Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema
hakuna hila yoyote katika marekebisho ya Katiba kwa vile yametokana na
maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
* *
Akizungumza na Wahariri wa Michezo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo
(Julai 9 mwaka huu), Rais Tenga amewahakikishia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa
Dharura kuwa dhamira ya marekebisho hayo ni nzuri, kwani lengo ni kila mtu
apate haki yake.
* *
Amesema Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na
ajenda moja tu ya kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya
Maadili katika Katiba ya TFF kama ilivyoelekezwa na FIFA ili baadaye uanze
mchakato wa uchaguzi.
* *
“Katika kuunda Kamati ya Maadili tumeangalia ile ile ya FIFA, tusitengeneze
kitu kipya, yaondolewe yale yanayotakiwa kuondolewa, na yaongezwe yale
yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu tumeangalia mazingira kwa Tanzania ni
tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu zingine,” amesema.
Rais Tenga amewataka wajumbe wafike kwenye Mkutano wakiwa na mtazamo wa
kujenga, kwani kuna maagizo ya FIFA ambayo wanatakiwa kuyatekeleza ili
wasonge mbele.
“Tutawaeleza kwanini hili limewekwa na lile limeondolewa. Mpira unataka
unit (kitu kimoja), ni mchezo wa kila mtu. Baada ya hapa tunaanzisha
mchakato wa uchaguzi. Watu wanaingia wakiwa wamoja, wanatoa hoja
wanasikilizwa. Wanahukumiwa kwa hoja,” amesema na kuongeza utatolewa muda
wa kutosha wajumbe ili wayaone na kuelewa marekebisho hayo.
Rais Tenga pia alizungumzia kipindi hiki cha usajili na kutaka klabu
ziwaachie wataalamu wa mpira wa miguu kwani ndiyo wanaojua upungufu wa
timu, hivyo wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
Amesema tatizo kubwa la klabu za Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa
kuhimili dakika 90, hivyo watu wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi
ambayo timu zao zinafanya badala ya kubakia kutaja tu majina ya wachezaji
wanaotaka kusajiliwa.
* *
*KIINGILIO MECHI YA STARS, UGANDA 5,000/-*
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji
wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The
Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000
viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045
kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo
viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060
ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A
yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali
hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika itachezeshwa na mwamuzi Thierry
Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Kampala kati
ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza
kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule ya
Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa
Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na
BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia
yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.
Tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au
katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa
fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
* *
*MIKOA YATAKIWA KUWASILISHA RATIBA COPA COCA-COLA*
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linavitaka vyama vya mpira wa
miguu vya mikoa kuwasilisha ratiba zao za michuano ya U15 Copa Coca-Cola
kabla ya Julai 15 mwaka huu.
Ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa 16 pekee ambavyo ndivyo vimewasilisha
TFF ratiba hizo mpaka sasa. Jumla ya mikoa 32 ya Tanzania Bara na Zanzibar
inashiriki katika michuano hiyo ya umri chini ya miaka 15 kuanzia ngazi ya
wilaya ambapo ngazi ya mikoa inatakiwa kuanza Julai 15 mwaka huu.
Mikoa ambayo tayari imewasilisha ratiba zao ni Arusha, Ilala, Kagera,
Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja, Kigoma, Kinondoni, Kusini Pemba, Kusini
Unguja, Manyara, Mara, Mjini Magharibi, Morogoro, Singida, Tanga na Temeke.
* *
WASH UNITED YAKABIDHI FULANI 200 KWA KLINIKI YA TFF
Taasisi ya Wash United inayojishughulisha na usaji na utunzaji mazingira
imeikabidhi fulana 200 na dola 1,000 za Marekani kwa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati
yake na TFF yaliyosainiwa Novemba mwaka jana.
Fulana hizo kwa ajili ya kliniki za kila wikiendi (Jumamosi na Jumapili)
zinazoendeshwa na TFF katika vituo 20 nchini kikiwemo cha Karume ikiwa ni
sehemu ya mpango wa grassroots unaoshirikisha watoto wa umri kati ya 6 na
17 zimekabidhiwa na Mratibu wa Wash United, Femin Mabachi.
Hafla ya kukabidhi msaada huo imefanyika leo (Julai 9 mwaka huu) kwenye
ofisi za TFF ambapo kwa upande wake ulipokelewa na Ofisa Maendeleo wake
Salum Madadi.
Wash United inafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la
maendeleo la GIZ, na hapa nchini moja ya eneo wanalotumia katika kampeni
hiyo ili kupambana na magonjwa kama kuhara yanayosababishwa na uchafu
ikiwemo kutonawa mikono vizuri, hivyo kusababisha vifo kwa Watanzania ni
mpira wa miguu.**