*Hispania: Soka yapoza madhila ya uchumi
Mwaka 2012 umekuwa mchungu kwa Hispania, nchi iliyokumbwa na mtikisiko mkubwa wa uchumi.
Hali hiyo ilitanda nchi nzima, hivyo kwamba si rahisi kufungua televisheni au kusikia majadiliano bila kutajwa msukosuko huo wa kiuchumi.
Ukosefu wa ajira umekua kwa kiwango kikubwa, benki zinakwama kujiendesha, serikali inapunguza ruzuku na posho iliyokuwa ikitoa kwa wananchi, ambao wanaijibu kwa kuipinga kwa maandamano mitaani.
Serikali ilishapata msaada wa Umoja wa Ulaya (EU) kuikwamua nchi kwenye madeni na hali tete ya uchumi, lakini bado hali si nzuri na msaada zaidi wa jumuiya hiyo unahitajika, japokuwa haijulikani kama utatolewa.
Soka Yageuka Liwazo kwa Taifa
Katikati ya hali hiyo tete na giza, hata hivyo, kuna liwazo moja kubwa na muhimu kwa watu wengi wa taifa hilo linalopenda michezo, liwazo hilo ni mafanikio ya soka.
Julai mwaka jana, Hispania iliweka historia kwa kuwa timu ya kwanza ya kimataifa kutwaa vikombe vitatu mfululizo katika mashindano makubwa.
Hispania iling’ara kwenye kombe la Euro mwaka 2008, ikatwaa Kombe la Dunia la Fifa mwaka 2010 kabla ya kufunika kwa kutwaa tena lile la Euro mwaka jana.
Yote hayo yalikuwa tisa, kwani kumi ni pale timu hiyo inayofundishwa na Mhispania Vicente Del Bosque ilipotwaa ushindi kwa staili ya aina yake, kwa kuwanyuka Italia mabao 4-0 kwenye fainali.
Ushindi huo na utwaaji makombe kwa ujumla, umewaweka katika daraja la juu, na sasa timu ya taifa ya Hispania inatajwa kuwa ya kiwango kikubwa zaidi kimataifa katika soka enzi zote.
Taifa linatamba na raia wake wenye vipaji visivyo vya kawaida na ufundi kwenye soka, kama akina
Xabi Alonso, Xavi Hernandez, Andres Iniesta na David Silva.
Hata wasioijua vyema soka au wasiotazama mechi kila mara, wamevutwa na wachezaji hao na timu ya taifa kiasi cha kuachwa midomo wazi wakiona mtiririko wa pasi, ufundi wa chenga na umaliziaji kwa kupachika mabao ya kiwango cha juu.
Miguel Angel Aguirre, ana uelewa mkubwa wa maoni ya umma, kwa sababu yeye ni mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya kimataifa ya uhusiano wa umma iitwayo Edelman yenye makao yake makuu jijini Madrid.
Huyu anakiri kwamba katikati ya mazonge yote hayo, hisia za taifa zilisuuzwa na ari kupandishwa na vitu visivyo vya kawaida vya wanasoka wake msimu ule wa kiangazi.
“Kwa kiwango kikubwa sana soka ndio mchezo unaopendwa zaidi hapa Hispania, na kwa kweli wengi wana hisia za hali ya juu kwamba wanaimiliki La Roja, timu yetu ya taifa.
“Mafanikio ya timu hii yamewasaidia watu kusahau matatizo haya ya uchumi, hata kama ni kwa muda mfupi. Wachezaji walikuwa kwenye shinikizo kubwa, wakafanikisha kazi wakaja kufanyiwa sherehe kubwa.
“Maelfu ya watu walijitokeza na kuwa pamoja kutazama fainali zile kwenye skrini kubwa ya televisheni iliyowekwa Paseo de la Castellana, moja ya mitaa mikubwa kabisa ya Madrid, na mandhari yale hayakuwa ya kawaida,” anasema Aguirre.
La Liga Matawi ya Juu
Hata hivyo, kutamba na kufanikiwa kwa soka si katika timu ya taifa tu, kwani ligi ya nyumbani, yaani La Liga, ni maarufu sana, inapendwa nyumbani na inafuatiwa na wengi.
La Liga imejisimika kama moja ya ligi zinazopendwa zaidi duniani, ikishika nafasi ya pili tu baada ya England, Premier League.
Nchini Hispania, ligi hiyo ni ya kiwango cha juu, ambapo kuna pambano lisilokuwa la kawaida linaloitwa El Clasico – yaani mtifuano baina ya vigogo wawili – Barcelona na Real Madrid, timu zenye mkusanyiko wa wachezaji nyota kutoka pande zote duniani.
Hapa ndipo wapo namba moja na namba mbili wa soka kimataifa, yaani raia wa Argentina, Lionel Messi anayekipiga Barcelona na Cristiano Ronaldo anayemfuatia, akichezea Real Madrid; hawa wanavuta hisia za dunia yote.
