Menu
in

HATIMAYE WENGER ANAIACHA ARSENAL: LAKINI NANI ANAFAA ZAIDI KUMRITHI?

Patrick Vieira, former Barcelona manager Luis Enrique and Juventus boss Massimiliano Allegri.

Baada ya takribani miaka 22 ndani ya klabu ya Arsenal hatimaye Arsene Wenger ametangaza kuiacha klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu. Atakuwa amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake wa sasa. Huenda ataiacha klabu kwa ufahari kwa kuisaidia kushinda taji la Ligi ya Europa ambapo Arsenal wamo kwenye hatua ya nusu fainali.

Wenger ametangaza uamuzi huo uliowashangaza wengi siku ya Ijumaa akisema kuwa anaishukuru klabu hiyo kwa kumpa fursa ya kuitumikia kwa miaka mingi yenye kumbukumbu tele. Aliongeza: “Baada ya kufikiri kwa umakini na kufuatia majadiliano na klabu, nadhani sasa ni muda sahihi wa kuachia ngazi hapo mwishoni mwa msimu”.

Brendan Rodgers won the treble with Celtic last season.

Hakika ni muda sahihi. Wachezaji wa Arsenal bila shaka wana maoni kama hayo ya mwalimu wao. Hapana wasiwasi kuwa washabiki wa timu hiyo nao pia wanamuunga mkono Arsene Wenger kwenye uamuzi wake huu. Kwa miaka mingi wamekuwa wakisubiri jambo hili litokee kwa kuwa klabu imeshindwa kupata mafanikio ya maana kwa muda mrefu sasa chini ya mwalimu huyo.

Wenger anakumbukwa kwa kuifanya Arsenal kuwa timu hatari na yenye mafanikio kwenye miaka ya mwanzoni akiwa na timu hiyo. Aliiwezesha kushinda mataji matatu ya Ligi Kuu ya England ambapo moja kati ya hayo walilitwaa pasipo kupoteza mchezo wowote msimu mzima. Lakini ukame wa mataji ya maana ukakifuatia kipindi hicho mbaka hivi sasa.

Kwa miezi kadhaa imekuwa ikitazamiwa kuwa Mfaransa angeweza kuachia ngazi mwishoni mwa msimu kufuatia nafasi finyu mno ya kuiwezesha Arsenal kumalizia kwenye nafasi nne za juu kwenye Ligi Kuu ya England. Lakini fursa aliyo nayo ya kuipeleka timu kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao kupitia ubingwa wa Ligi ya Europa ilidhaniwa ingeweza kumbakisha Emirates kama angeitumia vyema.

Arsenal wamebainisha kuwa mrithi wa Wenger atateuliwa haraka iwezekanavyo. Ni mwalimu yupi anaweza kupata nafasi hii? Hili ni swali linalobaki bila majibu kwa sasa. Patrick Vieira, Thomas Tuchel, Massimiliano Allegri, Luis Enrique, na Mikel Arteta ni kati ya majina yanayopewa nafasi ya kuchukua mikoba ya Arsene Wenger.

Alhamisi Arsene Wenger alibainisha kuwa Patrick Vieira ni mtu anayefaa kuja kumrithi ndani ya Arsenal siku moja. Nahodha huyu wa zamani wa Arsenal aliitumikia klabu hiyo kwa miaka tisa chini ya Arsene Wenger akicheza jumla ya michezo 279. Kwa sasa anainoa New York FC ya Marekani. Inaonekana Wenger anapendelea mchezaji wake wa zamani achukue nafasi yake lakini huenda bodi itakuja na uamuzi tofauti.

Mikel Arteta is currently working as an assistant manager to Pep Guardiola at Manchester City.

Thomas Tuchel ambaye hana timu kwa sasa baada kuinoa Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa misimu miwili kuanzia 2015 mbaka 2017 huenda atapata nafasi ya kujumuika kwa mara nyingine na mchezaji wake wa zamani Pierre-Emerick Aubameyang. Lakini Mjerumani huyo anatajwa pia kuwa miongoni mwa wanaoweza kujiunga na PSG ya Ufaransa jambo linalofanya uwezekano wa kutua Emirates kuwa finyu.

Kocha Bora wa Dunia wa mwaka 2015 Luis Enrique naye ni miongoni mwa wanaotabiriwa kuja kurithi kiti cha Arsene Wenger. Mhispania huyo alipata mafanikio makubwa akishinda mataji 9 kwa misimu mitatu aliyodumu na FC Barcelona. Kwa sasa yupo mapumzikoni na aliwahi kusema wiki chache zilizopita kuwa anaweza kurejea kwenye soka ikiwa timu itamuhitaji, lakini timu hiyo ni lazima imvutie kwanza.

Massimiliano Allegri wa Juventus naye aliwahi kubainisha siku chache zilizopita kuwa angependa kupata changamoto mpya nje ya Ligi Kuu ya Italia ambamo amefanya kazi kwa misimu minne sasa akishinda taji la Serie kila msimu. Pia aliifikisha Juventus kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa mara mbili.

Nani kati ya hao anafaa zaidi kumrithi Arsene Wenger? Luis Enrique pengine ndiye anayeweza kuwa chaguo sahihi zaidi. Ni kocha mwenye mafanikio zaidi kuliko wote kwenye orodha hii. Rekodi zake na hali ya kujiamini vinaweza kumuwezesha kurejesha heshima na hadhi ya Washika Bunduki hawa wa London. Vipaji vilivyopo Arsenal vinamtosha Luis Enrique kuifikia dhamira hiyo. Lakini bodi ya Arsenal ndiyo yenye uamuzi wa mwisho. Tusubiri.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version