Menu
in , , ,

HEKA HEKA ZA KOMBE LA DUNIA LA WANAWAKE CANADA 2015 ZATUELEZA NINI KUHUSU SOKA?

 
Michuano ya kombe la dunia la soka ya akina mama, Canada mwezi Juni 2015 itafanywa miji sita, Ottawa, Edmonton, Montreal, Vancouver,Moncton na Winnipeg na kushirikisha nchi 24.

Afrika itawakilishwa na Nigeria, Ivory Coast, Ghana na Cameroon. Kiasi hiki ni pungufu kuliko kile cha wanaume (32). Tofauti haziishi hapo maana juma lililopita wanawake walifanya mashtaka dhidi ya shirika la mpira la Canada (CSA) mahakama ya Ontario, mjini Canada.

Mashtaka yanapinga uamuzi wa CSA kuwa na viwanja vyenye majani ya plastiki na kudai “wanawaume hawawezi kufanyiwa hivyo.”

Mashtaka yanaongozwa na wachezaji mashuhuri na washindi wa Tuzo la Mchezaji Bora wa Mwaka, Nadine Angerer (Ujerumani) na Abby Wambach (Marekani). Hadhi yao ni sawa na ya washindi, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo. Hatua inadhihirisha uzito wa mgogoro unaoendelea kudai pia kwamba viwanja vya majani ya plastiki ni vya hatari kwa usalama wa wachezaji.

Akijibu mashtaka, Katibu Mkuu wa FIFA, Bwana Jerome Valcke, aliiambia BBC ipo mikakati kufanya mashindano yajayo ya wanaume katika majani ya plastiki.

Bwana Valcke : “Uamuzi huu wa Canada hautokani na fedha au tofauti za wanaume na wanawake bali jinsi mazingira halisi ya Canada yalivyo. Tunataka kuhakikisha viwanja viko katika hali nzuri kwa timu 24 zitakazoshiriki.”

Kwa kuwa mgogoro ulikuwa mkali, ilibidi FIFA isisitize pia kwamba mgogoro mwingine wa kombe la wanaume la Qatar mwaka 2022, unakabiliwa na hali ya hewa. Kutokana na joto kali la Mashariki ya Kati, wapo wanaotaka michuano ifanyike miezi ya baridi . FIFA imesisitiza lazima michezo ifanywe mwezi Juni na Julai, kipindi cha desturi ya mashindano na pia wakati wa mapumziko wa ligi mbalimbali ulimwenguni.

Kihistoria kila michuano ya kombe la dunia imekuwa na migongano ya kisiasa, kimipango au kifedha. Ila mgogoro wa Canada 2015 unamulika vile vile suala la jinsia katika michezo. Kutokana na namna wanawake walivyopiga kelele na kudai, “wanaume hawawezi kufanyiwa hivyo” inaonesha kinyongo na hasira za chini chini katika ulimwengu wa michezo ya wanawake.

Wakati mpira wa miguu ukivuma sana baada ya vita vikuu vya kwanza vya dunia hamasa ya mchezo ilikuwa sawa baina ya wanaume na wanawake. Miaka ya 1920 kwa mfano, viwanja vya soka vilijazana idadi sawa ya watazamaji iliyofikia 50, 000 kwa mechi. Hapa Uingereza mwaka 1921 mpira wa akina mama ulipigwa marufuku hadi Julai 1971.

Moja ya sababu zilizotolewa ni kwamba wanawake hawakuwa wakifanya kazi za nyumbani, walizorotesha familia na ulezi wa watoto.

Leo si kawaida kuona michuano ya wanawake ikijazana idadi sawa na ya wanaume.Utafiti uliofanywa na BBC , Oktoba 2014 ulibainisha vipato vya wanamichezo wa kike na wa kiume havilingani. Utafiti uliangalia michezo 35 ukabaini kuwa toka mwaka 2004, michezo 25 ikiwemo riadha, tennis na nyavu, hulipa sawa na wanaume lakini mingine kumi siyo sawa.

Ukiacha michezo isiyolipa sawa kuna ambayo hailipi kama mpira wa kikapu, ngalawa, rugby, magongo (hockey) na badminton. Baadhi ya mashindano ya ngumi na baiskeli huwalipa wanawake lakini anamichezo wa kike hutegemea kutangaza bidhaa za biashara. Tofauti zilizotajwa Kombe la Canada, 2015, ni sehemu ya mgogoro unaowapa usongo wanawake.
 

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Leave a Reply

Exit mobile version