Katika wahamasishaji(influencers) wakubwa nchini Tanzania katika mitandao ya kijamii hauwezi kumuacha kumtaja bwana Haji Sunday Manara ambaye amejizolea umaarufu mkubwa Zaidi kupitia kiwanda cha soka. Haji anatokea katika familia ya soka na kizazi chake kina jina kubwa katika soka la Tanzania. Ukianzia kwa babu yake mzaa mama yake alikuwa ni mwenyekiti wa klabu ya soka ya Simba na inasemekana baba yake mzazi bwana Sunday Manara wakati anacheza klabu ya soka ya Yanga alipomposa kumuoa mama yake mzazi Haji tukio hilo lilizua mjadala mkubwa sana kwa wakati huo kwani ilionekana kama ni kitu cha ajabu sana kwa mchezaji tegemeo wa Yanga kwenda kuposa kwa kiongozi wa Simba na ilizua mjadala na hata baadhi ya watu hudai ndoa hiyo ilibidi ikafungwe sehemu nyingine na sio nyumbani kwa baba mzazi ili kuepusha maneno ambayo yaliyokuwa yameanza kujengeka. Mwenyewe Haji huwa ana picha za kumbukumbu ya kuzaliwa kwake ambapo magazeti yaliripoti juu ya kuzaliwa kwake.
Mzee Sunday Manara ndio alikuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya na hivyo kuanza kujenga alama yake katika soka la Tanzania. Alienda kucheza soka la kulipwa nchini Uholanzi na pia aliwahi kucheza soka la kulipwa katika taifa la Marekani katika nyakati ambapo gwiji wa soka kutoka taifa la Brazil bwana Pele ambaye naye katika nyakati hizo alikuwa anacheza katika ligi hiyo.
Kwenye soka la Tanzania Haji alianza kuweka alama yake kwa kuanza kama mchambuzi wa soka mwanzoni mwa miaka ya 2000 ambapo alikuwa anafanya kazi katika kituo cha Redio Uhuru ambacho kinamilikiwa na chama cha Mapinduzi. Zilipokuja nyakati za mageuzi ya teknolojia ya habari na mawasiliano bwana Haji ndipo alijikuta jina lake linakuwa kubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki pake alipopata mkataba wa kuwa msemaji wa klabu hiyo ya Msimbazi.
Uwezo wake wa kutengeneza kampeni za kuhamasisha mashabiki kujaza uwanja zilikuwa zinagusa hisia za wadau wengi wa soka na alijitahidi kuwa mbunifu wa misamiati mpya ambayo ilikuwa inafanya mechi ziwe zina msisimko kwa mashabiki. Misamiati kama ‘utopolo’ ilinogesha utani wa jadi baina ya mashabiki wa klabu za Simba na Yanga. Atakumbukwa sana mchango wake wa kuhamasisha mashabiki kutokea kwa wingi kwenye uwanja wa Benjamini William Mkapa kuishangilia klabu hiyo katika mechi za vilabu katika ngazi ya mashindano ya kimataifa.
Atakumbukwa Zaidi pale alipozungumza kauli za kutamba na kusema kwamba ndani ya uwanja wa Mkapa klabu ya Simba haiwezi kufungwa na klabu yoyote ile na alienda mbali na kusema kwamba hata ingeenda pale klabu kubwa duniani kama Barcelona, PSG na nyinginezo basi zisingiweza kupata matokeo ya ushindi katika uwanja ule. Ni dhahiri kwamba maneno yake yaliwajaza mashabiki wa klabu ya Simba ari ya kujiamini sana na matokeo yalipotokea kuwa mazuri katika mechi za nyumbani basi yaliongeza utamu wa ladha za mechi za kimataifa.
Katika nyakati zake kama msemaji wa klabu ya Simba alijiongezea umaarufu sana na kujikuta anapata mikataba mingi tofauti ya kutangaza bidhaa za makampuni mbalimbali ambazo zilishawishika kufanya naye biashara kwa kuwatangazia biashara zao. Klabu ya Simba kwa mafanikio waliyokuwa wanayapata kupitia mechi za nyumbani walifanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa pamoja na kubeba ubingwa wa ligi kuu Tanzania bara kwa mara kadhaa.
Baada ya misimu kadhaa kutumikia klabu ya Simba ilitokea hali ya kutoelewana baina yake na waajiri wake hali ambayo ilitengeneza mahusiano ambayo hayakuwa mazuri hadi kufikia kiwango cha kumweka pembeni na huo ndio ukawa mwisho way eye kutumikia klabu hiyo. Msimu uliofuatia lilitokea jambo ambalo halikudhaniwa hapo awali ambapo Haji akasajiliwa na klabu ya Yanga na kuhamia klabu hiyo na kwenda kuwa msemaji wa klabu hiyo. Alitambulishwa siku ya Yanga day ambapo huwa ni tamasha ambalo hufanyika kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi kuu bara.
Haji Manara katika msimu wake wa kwanza ndani ya klabu ya Yanga alipata bahati ya klabu hiyo kubeba ubingwa wa ligi kuu bara pamoja na kombe la Azam Confederation. Haji alijitapa sana kwenye mitandao ya kijamii kwamba Simba haitaweza kubeba ubingwa wa ligi kuu bara kwa misimu 5 mfululizo kwanu yeye alikuwa nguzo ya klabu hiyo kubeba mataji waliyobeba katika misimu ya hivi karibuni na hawatabeba tena mataji. Mashabiki wa Simba walikuwa wanaweka mitandaoni vipande vifupi vya maudhui( short video clips) ambazo zilikuwa zinamuonyesha kauli alizozikuwa anazitoa wakati yuko katika klabu ya Simba na kisha kumuonyesha kwamba amebadili misimamo yake pindi amehamia Yanga. Manara hakujali hayo aliendeleza utani wake kwa washabiki wa Simba na akawa anawatania kw asana na huku akiwakera.
Ilipofika mnamo mwezi Julani mwaka 2022 kamati ya nidhamu na maadili ya shirikisho la soka Tanzania ilimkuta na hatia Manara ya kutoa matamshi ambayo hayakuwa ya staha kwa raisi wa shirkisho la soka Tanzania bwana Wallace Karia katika mchezo fainali ya kombe la shirikisho ambao ulichezwa jijini Arusha kati ya Yanga na klabu ya Coastal Union. Alifungiwa kutojihusisha na masuala ya soka kwa miaka 2 na pia kulipa faini ya pesa kiasi cha shilioni milioni 20. Adhabu yake inaelekea kuishi na tayari ameshaanza kutoa matamshi ya kuwaweka mashabiki wake kukaa mkao wa kula kwani anarudi tena kwenye shughuli zake za soka. Swali ambalo mashabiki wa soka wanajiuliza ni jipya gani ambalo Haji Manara atakuja nalo?