Menu
in

Huu ni mwisho wa utawala wa La Liga duniani?

Washabiki wengi wa Hispania wamepigwa butwaa. Wanajiuliza huu ni mwisho wa  kutamba kwa La Liga katika mashindano na tuzo za wachezaji bota barani Ulaya  na duniani? Sababu mshindi wa tuzo ya mchezaji bora duniani wa FIFA mwaka  2020 kwa mara ya kwanza hachezi Ligi ya Hispania.  

Mshindi huyo ni Robert Lewandowski mchezaji wa klabu ya Bayern Munich ya  Ujerumani, yenye Ligi maarufu kwa jina la BundesLiga. Bayern Munich ndiye  bingwa wa Ulaya. Lewandowski ameibuka mshindi wa tuzo ya FIFA mwaka huu kwa upande wa wachezaji wanaume na kuwapiga kumbo mastaa wawili mahiri  Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. 

Ushindi wa Lewandowski umehitimisha ubabe wa wachezaji wa La Liga kutamba katika tuzo za Ulaya na duniani. Hadi mwaka huu 2020, wachezaji wa La Liga  walikuwa wanatamba katika tuzo za FIFA tangu ilipoanzishwa mwaka 2016. 

La Liga
La Liga

Cristiano Ronaldo alitwaa tuzo hiyo mwaka 2016 na 2017, kabla ya Luka Modric  na Lionel Messi kutwaa katika miaka miwili iliyofuata, 2018 na 2019. Lakini  Lewandowski alifunga mabao 55 katika mechi 47 msimu uliop[ita na kuthibitisha  angekuwa mshindani wa wachezaji wa La Liga na manguli Messi na Ronaldo. 

Ushindi wake umeleta hadhi nyingine kwa BundesLiga, akiwa ametwaa mataji ya  DFB Pokal,DFL-Super Cup,Ligi ya Mabingwa Ulaya na UEFA Super Cup. 

Tangu alipowasili klabu ya Bayern Munich, Lewandowski ana rekodi ya kipekee  klabuni hapo na haitakuwa rahisi kulinganishwa na mshambuliaji mwingine wala  nchini kwao Poland. 

Ukweli ni kwamba, Lewandowski amekuwa mchezaji mwenye utajiri wa mabao  na kipaji. Amefunga mabao 264 na kupika mengine 62 kwa viggo hao wa  BundesLiga, ikiwa na maana na wastani wa mabao 40 kwa kila msimu.  

Kuwa mfungaji bora wa Bundesliga akiwa ametupia wavuni mabao 34 katika  mechi 31, kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kufunga mabao  15 katika mechi 10 msimu uliopita 2019/2020, bado inategemewa atafunga  mengine msimu huu. Uwezekano huo umeonekana msimu huu tena 2020/2021.

Msimu huu 2020/2021 amepachika wavuni mabao 18nkatika mechi 11 alizochezea  Bayern Munich pamoja na kutengeneza mengine 11. Hesabu hizo ni pamoja na  mabao manne ya Ligi ya Mabingwa. Hadi sasa bado mshambuliaji huyo amekuwa  mwiba Bundesliga na barani Ulaya. Kasi ua ufungaji wake imekuwa ya kusisimua.  Uwezo wa kupachika mabao hakuanza kuonesha akiwa Bayern Munich, bali akiwa  mchezaji nambari moja wa mabao kwa wapinzani wao wa jadi Borrusia Dortmund. 

Hii ina maana ikiwa kasi hii itaendelea hadi mwisho wa msimu huu upo  uwezekano akaibuka kuwa mfungaji bora wa Ulaya kuanzia lugi ya Ujerumani  hadi Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mabao yake yanaweza kuleta taji lingine la  Bundesliga na Ligi ya Mabingwa Ulaya hali ambvayo itakuwa inaua kabisa ubabe  wa La Liga. 

