Bingwa mpya wa Mashindano ya Dunia ya Langalanga yaliyofanyika Abu Dhabi, Lewis Hamilton amesema kutwaa taji hilo kwake ni furaha ya aina yake na mwanzo wa kitu cha kipekee kwake na timu ya Mercedes.
Hamilton (29) aliyejiunga na Mercedes akitoka McLaren mwaka jana akiahidiwa kupewa gari lenye ushindani anafurahia ushindi huo wa dunia ambao ni mara ya pili kuupata. Mashindano hayo yalihitimishwa Jumapili, yakienda kwa jina la Abu Dhabi Grand Prix.
“Najihisi kana kwamba ndio naanza. Timu hii imefanya mambo makubwa. Nilitamani sana kuwa sehemu ya kitu kipya kilichokuwa kikianza na kukua,” alisema baada ya kujikusanyia pointi 67 akiwa katika vita kali na mwanatimu mwenzake, Nico Rosberg.
Hamilton amesema kwamba yeye na Nico wataendelea kuisongesha mbele timu yao, akiongeza pia kwamba wana watu wazuri waliowekwa kwenye nafasi mwafaka na kwamba mwaka huu umekuwa wa aina yake.
Mwanatimu mwenzake, Rosberg alisaini mkataba mpya mwaka jana utakaomalizika Mei mwaka 2016 wakati ule wa Hamilton umamalizika mwishoni mwa mwaka kesho. Yeye na uongozi wa Mercedes walikwisha anza mazungumzo ya kuhuisha mkataba ili ajikite kwenye mashindano hayo, na wakati wowote yataanza.
Bosi wa Mercedes katika Langalanga, Toto Wolff amesema watakaa chini kuona cha kufanya, lakini matarajio ni kuendelea kufanya kazi pamoja kwa muda mrefu ujao. Hamilton amesema hana haraka ya majadiliano kwa sababu bado kuna mwaka mmoja mbele, ana furaha kuwa Mercedes na kwamba hatarajii kukabiliana na changamoto tofauti.
Mwenyekiti Mtendaji wa Mercedes, Niki Lauda aliyemshawishi Hamilton ajiunge nao alisema kwamba mazungumzo yataanza ndani ya wiki mbili lakini haoni tatizo lolote mbele yao.