Na:Ramadhani Juma
Waswahili wanasema siku zote panapofuka moshi pana moto, hii ndio kauli ninayoweza kuitumia sasa kueleza kinachoendelea ndani ya klabu ya Simba kwa sasa, moshi umefuka kwa muda mrefu na sasa umeanza kuonekana moto, baada ya kocha msaidizi wa Simba kuachwa Dar es Salaam Simba ikisafiri kwenda kucheza na Ndanda FC ya Mtwara, Mbao FC ya Mwanza na Mwadui FC ya Shinyanga.
Kinachoendela kwa sasa kati ya kocha mkuu wa Simba SC raia wa Ubelgiji Patrick Aussems na msaidizi wake Masoud Djuma, hakina tofauti sana na moshi uliofuka kwa muda mrefu na sasa kuonekana moto umekolea inabidi kuuzima, pamoja na kuwa viongozi wa Simba wamejitahidi kadri ya uwezo wao kuficha mahusiano ya Patrick na Masoud kuwa yapo sawa lakini kwa sasa hilo halifichiki tena ni wazi Patrick na Masoud hawaivi chungu kimoja.
Vyanzo vya ndani ya uongozi wa klabu ya Simba SC vinadaiwa kueleza kuwa kocha mkuu Patrick Aussems haelewani na msaidizi wake Masoud Djuma, licha ya uongozi kujaribu kuwasuluhisha mara kadhaa ni wazi Masoud Djuma ana matatizo na inabidi aondolewa kuinusuru timu na kuleta umoja.
Unaweza kujiuliza kwa nini aondolewe Masoud Djuma na sio Patrick kwani wote ni waajiriwa wa Simba na hakuna mwenye mamlaka ya kusema mwenzake afukuzwe abaki yeye, kiukweli Masoud anabidi aondoke kwa nadharia nyepesi sana ambayo inatumika sana Tanzania.
Kuna usemi unasema katika kundi la watu 10 wakikaa chini watu saba kati yao hao wakakwambia una matatizo na watatu waliosalia wakisema upo sahihi basi jua una matatizo kweli lakini saba kati ya 10 wakisema upo sawa na watatu kati ya 10 wakisema una matatizo jua wao (watatu) ndio wana matatizo.
Kwa nini kila kocha mkuu aliyeondoka Simba SC amewahi kumtuhumu Masoud Djuma kuwa ana matatizo, kabla ya Patrick alikuwepo Joseph Omog raia wa Cameroon ambeye alifutwa kazi na kueleza kuwa Masoud ana matatizo, Pierre Lichantre raia wa Ufaransa nae aliondoka Simba SC kwa sababu ambazo hazikuwekwa wazi mara moja lakini inatajwa kuwa ni maslahi nae aliwahi kumtuhumu Masoud Djuma kuwa ana matatizo.
Naamini Omog, Lechantre na Aussems hawajawahi kukutana wala kuongea hata kwa njia ya simu lakini kwa nini wote kwa nyakati tofauti wamlaumu Masoud Djuma lazima kuna jambo hivyo lazima Masoud Djuma aondolewe kwenye timu ili kunusuru mgawanyo ndani ya timu kwani kuendelea kuwepo ni rahisi kuwagawa wachezaji.
Kwa nini nasema hata tukimuondoa Aussems, Simba SC kocha mkuu mpya wa Simba atakayefuatia lazima atamlaumu tu Masoud Djuma, naanza kuamini kauli yake ya mwisho aliyowahi kunukuliwa Masoud Djuma akiwa Rwanda kuwa kwa sasa basi hawezi kuwa kocha msaidizi tena, hiyo kauli aliitoa akiwa Rwanda hata kabla ya kujiunga na Simba lakini alipotua Tanzania akasema alimaanisha kuwa hawezi kuwa kocha msaidizi ndani ya Rwanda sio nje ya nchi, naamini Masoud Djuma kwa sasa anamiini ameiva kuwa kocha mkuu, mtu wa namna hii ni ngumu kumuweka chini ya mtu akafanya vizuri.
Masoud Djuma ni kocha ambaye anaamini anastahili kuwa kocha mkuu sasa kuwekwa msaidizi sidhani kama anapenda, kauli yake tu kama uliwahi kusikia ni wazi huwezi kumchukua kwenye timu yako ukitegemea awe kocha msaidizi pasipo kugombana na mkuu wake, Masoud inawezekana anaamini ana uwezo mkubwa kuliko maboss wake waliopita Simba na aliyepo, sasa ni ngumu kumbadili Masoud kwa nadharia hiyo ni wazi Simba inahitaji kuachana na Masoud ili kuiweka timu katika umoja, hiki kilio wamelia makocha wengi na kuna usemi unasema wengi wape kwa hili uongozi wa Simba uangalie upande wa wengi na kuwapa wakitakacho kwa kumuondoa Masoud Djuma.