Wakati nakuwa kwenye miaka ya 1999 mpaka miaka ya 2000 masikio yangu
yalikuwa yanabembelezwa na nyimbo nzuri kutoka Morogoro katika wilaya
moja inayoitwa Turiani.
Nyimbo ambayo ilikuwa imepangaliwa vizuri kuanzia utunzi wa mashairi,
mpangalio mzuri wa sauti murua, vyombo vya muziki vilikuwa
vimepangiliwa vizuri kwenye hiyo nyimbo. Kila chombo kilisikika vizuri
na kilikuwa kimepigwa kwa ustadi mkubwa kitu kilichosababisha nyimbo
ya manoir Mtibwa Sugar kuwa maarufu.
Umaarufu pekee haukutosha kuupa heshima wimbo huo,waandaji wa tuzo
waliwatunuku Mtibwa kama mabingwa wa nyimbo nzuri kwa kipindi kile.
Haikuwa rahisi hata kidogo kwa msanii mdogo kama Mtibwa Sugar
kupenyeza katikati ya wasanii wakongwe wa Tanzania yani Simba na Yanga
( Sikinde na Msondo ngoma).
Kitu kikubwa nilichojifunza kipindi hicho ni kwamba kuwa kwenye siasa
ni kama kuwa kocha wa mpira wa mguu, unatakiwa ujifunze vitu vingi
sana ili kuwa mwanasiasa bora anayeendana na wakati. Ndicho
alichokifanya Sunday Kayuni, alihakikisha anajifunza vitu vingi ili
kuwa mpinzani bora wa Simba na Yanga.
Mpira ni kitu chepesi sana, lakini ni ngumu kucheza kiwepesi. Kayuni
hakuchukulia mpira kama kitu chepesi, alikuwa anahakikisha wachezaji
wake wacheze katika hali ya kutoweka wepesi ndani yao, ilichukua miaka
mingi tena kutokea mwanamziki wa kuja kuwatikisa hawa kina Msondo
ngoma baada ya Mtibwa kupotea.
Wengi walicheza kiwepesi kwa sababu mpira waliuchukulia kiwepesi,
hawakuweza kufanikiwa kukaa katikati ya Sikinde na Msondo ngoma. Azam
alikuja baada ya hapo tukapata matumaini kuwa ndiye mwanamziki
tuliyekuwa tunamsubiria baada ya Mtibwa.
Azam pekee hatoshi kuwa mpinzani bora wa Sikinde na Msondo ngoma.
Ushindani mkubwa huleta maendelo makubwa siku zote, tumekuwa na
maendeleo hafifu kwenye hii tasnia kwa sababu hakuna ushindani mkubwa.
Kila anayekuja kuleta upinzani kwa hawa watu hajidhatiti ipasavyo, na
moja ya njia ya kujidhatiti ipasavyo kwenye hii tasnia ni kuwa na
kocha bora.
Kocha bora siku zote hufundisha, hupandisha Morali ya timu na kuweka
hamasa ndani ya mioyo ya wachezaji ili waweze kupigana kwa ajili ya
kupata vitu vinavyoonekana haviwezekani kwenye macho ya nyama.
Ndicho kitu akichonacho kocha Hans, kocha mpya wa Singida United.
Ukiniuliza kama ameenda sehemu sahihi nitakutazama kisha nakurudisha
jicho langu kwa Hans, kuna kitu kimoja tu nitamuomba.
Ni muda mrefu sana masiko yetu yamekuwa yakisikia nyimbo za Msondo
ngoma na Sikinde. Hakuna nyimbo mpya iliyokuja kuleta upinzani mzuri
kwa hawa mababu.
Ndiyo maana hawafanyi vizuri kwenye mechi za kimataifa. Ni wewe pekee
uliyewafanya Yanga wafike robo fainali ya michuano ya kombe là
shirikisho barani Afrika, hii pekee inatosha kuonesha kuwa unauwezo
mkubwa wa kufanya kitu kisichowezekana mbele ya macho ya nyama ya
watu.
Uwezo huu nakuomba uupeleke Singida United. Tunatamani kupata mpinzani
wa nguvu ili ligi yetu ipate upinzani na ushindani mkubwa.
Usije ukakubali kutumika kwenye siasa za mpira kwa kuwafanya Singida
wawe tawi jipya la Yanga eti kwa sababu uliwahi kufundisha timu ya
Yanga ,au pia Mwigulu ni shabiki wa Yanga na ni mmoja wa watu
wanaoisaidia Singida United.
Nenda katengeneze ufalme wako kwa Wanyaturu, ufalme hutengenezwa
popote,Ufalme haukuletwa kwenye mitaa ya Kariakoo pekee.
Heshima ambayo haikupewa thamani Kariakoo, nenda kaithihirishie
thamani yake kwa Wanyaturu.
Onesha ni jinsi gani ulivyona thamani kubwa, na ikizingatia ya kwamba
wewe siyo mgeni na soka letu.
Unalijua vizuri kuanzia wachezaji mpaka viongozi wa mpira.
Hakuna kipya ambacho kitakuja katika macho yako, na kitu kizuri kwako
ni kwamba ulikataliwa Kariakoo sehemu yenye kelele nyingi, muda huu
upo Singida, sehemu yenye ukimya mkubwa, ni kazi yako tu imebaki ya
kutengeneza muziki mzuri utakaoweza kushusha nyimbo za Sikinde na
Msondo ngoma