MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Afrika inatarajiwa kunguruma mwaka 2025 nchini Morocco. Ni michuano mikubwa sana Afrika na duniani. Hiyo ndiyo sehemu ambao kila nchi inatamani kupata fursa ya kuonesha uwezo,vipaji na uongozi wa michezo. Tanzania ni miongoni mwa Mataifa ambayo yatashiriki kwenye mashindano ya AFCON na kuwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki.
Hata hivyo TANZANIASPORTS imebaini kuwa suala la waamuzi wa mchezo wa soka katika Ligi Kuu Tanzania linatakiwa kutiliwa mkazo na uongozi unapaswa kuchukua hatua madhubuti. Wakati Afrika na Dunia inasubiri mashindano ya AFCON kumekuwa na jambo la kusikitisha kuhusiana na waamuzi wa Tanzania. Kwa muda mrefu waamuzi wa soka Tanzania wamelalamikiwa kwa maamuzi wanayochukua dimbani.
Kumekuwa kelele nyingi sana kuhusiana na uwezo wa waamuzi kuzingatia weledi wa kazi yao. Katikati ya malalamiko hayo tumeona waamuzi wa kitanzania kama vile Peter Komba na Ahmed Aragija wakipata nafasi kuchezesha michezo mbalimbali ya soka ya CAF. Hata hivyo CAF wameonesha wazi kutoridhishwa na waamuzi kutoka Tanzania kutokana na orodha yao. Hivi karibuni shirikisho la soka lilitoa orodha ya waamuzi watakaoshiriki kozi ya maandalizi ya fainali za AFCON mwakani nchini Morocco.
Waamuzi 32 bila Watanzania
Waamuzi wanapoteuliwa kuchezesha fainali za AFCON wanawakilisha weledi na umahiri wa Ligi za nyumbani kwao. Vilevile wanawakilisha umahiri wa CAF katika kusimamia waamuzi wenye ubora. Kati ya waamuzi 33 walioteuliwa na shirikisho la soka CAF hakuna mwamuzi kutoka Tanzania. Ndiyo kusema kati ya waamuzi wote wanaotumika katika Ligi Kuu Tanzania hawajakidhi vigezo vya kuchezesha mashindano ya AFCON. Katika mazingira haya unapoona orodha hii lazima inakugusa na kuuliza kuna kitu gani kinachochangia waamuzi wa Tanzania kutoteuliwa kuchezesha AFCON. Licha ya kupewa mechi kadhaa za ngazi ya vilabu na mataifa mbalimbali hatua ya kufuzu bado hali ya waamuzi wa Tanzania haijabadilika. Taswira ya waamuzi wa Tanzania inazidi gizani. Ni wajibu wa viongozi kuhakikisha jambo hili linachukuliwa hatua na kutafutiwa ufumbuzi.
Waamuzi wasaidizi 33 AFCON
CAF katika orodha yake imebainisha kuwa waamuzi wasaidizi watakuwa 33 na ambao wamtokea mataifa mbalimbali. Katika nafasi ya kwanza ya waamuzi wa kati 32 unaweza kusema huenda ni ushindani mkali wa viwango vya waamuzi ndiyo maana wale wa kutoka Tanzania hawajapata nafasi. Hali kadhalika wale wa waamuzi wasaidizi 33 nako hakuna hata moja kutoka Tanzania. Ukiangalia nafasi ya waamuzi wa kati na wasaidizi unagundua kuwa jumla ni 65. Kwa maana hiyo Tanzania imeshindwa kuzalisha waamuzi wa kati na wasaidizi katika fursa ya waamuzi 65. Kama taifa lazima jambo hili kulifikiria na kutafuta suluhisho la kwanini hakuna waamuzi wa ligi Kuu Tanzania katika nafasi 65 za AFCON.
Ligi Kuu Tanzania bila VAR
Kwenye orodha ya waamuzi wa CAF kuna maeneo makuu matatu; eneo la kwanza linahusisha waamuzi wa kati ambao wapo 32. Eneo la pili ni waamuzi wasaidizi ambao wapo 33. Eneo la tatu ni waamuzi wa VAR ambao ni wanne. Waamuzi hao ni wachache na wameonesha umuhimu wa teknolojia ya VAR. Ligi Kuu imekuwa na malalamiko kadhaa kutoka kwa walimu na wadau wa mchezo huo kutokana na uwezo wa waamuzi. Kwa maana hiyo hali iliyopo sasa inashawishi kuandaa waamuzi wenye uwezo wa kutumika katika VAR. kwahiyo Tanzania imekosa nafasi jumla 69 za kuwa waamuzi wa AFCON. Ni lazima tujikague kwanini fursa hii haipo kwa waamuzi wa Tanzania. Hili ni jukumu la vyama vya waamuzi na TFF kulikwamua taifa kutoka katika aibu hii. Inakubalika kuwa sio kila nchi inapeleka waamuzi lakini haifurahishi kukosa kabisa nafasi. Je ni lini tutawaandaa marefa wetu kutumia teknolojia ya VAR? ama tupo tayari kupitwa na teknolojia hii ambayo inasaidia waamuzi wa nchi zingine hadi kupewa fursa ya kuongoza mafunzo na usimamizi wa fainali hizo.
Ukanda wa CECAFA
Pengine tunaweza kudhani waamuzi wengi wanatoka nchi za Afrika kaskazini lakini takwimu zinaonesha hata nchi jirani zimefanikiwa kuwa na waamuzi kwenye mashindano ya AFCON 2025. Katika nafasi ya waamuzi wa Kati;- Peter Waweru Kamaku (Kenya)Pacifique Ndabihawenimana (Burundi), Mahmoud Ali Mahmood (Sudan), Omar Abdulkadir Artan (Somalia) na Samuel Uwikunda (Rwanda). Upande wa waamuzi wasaidizi; Gilbert Cheriyot (Kenya),Ibrahim Abdallah Mohammed (Sudan), Yiembe Stephen (Kenya) na. Ukitazama orodha zote mbili unaona Tanzania imewaacha mbali sana kwenye msisimko na ubora wa Ligi ya soka kwneye ukanda huu, lakini hakuna mwamuzi hata mmoja wala msaidizi aliyeteuliwa kutoka Tanzania. Hili si jambo la kufurahia kabisa. Ni wakati wa kuangalia namna bora ya kuibua waamuzi wazuri na kuendeleza kuipa thamani Ligi Kuu Tanzania.