Big Brother`, ambapo sasa itakumbana na Arusha katika mchezo wa nusu fainali utakaofanyika kesho, huku Pwani wakiondolewa katika jumba hilo na kurejea kwao.
Mchezo huo ulichezwa juzi kwa dakika 116 na ulisimamishwa baada ya giza kutanda na hadi mpira huo unaahirishwa, timu zote zilikuwa hazijafungana.
Katika mchezo wa jana ulioanza saa tisa, Ilala ilipata bao lake la kuongoza katika dakika ya 46 lililofungwa kwa kichwa na Mohamed Kijuso akiunganisha wavuni kona iliyochongwa na Salum Kanoni.
Pamoja na kuzidiwa kimchezo, Ilala ilitumia vizuri uzoefu wa wachezaji wake na kuandika bao la pili dakika mbili baadae lililowekwa kimiani na Athumani Machupa baada ya Greyson Haule wa Pwani kutoa pasi mbovu ya nyuma iliyonaswa na Machupa aliyefunga bao hilo.
Kocha wa Ilala Jamhuri Kuhwelo alisema baada ya mchezo huo kuwa hakushangazwa na matokeo hayo kwani aliyatarajia.
Alisema kuwa timu yake haitakuwa na mapumziko na leo itaendelea na mazoezi ili kujiweka tayari kuikabili Arusha katika mchezo wa nusu fainali utakaofanyika kesho.
Naye kocha wa Pwani, Fred Felix Minziro alisema kuwa amekubali matokeo lakini amesikitishwa na TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, kushindwa kuuanza mapema mchezo wa juzi hadi kusababisha giza kuvunja pambano.
Alisema kuwa kwanini TFF wasingeuanza mchezo huo mapema kama walivyofanya ule wa jana ili kuhakikisha giza halitibui mchezo huo.
Hatahivyo, nje ya uwanja mchezo huo ulitawaliwa na ghasia katika jukwaa la kijani kutokana na upinzani wa Simba na Yanga na kusababisha mashabiki kurusiana chupa zilizojaa mkojo, mawe na maganda ya machungwa.
Wakati huohuo, timu ya Mkoa wa Mbeya, Mapinduzi Stars, leo itashuka kwenye Uwanja wa Taifa kucheza na Kinondoni katika mchezo wa kusaka tiketi ya kucheza nusu fainali.
- SOURCE: Nipashe