Aliyekuwa kocha mkuu wa timu ya soka ya wanawake Tanzania (Twiga Stars), Boniface Mkwasa, amesema kuwa suala la usagaji linalozungumziwa hivi sasa baada ya timu hiyo kutolewa katika mashindano ya Afrika linawadhalilisha na athari zake zitakuwa kubwa kwenye maendeleo ya soka la wanawake hapa nchini.
Mkwasa alisema kuwa baada ya timu hiyo kuondolewa kwenye mashindano ya kimataifa aliamua kubeba lawama kwa kujiuzulu na isitafute sababu nyingine ya kufanya vibaya kwa timu hiyo.
Alisema jambo hilo halipo kwenye timu hiyo na kwa muda wote hakuwahi kusikia kuna wachezaji wanaojihusisha na vitendo vya usagaji kama inavyodaiwa na baadhi ya wadau wa soka hapa nchini.
“Usagaji Twiga haupo, yoyote anayejua alipaswa kutuambia ili tuweze kulifanyia kazi, hilo suala silijui, na kama kambini Ruvu wachezaji wanalala sita, litafanyikaje katika hali kama hiyo,” Mkwasa aliongeza.
Alisema kuwa linapoendelea kuzungumzwa litawafanya wazazi washindwe kuruhusu mabinti zao ambao wana vipaji vya kucheza soka na hivyo soka la wanawake litashuka badala ya kupanda kama tunavyotarajia.
Meneja wa Twiga Stars, Furaha Francis, alisema kuwa wachezaji na benchi la ufundi liliumia kutokana na timu hiyo kuondolewa kwenye michuano ya kimataifa lakini matokeo hayo kuhusishwa na ‘usagaji’ imewaumiza zaidi.
“Mmetudhalilisha, kwanini hiyo ijitokeze wakati tumefungwa, kitu kama hicho hakipo, sijawahi kukiona,” alisema Furaha.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Soka la Wanawake Tanzania (TWFA), Lina Mhando, alisema kwamba huu ni wakati wa kuijenga timu na njia za kuikosoa zipo nyingi.
Lina alisema timu hiyo ilipofika ina mabadiliko tofauti na ilivyokuwa mwaka 2006 na bado wanawaomba wadau waendelee kuisaidia ili ipate maendeleo.
Aliongeza kwa kuwataka wazazi na viongozi wa klabu wanazotoka kusaidia kubadili tabia za wachezaji hao kwa sababu huko ndiko wanakokaa na nyota hao kwa muda mrefu