Arsenal watakuwa wageni wa Barcelona kwenye mchezo wa marudiano wa hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya leo Jumatano.
Vijana hao wa Arsene Wenger wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa nyuma kwa mabao mawili baada ya kukubali kipigo cha 2-0 ndani ya Emirates wiki tatu zilizopita.
Pengine Barca ni timu tishio kuliko timu nyingine yoyote kwa sasa Ulaya. Arsenal watakuwa na kibarua kigumu jioni ya leo katika jaribio la kutimiza dhamira yao ya kupindua matokeo.
Hata hivyo kuna mambo matano yafuatayo yanayotakiwa kufanywa na Arsenal na ikiwa watafanikiwa kuyafanya kwenye mchezo wa kesho basi wataweza kuibuka na ushindi ambao pengine utatosha kuwaondosha Barcelona.
Kwanza Arsenal wanatakiwa kukabia juu yaani kuziba mianya ya walinzi wa Barca kusambaza mipira kwa Sergio Busquets. Busquets ni injini ya mfumo wa Barca na hivyo kwa vyovyote vile Arsenal wanatakiwa kumdhibiti.
Njia pekee ya kumdhibiti Busquets ni kuhakikisha hapokei mipira ya kutosha kutoka kwa walinzi vinginevyo umahiri wa kiungo huyo utawafanya Barca wasambaze mipira mingi mno kwa washambuliaji wao.
Athletic Bilbao walifanikiwa kuwaadhibu Barca 4-0 Agosti mwaka jana kwa kutumia mbinu hii ya kuwanyima nafasi walinzi wa Barcelona.
Jambo la pili ni kuepuka kukaa na mipira mara Barca wanapopoteza mipira hiyo wakati wanashambulia.
Hii ina maana ya kuepuka kupoteza mipira hiyo kwa kuwa Barcelona huwa hawajipangi kukaba baada ya kupoteza mipira. Huwa wanakaba mara moja ili kuwanyima wapinzani nafasi ya kutulia.
Hili litawasaidia Arsenal kutumia nafasi zitakazopatikana za kufanya mashambulizi ya kustukiza mara baada ya kuwapokonya mipira Barcelona.
La tatu ni kwamba Arsenal wanatakiwa kutilia umakini na kutumia vyema udhaifu wa Barcelona hewani. Krosi, mipira ya kona, na mipira ya adhabu inaweza kuwapatia Arsenal mabao ya vichwa.
Urefu wa Olivier Giroud unampa faida kubwa dhidi ya Javier Mascherano mwenye kimo cha kawaida kabisa. Giroud anatakiwa kupokea krosi za kutosha zitakazomwezesha kudhuru ngome ya Barcelona.
Pengine kutokana na Arsenal kupata kona moja pekee kwenye mchezo wa kwanza kule Emirates kuliwanusuru Barcelona na kuruhusu bao la kichwa.
Ila huenda kesho zinaweza kupatikana kona za kutosha na hivyo uwezo wa mipira ya hewani wa Giroud, Mertesacker, Paulista, Koscielny na wengine unaweza kuwaletea Barca madhara.
Kitu kingine muhimu ni kutumia vyema nafasi inayoachwa nyuma na Daniel Alves na Jordi Alba ambao mara nyingi husogea mbele zaidi wakishambulia.
Hapa nazungumzia matumizi ya mwendokasi wa Theo Walcott, Alexis Sanchez na wengine kwenye mianya ya pembeni inayoachwa wazi na walinzi hao wa pembeni wa Barca.
Ikiwa viungo wa Arsenal watafanikiwa kusambaza mipira ya kutosha kwa washambulizi wao wa pembeni wakati Alves au Alba wanapokuwa wamepanda, mwendokasi wa washambulizi hao unaweza kuwaletea madhara Barcelona.
Jambo la tano na la mwisho linalotakiwa kufanywa na Arsenal ni sala na maombi. Hili si tu kwa wachezaji wa ndani ya uwanja bali hata washabiki wanatakiwa kusali kwenye dakika zote za mchezo.
Hii ni kwa kuwa mambo yote niliyoyataja hapo juu ni rahisi kuwekwa kwenye maandishi na kuzungumzwa mdomoni lakini utekelezaji wake ndani ya Uwanja ni mgumu mno.
Sababu kubwa ya ugumu wa utekelezaji ni vipaji vya hali ya juu walivyo navyo wachezaji wa Barcelona. Unaweza kuwashinda kimbinu lakini vipaji binafsi vya wachezaji wa timu hiyo vikakuadhibu bila huruma.
Hivyo sala na maombi pia vinahitajika ili wachezaji wa Barcelona washindwe kutumia vyema uwezo wao binafsi hapo kesho.