Kongo Kinshasa, Tunisia wavuka
Timu za Kongo Kinshasa na Tunia zimefanikiwa kuvuka hatua ya makundi katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwenye Kundi B, huku Visiwa vya Cape Verde na Zambia wakiaga.
Waliofuzu walicheza katika dimba la Bata na kwenda sare ya 1-1 wakati Cape Verde na Zambia pia walitoshana nguvu, bali walitoka suluhu. Tunisia walipoteza nafasi mbili za wazi mapema, kabla ya Ahmed Akaichi kufunga dakika ya 31.
Wahbi Khazri baadaye alishindwa kuongeza bao la pili badala yake akapiga mpira juu akiwa kwenye nafasi nzuri, ndipo Jeremy Bokila alipotumia vyema nafasi iliyojitokeza dakika ya 66 na kukwamisha mpira wavuni.
Bao la Bokila lilibadilisha kabisa mwelekeo wa mambo kwa kundi hilo, ambapo sare hiyo ilimaanisha Kongo Kinshasa wanafungana na Cape Verde, kila mmoja akiwa na pointi tatu huku Zambia wakiwa nazo mbili tu, laiti wangeshinda wangefuzu.
Kongo wamevuka kwa sababu ya kuwa na bao moja zaidi ya Cape Verde, nchi ndogo zaidi kijiografia katika mashindano haya. Bokila aliingia dakika ya 60 akitokea benchi na kufunga bao dakika sita tu baadaye, ambapo palikuwa na kila dalili za Kongo kutupwa nje ya mashindano kuwaachia nafasi Cape Verde.
Katika mechi yao, Cape Verde na Zambia walicheza huku mvua ikinyesha, na ilifika mahali ikadhaniwa mchezo ungeahirishwa kutokana na mvua hiyo, kwani ilikuwa kubwa wakati wa mapumziko na mwanzoni mwa kipindi cha pili kabla ya kuacha kunyesha.
Evans Kangwa wa Zambia nusura awavushe dakika za mwisho, lakini mkwaju wake haukufika nyavuni, wakati kwa upande wa pili Antonio Varela alipigwa kichwa kizuri lakini mpira ukapita juu kidogo ya mtambaa wa panya.
Cape Verde wamefunga bao moja tu kwenye mashindano haya wakati Kongo Kinshasa wamefunga mawili. Zambia ndio walikuwa mabingwa 2012 lakini tangu hapo hawajaweza kurudia makali yale.
Hatima ya Kundi C ni leo, ambapo Senegal wanacheza na Algeria huku Afrika Kusini wakikipiga na Ghana. Senegal wanaongoza kundi hilo wakiwa na pointi nne, wakifuatiwa na Ghana wenye tatu sawa na Algeria, lakini Black Stars wapo mbele kwa uwiano wa mabao. Afrika Kusini wana pointi moja. Timu yoyote itakayoshinda ina nafasi ya kuvuka kutegemeana na uwiano wa mabao.