Ni mshambuliaji mwenye uwezo mzuri nje ya klabu kubwa za juu. Katika maisha ya soka Harry Kane hajawahi kutwaa taji lolote…
RONALDO DE LIMA hadi anastaafu soka la kimataifa alikuwa amenyakua mataji mawili ya Kombe la Dunia (1994-2002). Hadi alipostaafu kucheza ngazi ya klabu hakuwahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Si Barcelona wala Real Madrid au Inter Milan. Lakini kipaji cha Ronaldo De Lima kinafahamika bayana.
Labda ni kwa vile ni Mbrazil. Hebu tuangalie Allan Shearer raia wa Uingereza, anasifika kwa umahiri mkubwa wa soka lakini ni nyota ambaye hakutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Huyu alikuwa kati ya wafungaji vinara wa EPL. Ni mchezaji aliyewika sana Newcastle United na mshambuliaji kinara wa timu ya taifa ya Uingereza.
Kama dhulumu aliyofanyiwa Alan Shearer katika maisha yake ya soka ni kutotwaa mataji makubwa, lakini pia hakuwa na tuzo za kimataifa kama Ronaldo De Lima. Kiujumla hawa ni washambuliaji ambao wametikisa Ligi tofauti. Ronaldo De Lima alicheza soka Brazil kisha akaenda zake Uholanzi,
Hispania (Barcelona) na baadaye Italia kabla ya kurudi tena Hispania (Real Madrid). Yupo mshambuliaji mwingine Andy Cole aliyekipiga katika kikosi kilichofanya maajabu mwaka 1999 kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich ya akina Sammy Kuffour.
Ni mshambuliaji mwenye sifa nyingi EPL kama ilivyo kwa Wayne Rooney aliyekipiga Man United. Ukibaki kwenye uzawa wa Uingereza hata Danny Welbeck alikuwa mshambuliaji mzuri kwa wakati wake. Hata hivyo nje ya miamba ya Man United, Arsenal, Chelsea, Liverpool na Man City yupo kijana mwingine kutokana jijini London, Harry Kane. Kijana huyu Harry Kane anakipiga katika klabu ya Tottenham Hotspurs.
Timu hiyo iko chini ya Uenyekiti wa Daniel Levy lakini mafanikio yao kisoko waliyafikia kwa kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Spurs hiyo ilikuwa chini ya Mauricio Pochettino na tangu hapo haijawahi kufika hata robo ya mafanikio aliyoleta kocha huyo.
Pochettino licha ya kutengeneza Spurs yenye ubora aliishia kutupiwa virago. Kati ya wachezaji waliokuwa wananolewa na Pochettino ni Harry Kane. Raia huyo wa Uingereza amekuwa nahodha wa timu yao ya Taifa.
Ni mshambuliaji mwenye uwezo mzuri nje ya klabu kubwa za juu. Katika maisha ya soka Harry Kane hajawahi kutwaa taji lolote. EPL, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Europa League na huko kwenye Euro alishuhudia ndoto zao zikiyeyuka katika hatua ya matuta na kuipa ubingwa Italia. Akiwa katika kikosi cha England,
Harry Kane anaonekana kuwa mchezaji anayemudu mfumo wa unaotumiwa nan a kocha Gareth Southgate. Ni kocha huyo alimfanya Harry Kane kuwa nahodha wa Three Lion. Lakini hadi leo Harry Kane hana taji lolote. Timu mbalimbali zimekuwa zikibisha hodi kutaka kumsajili lakini zinaambulia patupu.
Kane amefundishwa na makocha wa daraja la juu, Jose Mourinho, Antonio Conte na Mauricio Pochettino bila kunyanyua kwapa zake kwa maana ya kutwaa taji. Mshambuliaji huyo amehusishwa na timu za Man United, Man City, Liverpool, na Chelsea kwa nyakati tofauti lakini hakuna aliyofanikiwa.
Kwa kipindi hiki cha usajili Harry Kane amehusishwa tena na timu nilizotaja hapo juu, lakini sasa imeongezeka Real Madrid. Mabingwa wanaomaliza muda wao Real Madrid wameondokewa na Karim Benzema, hivyo wapo sokoni kusaka saini ya nyota mpya kuziba pengo hilo. Harry Kane ni miongoni mwa nyota wanaotajwa tajwa kuhamia Real Madrid, lakini kumekuwa na wasiwasi kwa pande mbili.
Upande wa kwanza timu kadhaa zinazomtaja Harry Kane zimekuwa zikikwamishwa na msimamo wa Mwenyekiti wake, Daniel Levy. Pili kikwazo kingine ni kutoka kwa Harry Kane mwenyewe ambaye hajaweza kuweka wazi ikiwa anatama kuhama timu hiyo kwani haijafanikisha ndoto zake za kutwaa mataji. Majaribio ya msimu kadhaa iliyopita yalikwamishwa na Kane na Levy kwa pande zao. Lakini sasa jua linamchwea bado zipo timu zina imani na nyota huyo.
Je ataendelea kubaki Spurs mahali ambako kocha Antonio Conte aliona kwamba hakuna kitu chochote kinachopiganiwa na wachezaji wa timu hiyo na hawaonekani kuwa ari ya aina yoyote. Harry Kane jua linamchwea kwa maana anaelekea umri wa miaka zaidi ya miaka 30 huku akiwa hana uhakika wa kuchukua ubingwa wowote akiwa na jezi za Tottenham Hotspurs.
Kwa namna timu hiyo ilivyovurugika misimu kadhaa hadi sasa, linakuwa jambo la ajabu kuona kipaji kizuri kama hicho kikimaliza soka lake bila taji lolote. Ronaldo De Lima alitwaa Kombe la Dunia, kisha alitwaa mataji kadhaa ya Ligi pamoja na tuzo binafsi. Wenzake Wayne Rooney, Andy Cole na Allan Shearer walikuwa na tuzo nyingi binafsi na mataji.
Lakini Harry Kane anakuwa nahodha wa timu ambayo haimpi mafanikio yoyote zaidi ya mshahara. Msimu huu unategemewa kuwa nyota huyu anaweza kufanya uamuzi, lakini kwa maisha aliyozowea Spurs yamfanya awe mchezaji duni ambaye hana shauku ya mataji ngazi ya klabu. Ni wapi atakwenda? Huo ni uamuzi wake na huenda ukawa bora zaidi akitafuta timu yenye uhakika wa kuwania mataji kuliko ‘likizo’ iliyopo Spurs huku jua likimchwea.