*Ahaidi kutomng’ata mtu tena maishani!
Hatimaye mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez ameomba radhi kwa kitendo chake cha kumng’ata Giorgio Chiellini wa Italia.
Mchezaji huyo wa Liverpool aliyefungiwa soka kwa miezi minne na mechi tisa za kimataifa amemtaka radhi Chiellini, akisema ni dhahiri aliumia.
“Ukweli ni kwamba jamaa yangu huyo Giorgio Chiellini aliumia mwilini kutokana na mng’ato ule tulipogongana naye. Najutia sana kwa hilo lililotokea.
“Naomba radhi kwa Giorgio Chiellini na ulimwengu wote wa wanasoka. Naahidi hadharani kwamba hapatatokea tena tukio jingine kama hili,” anasema Suarez.
Awali, Suarez (27) alidai kwamba alipoteza mizania, akayumba na wala hakumng’ata Chiellini. Hii ni mara ya tatu Suarez anatiwa hatiani kwa kung’ata wanasoka wa timu pinzani; mara ya kwanza ilikuwa Aprili mwaka jana akiwa Liverpool alimng’ata Branislav Ivanovic wa Chelsea na 2010 akiwa Ajax alimng’ata Otman Bakkal wa PSV.
Chiellini amemjibu Suarez kupitia mtandao wa Twitter akisema; “yameisha na nimeshasahau hayo. Natumaini Fifa watakupunguzia adhabu.”
Suarez atakosa mechi tisa za Ligi Kuu ya England na atarudi uwanjani Oktoba 26. Kutokana na ung’ataji wake kwa ujumla, atakuwa amekosa mechi 39.
Hata hivyo, taarifa yake ya kuomba radhi kwa tukio hili inafanana na aliyotoa mwaka jana alipomng’ata Ivanovic, ambapo licha ya kuomba radhi, alisema vitendo vyake havikubaliki uwanjani.