Hodgson ajipalia mkaa kwa Rio Ferdinand
Kocha mkuu wa timu ya taifa ya England, Roy Hodgson amejipalia mkaa kwa kumbeza mchezaji maarufu, Rio Ferdinand.
Hodgson ambaye amekuwa akikataa kumwita kikosini beki huyo mahiri wa Manchester United, akimpendelea zaidi Jon Terry wa Chelsea.
Baada ya Terry kujiuzulu kuchezea England, wengi walidhani ni wakati mwafaka kwa Rio kuchukua nafasi yake, Hodgson amemfungia tena vioo.
Kilichomzushia balaa Hodgson ni safari yake kwenye treni ya chini ya ardhi, ambapo alijikuta akizungumza masuala ya Rio humo, kwa kujibu watu maswali.
Inadaiwa alisema kwamba huu ndio mwisho wa Rio kuchezea timu ya taifa ya England, baada ya abiria mwenzake kumtupia swali hilo muhimu, pengine kwa mtego.
Hodgson amekimbilia kumwomba radhi Rio kwa kujadili suala lake kwenye treni, lakini anakana kusema Rio hataliwakilisha tena taifa.
Anakiri kwamba aliwaambia wasafiri kwamba mlinzi huyo mwenye umri wa miaka 34 hangekuwapo kwenye kikosi chake cha sasa, ikiwa ni siku moja kabla ya kukitangaza.
“Nimesikitishwa kwamba habari kama ile imechapishwa na namwomba (Rio) radhi.
Hodgson alimwaga siri za kikosi chake wakati akisafiri kwenda uwanja wa Emirates Jumatano kwa ajili ya kushuhudia mechi ya Klabu Bingwa Ulaya katika hatua za makundi kati ya Arsenal na Olympiakos, ambapo Washika Bunduki wa London waliwafyatua Wareno hao kwa mabao 3-1.
“Inanibidi tu niseme kwamba ndio basi tena kwake kuchezea England. Ndio mwisho wa safari yake,” Hodgson amekaririwa na gazeti akisema hivyo kumhusu Rio mwenye uhasama na Terry.
Itakumbukwa kwamba, Hodgson alimwita Terry hata pale alipokuwa na kesi ya kumkashifu kibaguzi Anton Ferdinand, ambaye ni mdogo wake Rio, huku baadhi ya watu wakiona Rio angekuwa mwafaka kucheza kwa vile Terry alishachafuka kwa tuhuma.
Terry alijitoa kwenye timu ya England baada ya Chama cha Soka (FA) cha England kung’ang’ania mashitaka dhidi yake, na hatimaye kumtia hatiani, kumfungia mechi nne na kumtoza faini ya zaidi ya pauni 200,000.
Lakini Hodgson alipoulizwa baadaye na waandishi wa habari kuhusu kumng’ong’a Rio, alikuwa na haya ya kusema:
“Bila shaka yoyote, sikusema kwamba ndio mwisho wa Rio…ninachokumbuka ni kuzungumza na watu wengi tu kwenye treni ile na mtu mmoja akasema;
‘Je, Rio yupo kwenye kikosi kijacho?’ nadhani nilichomjibu ni; ‘sidhani’…sikusema zaidi ya hapo nadhani.
“Hata hivyo, bila shaka sikutakiwa hata kusema hivyo. Hilo ni kosa na natakiwa kuomba radhi kwa hilo. Hii ni moja ya kasheshe ninazowaziaga juu ya kusafiri kwenye treni.
“Lakini treni ndiyo njia yangu rahisi zaidi ya kuja London – halafu unapata fursa ya kuzungumza na watu ambao wanakuwa wanakuuliza maswali, badala ya kukaa umefumba mdomo wako muda wote.
“Nimegharimika kwa hili, nitakuwa makini zaidi siku zijazo na ni funzo pia kwa watu wote wanaoniona kwenye treni. Kwa hiyo msiudhike snaa nikikataa kujibu maswali mtakayoniuliza.”
Hayo ndiyo yamemkuta Hodgson, wakati kikosi cha England kikiandaliwa kwa ajili ya michezo ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya timu za taifa za San Marino na Poland.
Mabeki wapya walioitwa kikosini ni Kieran Gibbs wa Arsenal na Ryan Shawcross wa Stoke City.