Pamoja na kuwa taifa moja, kuna hisia za umajimbo zinazozidi kustawi kisiasa na kijamii, na pia kuingia kwenye michezo.
Uzalendo wa Catalans Waligawa Taifa
Hali hiyo inafanya baadhi ya watu, kwa mfano kutoka eneo la Catalonia, kutoiunga mkono moja kwa moja timu ya taifa, licha ya kwamba humo kuna wachezaji wanaotoka Catalonia.
Hili ni eneo ambalo lina uhuru kiasi na watu wake hujichukulia kuwa huru kutoka Hispania, wakijiita Catalans. Huko ndiko ipo klabu bingwa ya Hispania, Barcelona.
Maeneo mengine katika jimbo hilo la kaskazini mashariki ni Girona, Lleida na Tarragona. Kwa hiyo sherehe za timu hiyo huwa na ukungu kidogo kwa sababu ya watu hawa, lakini huishabikia vilivyo Barcelona.
Ukuaji wa hisia za uzalendo na tamaa ya kujiundia taifa lao kwa watu wa catalonia zilisababisha baadhi ya watu katika jimbo hilo kutoshangilia ubingwa wa Euro mwaka jana.
“Watu wengi hapa hawaipendi timu ya taifa, wanaona hawana maslahi nayo. Kinachosaidia kidogo ni uwapo wa wachezaji kadhaa kutoka Barcelona huko.
“Namba moja, mbili na tatu kwa watu wa hapa ni Barca, Barca, Barca. FC Barcelona ndiyo timu yetu ya taifa kwa Catalonia yote, wala si hapa Barcelona tu,” anasema Tomas Obrado Cugat, mkazi wa Catalonia ambaye ni mpagazi jijini Barcelona.
Pamekuwa na historia ya muda mrefu ya uhasama na chuki kati ya serikali kuu iliyoko Madrid na baadhi ya majimbo, hasa Catalonia na Basque.
Uchawi wa Messi na Fadhila kwa Taifa
Kuna watu wanaosema kwamba uchawi wa Messi klabuni Barcelona ungeweza kupunguza mvutano na uhasama uliopo kwenye soka ya Catalonia.
Hata hivyo, mwishoni mwa Mei mwaka jana, katika fainali ya Kombe la Taifa kati ya Barcelona inayotoka Catalonia na Athletic Bilbao wanaotoka Basque palitokea maajabu.
Katika mechi iliyochezwa makao makuu ya nchi, Madrid, washabiki walionyesha uhasama mkubwa tangu wakati wakiingia uwanjani, na kuzomea na kupiga miluzi wakati wimbo wa taifa ukiimbwa.
Ukuaji wa watu kutaka kujitenga kimaeneo umetokana na matatizo ya kiuchumi, ambapo serikali kuu ya Madrid inaondoa misaada yake kwa raia, nao wanadhani serikali za majimbo zitawajali.
Catalonia kwa upande wake, inaamini kwamba ikijitenga itaweza kujiendesha vizuri na kuwasaidia watu wake, kwa sababu klabu ya Barcelona ambayo ndiyo ya pili kwa utajiri duniani, itazalisha na kuwaingizia fedha nyingi sana.
Kwa sasa wanachukizwa na kile wanchodhani kwamba ni fedha zao zinazozalishwa na vijana wao wa Barcelona kupelekwa serikali kuu inayoyumba ya Madrid kuinusuru kiuchumi.
Miezi michache iliyopita imeshuhudia ukuaji wa vuguvugu linalotaka kuundwa kwa serikali huru ya Catalonia .
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba mwaka jana wengi walivipigia kura vyama vilivyoahidi kura ya maoni ili kutoa uhuru kwa jimbo hilo.
Serikali kuu ya Madrid, hata hivyo, ilishaonya na inashikilia kwamba hatua kama hiyo ni batili kisheria.
Klabu ya Barcelona nayo imekuwa kana kwamba imeongeza mafuta kwenye moto mkali, kutokana na jinsi ilivyoanza La Liga kwa kishindo.
Katika mechi 15 za kwanza walijikusanyia pointi nyingi ambazo hakuna timu iliyopata kuzifikia katika historia ya La Liga .
Watu Hawataishi kwa Soka Pekee
Japokuwa timu hii inayopendwa zaidi imechochea furaha kwa Catalans, na wale wengine kitaifa, watu wanatakiwa kujua kwamba soka pekee haiwezi kuikomboa nchi, ina ukomo wake.
Culgat anasema kwamba watu wengi nchini Hispania wana matatizo makubwa na wapo wasiojua hata watakula nini ‘kesho’. Pamoja na umuhimu wa soka kwao, lazima wajue mchezo huo hautawalisha.
Pengine ni wakati mwafaka sasa kwa EU kuiokoa nchi kwenye madhila yake ya kiuchumi, na wananchi kuelewa umuhimu wa makato ya mafao waliyokuwa wakipata, wajitume zaidi kwenye kazi, ili kuweka msingi wa uchumi imara na endelevu.