Ni wazi sasa Gareth Bale anaondoka Real Madrid. Ni wazi msimamo wa Zinedine Zidane juu ya Bale ni uleule, hasa tukitazama mechi za 10 za mwisho msimu uliopita, Bale hakupewa nafasi ya kutosha kama Rodrygo Goes, Vinicius Junior, Lucas Vazquez na Eden Hazard. Bale hakuwa na msimu mzuri na mchango wake ulikuwa hafifu kutokana na uhusiano mbovu kati yake na Zinedine Zidane.
Ni wazi msimu mpya utamkuta Gareth Bale akiwa timu mpya. Kuna uwezekano pia akawa katika ligi mpya badala ya Hispania maarufu kama La Liga.
Ripoti zinabainisha kuwa Real Madrid ipo kwenye mchakato wa kumuuza winga huyo. Upo uwezekano wa Bale kujiunga na klabu za Manchester United au Tottenham kabla ya dirisa la usajili kufungwa Oktoba 4 mwaka huu
WASIWASI WA JULEN LOPETEGUI
Wakati Cristiano Ronaldo alipoondoka Real Madrid ilitegemewa Bale angekuwa kinara na kuibeba timu hiyo mabegani mwake. Chini ya kocha Julen Lopetegui hakukuwa na maajabu kutoka kwa Bale.
Majeraha ya mara kwa mara, na ufanisi mdogo ukasababisha mjadala kutanda juu ya umuhimu wake katika kikosi cha timu hiyo. Angalau Lopetegui alikuwa na msimamo wa kuhakikisha Bale anaanza kuliko kumpanga Vinicius Junior.
Uamuzi wa kumweka kando Vinicius Junior ulikuwa na sababu za kiufundi, lakini mabosi wa Real Madrid hawakutaka jambo hilo. Bale akapewa nafasi zaidi kama mchezaji mwenye uzoefu lakini hakuna jambo la ajabu alilofanya. Hapo ndipo nafasi yake ilianza kuyeyuka kwa uwazi zaidi.
UKALI WA SANTIAGO SOLARI
Solari alichukua jukumu la kocha Julen Lopetegui baada ya kutimuliwa klabuni hapo. Kocha huyu aliweka wazi juu ya kutaka kuwaondoa kikosinu wachezaji wenye uzoefu ambao hawakuwa kwenye kiwango bora. Miongoni mwao ni Gareth Bale na Marcelo. Nafasi za wakongwe hao zilichukuliwa na Vinicius Junior na Sergio Reguilon. Solari alibainisha kuwa wapo wachezaji ndani ya Real Madrid muda wao ulikwisha hivyo walipaswa kuondolewa. Bale alikumbana na wakati mgumu, hata alipopewa nafasi hakuwa na maajabu. Solari aliamua kuwaondoa Bale na Marcelo katika kikosi cha kwanza kwa nia ya kuwataka waimarishe uwezo wao. Solari alifanikiwa kutwaa taji la Klabu bingwa dunia, lakini naye hakudumu kutokana na mwenendo mbovu wa timu.
UJIO WA HAZARD NA RODRYGO
Real Madrid ilijiandaa na maisha bila Bale baada ya kuwasajili Vinicius Junior na Rodrygo Goes. Halafu, likaja suala la Zinedine Zidane kurudi katika benchi la ufundi la Real Madrid. Eden Hazard ni winga wa kushoto na kulia au mshambuliaji wa pili.
Rodrygo Goes kama ilivyo kwa Vinicius wote wanacheza winga wa kulia na kushoto. Hii ina maana wachezaji watatu walikuja kugombana namba na Gareth Bale. Rodrygo na Vinicius walianzia Castilla kabla ya kupata nafasi zaidi kikosi cha kwanza. Hiyo ina maana Bale alikutana na changamoti kutoka kwa Eden Hazard, Vinicius Junior, Rodrygo Goes na Luca Vazquez. Mchango wa wachezaji hao ndio uliondoa nafasi ya Bale kikosini. Haikuwa rahisi kwake kupata namba ya kudumu.
MSIMAMO WA ZIDANE
Mara baada ya kumalizika msimu wa 2017/2018, Zinedine Zidane alipendekeza Gareth Bale auzwe. Pendekezo hilo lilikuja wakati ambao Bale ametoka kupachika mabao mawili katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Liverpool.
Mabosi wa Real Madrid Florentino Perez na Jose Angel Sanchez hawakukubaliana na mpango huo. Wakati huo huo Zidane alifahamu Ronaldo anaondoka klabuni. Pendekezo la Zidane liliambatana na kufanyika mabadiliko katika kikosi hicho kwa sababu kilifika kileleni mwa mafanikio.
Baada ya kushindwana na mabosi wake Zidane akaamua kujiuzulu. Nafasi yake haikuzibwa si na Julen Lopetegui wala Santiago Solari . Zidane aliporejea kikosini mwanzoni mwa 2019 alindeleza msimamo wake dhidi ya Bale. Taratibu akamgeuza kuwa mchezaji wa ziada.
Dirisha la usajili la 2019/2020 Bale alikaribia kuondoka Real Madrid, lakini uamuzi ulifutwa na akabakizwa kikosini. Msimu wa 2020/2021 inalekea Bale anaondoka Real Madrid, kwa sababu tayari Zidane ameshawapata wachezaji anaotaka HJazard, Rodrygo na Vinicius Junior, huku akiwa na mchezaji wake mtiifu Lucas Vazquez.
BALE ATAELEKEA WAPI?
Ni wazi sasa Zidane ameshikilia msimamo uleule, kwamba Bale aondoke zake. ndani ya uwanja Zidane amewapa majibu mabosi kwa kuwapa nafasi Rodrygo Goes na Vinicius Junior, huku Lucas Vazquez akiwa tayari kupokea kijiti. Katika nafasi hiyo Eden Hazard anamaliza matumaini ya Bale kucheza Real Madrid, sababu ya wachezaji wa akina waliopo kumsaidia. Hivyo basi Bale si muhimu kikosini.
Manchester United na Tottenham Hotspurs ni klabu zinazotajwa kumfukuzia Bale. Ole Gunna Solksjaer amekuwa akimfukizia kwa udi na uvumba winga wa Borussia Dortmun, Jadon Sancho bila mafanikio. Akili yake imemgeukia Bale ili kuwapa uzoefu makinda wake Mason Greenwood, Anthony Martial na Marcus Rashford. Bale anatarajiwa kuongeza ushindani kikosini katika eneo la winga wa kulia na kushoto, hivyo amekuwa akitafutwa na mabosi wa Old Traford.
Kwa upande wa Tottenham, wanafahamu umuhimu wa Bale. Ni nyota aliyepata mafanikio akiwa klabu hapo kwa miaka 6, na sasa kocha Jose Mourinho anataka kumtumia Bale kama winga wa kushoto ili kutengeneza kombinesheni na Harry Kane na Son Heung-min.
Beki wa kushoto Ben Davies atakuwa sehemu ya mabeki katika mfumo wa 3-4-3 huku beki wa kulia Matt Doherty akipewa uhuru zaidi kushambulia. Changamoto ya Spurs ni gharama za fedha. Usajili wa Bale unagharimu fedha nyingi, hali ambayo itamfanya mmiliki Daniel Levy kufikiria mara mbili zaidi juu ya kumwaga fedha kumrejesha nyota huyo.
Rais wa zamani wa Real Madrid, Ramon Calderon ambaye ni rafiki wa Jose Mourinho amekaririwa akisema Gareth Bale anapendwa na Mourinho na pia dili la usajili wake limekubaliwa.