*Cameroon wachapwa 4-0
*Uholanzi waingia 16 bora
Mabingwa watetezi, Hispania, wametema Kombe la Dunia baada ya kuaibishwa na Chile kwa kufungwa 2-0.
Wakati Diego Costa na Sergio Busquets walipoteza nafasi za wazi za kufunga, kipa Iker Casillas alifanya tena makosa kwa kusababisha moja ya mabao mawili aliyofungwa.
Utawala wa Hispania kwenye soka ya dunia ulifikishwa ukingoni pasipo kutarajiwa, baada ya Chile kuendeleza kichapo baada ya Hispania kuwa wamefungwa 5-1 na Uholanzi kwenye mchezo wa kwanza.
Hispania ambao pia ni mabingwa wa Ulaya walikuwa wakijaribu kuwa taifa pekee kutetea ubingwa wa dunia tangu Brazil walipofanya hivyo 1962.
Hispania walitwaa ubingwa wa Ulaya 2008, Kombe la Dunia 2010 na Ulaya tena 2012.
Mabao ya Chile yalifungwa katika kipindi cha kwanza kwenye uwanja maarufu wa Maracana kupitia kwa Eduardo Vargas na Charles Aranguiz.
Maswali mengi yanabaki juu ya hatima ya kimataifa kwa kocha Vincente Del Bosque na wachezaji wake aliowaamini sana kama Xabi Alonso, Xavi na Casillas.
Del Bosque alijaribu kuokoa jahazi kwa kumtoa Xavi, kumsogeza David Silva mbele na Pedro akaenda kulia kwa vile ni mdogo na ana kasi lakini haikusaidia.
Gerard Pique naye aliwekwa kando kwenye ulinzi badala yake Javi Martinez akasaidiana na Sergio Ramos.
CAMEROON HOI, NIDHAMU MBOVU
Cameroon wameaga fainali za Kombe la Dunia baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Croatia.
Walianza kuruhusu bao katika dakika ya 11 mfungaji akiwa ni Ivica Olic na muda mfupi kabla ya mapumziko wakabaki wachezaji 10.
Alex Song alizawadiwa kadi nyekundu baada ya kuonyesha ukosefu wa nidhamu dhidi ya Mario Mandzukic wa Croatia.
Ivan Perisic alifunga bao la pili baada ya kipa Charles Itanje kucheza vibaya mpira na Mandzukic akatiala tatu kabla ya kufuga kitabu kwa jingine la nne.
Croatia wanaofundishwa na Niko Kovac watakabiliana na Mexico kwenye Kundi A ambapo wakishinda watajihakikishia kusonga mbele.
Cameroon waliocheza bila nahodha wao majeruhi, Samuel Eto’o wanasubiri kukabiliana na wenyeji Brazil katika mechi ambayo Brazil watatakiwa kushindwa ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.
Cameroon ni timu ya kwanza kupoteza mechi sita mfululizo katika fainali za Kombe la Dunia tangu El Salvador walipoweka rekodi hiyo 1982.
Dakika za mwisho ziliwaongezea Cameroon aibu, kwani beki wao, Benoit Assou-Ekotto alitaka kuzichapa na mwenzake, Benjamin Moukandjo kabla ya kutenganishwa na mwenzao.
Mjomba wa Alex, Rigobert Song amepata kupewa kadi nyekundu mbili kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Cameroon waligomea kupanda ndege kwenda Brazil kabla ya kulipwa posho walizokuwa wakidai, hivyo watatakiwa kuboresha nidhamu yao kama wanataka kulinda heshima ya soka iliyokuwa juu sana miaka ya nyuma.
UHOLANZI WAFUZU KWA MTOANO
Uholanzi wamevuka hatua ya makundi baada ya kutishwa na Australia kwenye mechi kali ya Jumatano hii.
Alikuwa Memphis Depay aliyewahakikishia ushindi baada ya kuwa sare ya 2-2. Arjen Robben wa Uholanzi alifunga bao la kuongoza kabla ya Tim Cahill soon kusawazisha kwa mpira safi.
Australia walitangulia baada ya Mile Jedinak kufunga kwa penati lakini Robin van Persie akasawazisha na kufanya mambo kuwa 2-2.
Mathew Leckie alikosa bao la wazi kuwaweka Australia mbele na Depay hakufanya ajizi kutikisa nyavu kutoka umbali wa yadi 25 dakika 22 kabla ya mechi kumalizika.