Madhaifu ni jambo la kawaida kwa mwanadamu, wanadamu wote tumeumbwa tu
wadhaifu. Hakuna mkamilifu katika uso wa huu wa dunia.
Dunia yenyewe haijawahi kukamilika hata siku moja hivo ni ngumu kwa
vilivyomo ndani ya dunia kukosa madhaifu.
Kuwa na madhaifu siyo dhambi au kosa, kosa na dhambi huja pale
unaposhindwa kuyastiri madhaifu yako na kuyaonesha waziwazi mbele ya
macho ya watu.
Wanaume wengi tumeumbiwa hulka ya kutamani wanawake , hii ni hulka
iliyopo ndani yetu ambayo tumeikuta ikiwa kwenye miili yetu, hivo siyo
kosa letu kubeba hulka kama hii kwa sababu imewekwa makusudi kupima
ukomavu wetu wa kuhimili tamaa ya kutamani wanawake.
Kosa kubwa huja pale tunaposhindwa kuhimili tamaa hii na kuamua
kufanya vitu ambavyo vitaonesha madhaifu yetu waziwazi kwenye jamii na
kujishushia heshima.
Mpangilio wa vitu kama maisha ni nguzo muhimu ya busara, busara huja
mwishoni mwa maamuzi yako lakini kabla ya hapo kuna vitu ambavyo
humbeba mtu aweze kufanya maamuzi ya busara. Maamuzi ambayo husaidia
kuficha madhaifu ya mwanadamu yoyote.
Kuna kitu hakipo sawa kwenye hili suala la uwanja wa kuchezea fainali
ya kombe la TFF na kinaanzia kwenye mpangilio mbovu wa shirikisho ƙla
soka Tanzania TFF hali iliyosababisha watoe maamuzi yasiyo na busara
kubwa, maamuzi ambayo yanazidi kuwafanya wajianike madhaifu yao wazi.
Hakukuwa na sababu yoyote kubwa ambayo imesababisha kwa shirikisho la
soka Tanzania kutotangaza mapema uwanja ambao ungefanyika kwa fainali
ya kombe la shirikisho.
Kombe la shirikisho la soka nchini ndiyo hutoa mwakilishi wa kombe la
shirikisho barani Afrika hivo heshima stahiki inatakiwa itoke kwenye
kombe hili ili kutoa bingwa ambaye ni mwakilishi mzuri katika michuano
ya kimataifa.
Tumekuwa tukiona kila msimu, UEFA hutangaza mapema uwanja ambao
utatumika kwa ajili ya fainali ya kombe la UEFA na hii inakuwa na
faida kubwa sana.
Mfano msimu huu fainali ya UEFA inachezewa Cardiff na hii imejulikana
mapema sana na imeipa nafasi hata mji wa Cardiff kujiandaa vizuri
kuanzia ndani ya uwanja mpaka nje ya uwanja.
Kuchezwa fainali katika eneo fulani huwa kuna faida kubwa kibiashara
kwani mji husika hunufaika na wageni ambao huja kwa ajili ya kuangalia
fainali ile hivo wafanyabiashara wa Hotel, mabus, na wengine hunufaika
sana.
Kuundaa mapema mji wa kuchezewa fainali kunatoa hata fursa nzuri kwa
wafanyabiashara kujiandaa vizuri na mapokezi ya wageni pia hata chama
cha soka cha mji husika kufanya maandalizi mazuri ya kuandaa fainali
hiyo.
Haikuwa na haja ya kuchelewesha hili jambo mpaka mwishoni raisi wa
shirikisho la soka Tanzania kuanza kutoa taarifa ambazo
zinajichanganya.
Mwanzoni alitoa taarifa kutakuwa na draw ya viwanja viwili ya Uwanja
wa Taifa ambao kimsingi Simba hutumia kama uwanja wake wa nyumbani,
pia na CCM Kirumba ambao Mbao hutumia kama uwanja wake wa nyumbani
Hii ni fainali, fainali ambayo ilitakiwa kuchezewa kwenye uwanja wenye
hadhi ya fainali kama uwanja wa Taifa. Uwanja ambao una miundombinu
bora kuanzia eneo la kuchezea mpaka taa, maliwatoni.
Kupeleka mchezo wa fainali inayotoa mwakilishi wa nchi katika
mashindano ya kimataifa katika uwanja ambao una eneo bovu la kuchezea
unatoa mazingira kupata mechi isiyokuwa na ushindani hali ambayo
tutatoa mwakilishi ambaye siyo mshindani.
Utapelekaje fainali kwenye uwanja ambao siyo bora wakati tuna viwanja
ambavyo ni bora kuzidi hicho? Uwanja ambao hauruhusu utaambaji mzuri
wa mpira ndani ya uwanja.
Tumeiandaa fainali hii kuwa fainali ya kawaida isiyokuwa na ushindani
wa kucheza soka na tutapata mshindi atakuwa kawaida hivo
kutuwakilisha kawaida katika mashindano ya kimataifa.
Martin Kiyumbi