NYOTA pekee wa Tanzania anayecheza mpira wa kikapu katika ligi ngumu, yenye mvuto na utajiri mkubwa kwa ngazi za klabu duniani, Ligi ya Kikapu ya Marekani (NBA), Hasheem Thabeet amenyakuliwa na klabu ya Portland Trail Blazers inayoshiriki katika ligi hiyo.
Sasa akiwa na umri wa miaka 25, Thabeet ambaye hadi anatimiza umri wa miaka 15 alikuwa hajawahi kucheza mpira wa kikapu, ametua Blazers akitokea Houston Rockets akibadilishwa na mchezaji mwingine Marcus Camby.
Uhamisho huo ulikamilika jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho iliyowekwa na NBA kwa ajili ya klabu zinazocheza ligi hiyo kufanya utaratibu huo wa kubadilishana wachezaji.
Mlinzi Jonny Flynn, pia amejiunga na klabu ya Portland Trail Blazers kama sehemu ya utaratibu huo, Thabeet ambaye sasa amechukuliwa na Blazers kabla alichukuliwa na Houston Februari mwaka jana, akitokea Memphis na alifanikiwa kuichezea Rockets mechi tano pekee katika msimu huu wa ligi.
“Tunatazamia kuwa yale yatakayofanywa na Jonny pamoja na Thabeet yanaweza kuleta mafanikio katika timu yetu na pia tunamshukuru Marcus kwa mchango alioutoa kwa kipindi cha misimu mitatu aliyokuwa nasi na tunamtakia kila la heri huko alikoenda,” alisema Kaimu Meneja Mkuu wa Blazers, Chad Buchanan.
Katika michezo 120 ya misimu mitatu akiwa na klabu za Memphis na Houston, Thabeet anayetajwa mmoja wa wachezaji tajiri ukanda wa Afrika Mashariki, amekuwa na wastani wa kufunga pointi 2.2.