Kasi ya wababe wa La Liga imeshuka kwa kiasi kikubwa, na hakuna mshambuliaji  anayefumania nyavu kumzidi Lewandowski huko Ujerumani. Si Luis Suarez wa  Atletico Madrid, wala Lionel Messi pale Barcelona. Au Karim Benzema pale Real  Madrid. Hakuna washambuliaji wa Valencia,Atletico Bilbao, Real Sociedad wala  Villareal ambao wanaweza kulinganishwa na Lewandowski kwa upachikaji wa  mabao. Kupotea kwa washambuliaji hao kuna maana kuwa La Liga imeshindwa  kutamba hadi mwezi Desemba unapoekelea ukingoni. Hakuna dalili za  washambuliaji au wachezaji wengine kufuata kasi ya Lewandowski katika  upachikaji wa mabao. 

Kukosekana kwa washindani katika La Liga ina maana Bundesliga wanakuwa na  wana nafasi kubwa ya kuibuka na tuzo ya FIFA msimu huu pia. Kwa sababu upo  uwezekano timu ya Ujerumani kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya hali ambayo  itazikosesha nafasi timu za La Liga. 

Chukulia mfano kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Chelsea na  Sevilla. Kipigo walichokipata Sevilla nyumbani cha mabao 4-1 ni kielelezo cha  kutetereka kwa La Liga katika ushindani wa soka barani Ulaya. 

Real Madrid haina safu kali ya ushambuliaji, bado inamtegemea Karim Benzema,  hivyo wanaofuata kama vile Luka Jovic na Mariano Diaz hawajafikia hata robo ya  uwezo wa Mfaransa huyo hali ambayo inaashiria hawawezi kuwa washindani wa Lewandowski barani Ulaya.

Cristiano Ronaldo yuko Juventus, akikiongoza kikosi chake kuwazaba mabao 3-0  Barcelona waliokuwepo nyumbani kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kipigo hicho nacho kilikuwa na ujumbe kuwa timu za La Liga zimekuwa vibonde  barfani Ulaya ambapo zimefungwa mechi nyingi msimu huu. 

Kama Lionel Messi ameshindwa kufurukuta mbele ya Lewandowski ni mchezaji  gani mwingine wa La Liga anaweza kujaribu kumkaribia Mpolishi huyo? Ni nyota  yupi mwingine anaweza kuiwakilisha La Liga katika ushindani wa tuzo barani  ulaya kwa sasa? Jibu linakuwa rahisi tu, ni Lionel Messi.  

Kwahiyo akishindwa Lionel Messi maana yake hakuna mwingine mwenye uwezo  huo. Ndiyo kusema La Liga imetetereka na kudorora kiasi kwamba hakuna  miamba ya kutikisha tena barani Ulaya. 

Ingawaje timu za Sevilla, Atletico Madrid, Real Madrid na Barcelona zimefuzu  hatua ya 16 mtoano Ligi ya Mabingwa bado uhakika wao kushinda hautabiriki.  Viwango vilivyooneshwa msimu huu vinaashiria ukame wa ushindani kutoka La  Liga. Hakuna aliyefikisha mabao ya Lewandowski hadi sasa, na inaelekea huenda  akatamba tena msimu huu. Hapo ndipo linapokuja swali la msingi, je huu ni  mwisho wa utawala wa La Liga? Tusubiri na kuona mwishoni mwa msimu huu.

Written by Mark Mpangala

*Markus Mpangala ni Mhariri, Mwandishi wa Makala Maalumu, Mwanahabari,Mwanablogu,Mwanafasihi na Mwanasafu, ambapo kwa kipindi cha miaka 12 amefanya kazi katika vyombo vya habari mbalimbali vikubwa na vidogo nchini Tanzania katika Michezo, Siasa, Elimu na utalii. Pia ni mchambuzi mchangiaji wa masuala ya siasa na utawala bora katika idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC SWAHILI). Ni mhariri na mhamasishaji wa usomaji wa vitabu*

Leave a Reply

Exit mobile version