Menu
in , , ,

Harry Kane Madrid?

Tanzania Sports

Harry Kane Madrid?

Maneno yanazidi kuwa mengi juu ya uwezekano wa Nahodha wa Timu ya Taifa ya England anayekipiga Tottenham Hotspur, Harry Kane kujiunga na miamba wa Hispania, Real Madrid.

Mshambuliaji huyo mahiri amekuwa na uvumilivu wa kubaki Spurs – London Kaskazini tangu ajiunge hapo 2004, japokuwa kwa nyakati fulani alipata kutolewa kwa mkopo kwenye klabu tofauti, lakini hajaweza kunyanyua kombe la ubingwa.

Real Madrid wanafuatilia kwa karibu mambo ya Mwingereza huyu, na huenda wakabahatisha kutupa ndoano kiangazi hiki, hasa baada ya mweneywe Kane kunukuliwa akisema kwamba kuondoka klabuni hapo ni moja ya mambo yanayowezekana.

Rais Florentino Perez wa Real Madrid anajulikana kwa tambo zake na kupenda kununua wachezaji kwa bei kubwa, wenyewe wakisema ‘kuvunja benki’ na baada ya kuondoka kwa Cristiano Ronaldo huko Dimba la Santiago Bernabeu, kuna kila sababu ya kusajili mchezaji wa kiwango cha juu kabisa kimataifa, kwani pengo linaonekana wazi.

Mchezaji wao wanayemtegemea pale mbele, Karim Benzema sasa amefikisha umri wa miaka 32 na wakati akiwa amefunga mabao 14 hadi msimu uliposimamishwa kwa muda usiojulikana kutokana na virusi vya corona, klabu wanatafuta mrithi wake.

Kane akiwa na umri wa miaka 26 na kwenye kiwango cha hali ya juu cha soka kabla ya kuumia, ni mmoja wa washambuliaji bora duniani, ambapo Mundo Deportivo wanasema kwamba Perez na Kocha Zinedine Zidane wameweka matumaini yao kwa Kane kama chaguo muhimu kwao kuiogeza mbele klabu hiyo.

Mpachika mabao huyu hatari alisema mubashara kwenye mtandao wa Instagram: “Nikihisi hatusongi mbele wala kwenda kwenye uelekeo sahihi kama timu, mie si mtu wa kubaki kwa ajili hiyo tu. Mie ni mchezaji mwenye kutaka mambo makubwa.”

Ukame wa vikombe kwa Spurs utaendelea bado hata msimu huu ukianza, kwa sababu tayari wametupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL) na RB Leipzig waliowatandika nyumbani na ugenini, wakatupwa nje ya Kombe la FA na vibonde Norwich na pia nje ya Kombe la Ligi na Colchester United.

Ama kwenye Ligi Kuu ya England (EPL) Liverpool wamewaacha mbali mno – kwa alama 41 hivyo hakuna matarajio yoyote. Nusura wachukue kikombe msimu uliopita, pale walipofika fainali ya UCL lakini Liverpool wakawatandika kwenye mechi iliyochezwa jijini Madrid, Hispania.

Ni tangu hapo klabu wakaanza kuporomoka na msimu ulipoanza wakawa na hali mbaya kiasi cha kumfukuza kocha wao, Mauricio Pochettino anayeonekana kwamba alikuwa moja ya kitu kinachombakisha hapo kwa jinsi alivyokuwa ameujenga uhusiano mzuri naye Pamoja na wachezaji wengine.

Katika mazingira hayo, huku klabu kubwa yenye uhakika wa makombe kama Real wakiwa wanamtaka Bernabeu, upo uwezekano mkubwa kwake kuhamasika kwenda Madrid. Hata hivyo, Madrid lazima wajue kwamba vita ya kuchukua wachezaji mahiri Spurs si lelemama, kwani Mwenyekiti Daniel Levy ni mjanga, akijua kuwanunua kwa bei ndogo na kuwauza kwa bei ya kutupa hasa.

Kwa kuwa wapo tayari kuvunja benki, huenda ukawa wakati wao kumpata mchezaji huyu ambaye wachambuzi wameshasema kwamba ikiwa anataka kwenda kwenye klabu na kuzoa vikombe, wakati wenyewe ni huu. Madrid walishawanunua kwa bei kubwa wachezaji hapa – katika Luka Modric na Gareth Bale.

Kane alikuwa na majeraha ya paja na amekosa mechi nane zilizopita za Spurs, ambapo kama si virusi vya corona, angekuwa amekosa nyingi zaidi. Amefunga mabao 11 katika mechi 20 za juu alizocheza msimu huu

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version