ana kazi ngumu ya kuwanyanyua QPR, ambayo mashabiki wake walishakata tamaa na walifikia kumzomea kocha Hughes, wachezaji na hata watumishi siku za mechi.
Harry Redknapp atawaokoa QPR?
Ugumu wa Ligi Kuu ya England (EPL) umedhihirika kwa makocha wawili kufutwa kazi, na sasa Harry Redknapp amekuwa kocha wa Queen Park Rangers (QPR).
Subira ya mmiliki wa klabu hiyo, milionea wa Malaysia, Tony Fernandes kwa kocha wa zamani, Mark Hughes ilifikia kikomo baada ya kufungwa mabao 3-0 na timu dhaifu ya Southampton.
Redknapp (65) alikuwa kocha wa Tottenham Hotspurs msimu uliopita na alifutwa kazi baada ya timu hiyo kukosa nafasi Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo, Spurs walishika nafasi ya nne kwenye ligi na kufuzu, bali walipokwa ushiriki ligi ya mabingwa kutokana na Chelsea kutwaa kombe, hivyo kuwapisha wakalitetee msimu huu.
Hughes alifukuzwa kazi siku sita baada ya kupoteza mechi hiyo muhimu, iliyotarajiwa walau kuwapatia ushindi wa kwanza katika ligi, na kuwafanya QPR wamalize mechi 22 wakiwa na pointi nne tu za kutoka sare mechi kama nne.
Redknapp ni kocha mzuri, na alikuwa akipigiwa chapuo na Waingereza kuteuliwa kufundisha timu ya taifa, ikadhaniwa alishaipata kazi, lakini kwa mshangao wa wengi akatangazwa Roy Hodgson aliyekuwa West Bromwich Albion.
Hughes ni kocha wa pili kutimuliwa, baada ya Roberto Di Matteo wa Chelsea kunyang’anywa kibarua chake na nafasi hiyo kuchukuliwa na Rafa Benitez atakayekaa hadi mwisho wa msimu huu, miezi saba ijayo.
Redknapp pia alikuwa katika mipango ya kuinoa timu ya taifa ya Ukraine, ambapo mawakala wake walitoka huko wiki hii, baada ya chama cha soka cha huko kuonesha nia ya kumtaka.
Mwingereza huyo aliichukua Spurs mwaka 2008 ikiwa mkiani kama QPR sasa, akaijenga na kufanikiwa kuiweka nafasi za juu, kabla ya kuiwezesha kuingia mashindano ya Ulaya na kupata jina kubwa inalotambia sasa.
Nafasi yake ilichukuliwa na Mreno, Andre Villas-Boas aliyeanza msimu kwa matokeo mchanganyiko ya kufungwa, sare na kushinda mechi chache. Kabla ya hapo alifukuzwa kazi Chelsea mwaka jana, baada ya kufanya vibaya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Redknapp
Bodi ya QPR ilifanya vikao vingi kabla ya kumfuta kazi Hughes, kwani mmiliki alipata kusema lazima apewe muda zaidi, lakini naye alimkatia tamaa. Hughes (49) ni mchezaji wa zamani wa Manchester United, aliyecheza chini ya kocha Alex Ferguson.
Upo uwezekano wa Redknapp kufanya vyema hata bila kuongeza wachezaji Januari, kwa sababu kikosi kina wachezaji wengi wazuri, baadhi wakiwa wamesajiliwa kwa msimu huu na Hughes, wakiwamo waliochukuliwa kutoka ng’ambo.
Wachambuzi wa masuala ya soka wamekuwa wakisema tatizo la timu hiyo ni kocha, lakini mmiliki hakuelekea kukubaliana nao, na sasa wamebaki kuwa timu pekee isiyoshinda mechi msimu huu, kwani wenzao Reading walipata ushindi hivi karibuni.
Redknapp ameanza kukiangalia kikosi chake akiwa kwenye jukwaa katika uwanja wa Old Trafford dhidi ya Manchester United.
Anatarajiwa kuwa kwenye benchi la ufundi rasmi mwanzoni mwa wiki pale QPR watakapopepetana na Sunderland.
Tangu kufutwa kwake kazi alionekana dhahiri kuhaha kupata nafasi nyingine kwenye ligi kuu au popote, na kwa maneno yake alisema hii ndiyo taaluma aliyo nayo na hawezi kwenda kupiga deki.
Katika miaka yake 30 ya ukocha, Redkanpp ameweka rekodi ya kushinda mechi 520, sare 318 na kupoteza mecho 437, ambapo kwa asilimia za kihesabu, ushindi wake ni 40.82.