Menu
in , ,

HADITHI YA KAGERE HAITOFAUTIANI NA YA OKWI

Tanzania Sports

Hutokesea kipindi utakaposema nyumbani kwa Emmanuel Okwi ni kwenye klabu ya Simba.

Hapa ndipo kwao, wazazi wake wamezaliwa hapa na ndugu zake wanapatikana hapa, kwa kifupi furaha yake inapatikana hapa.

Anadekezwa sana, anajaliwa sana kwa kifupi ni mtoto kipenzi kati ya watoto wa mzee msimbazi.

Ingawa mzee msimbazi hakumzaa yeye lakini amemfanya Emmanuel Okwi asipakumbuke Uganda kama ndiyo sehemu ambayo kitovu chake kilizikwa.

Huku ndiko pumzi yake ya kwanza aliivuta, lakini hapati furaha kama akiwa Msimbazi.

Sehemu ambayo mara nyingi huondoka na kurudi. Alitoka Uganda akaja Simba, majirani zake Simba wakamchukua na kumpeleka Jangwani.

Alienda Jangwani kwa sababu ya pesa, moyo wake haukuwepo kabisa Jangwani. Mwili ndiyo ulikuwepo pale Jangwani lakini moyo wake ulikuwa Msimbazi, ndiyo maana hakufanya vizuri alipokuwa na Yanga.

Haikuwa kazi rahisi kwake yeye kurudi tena msimbazi, nyota yake iliwaka tena kwa sababu alipata utulivu wa nafsi na kucheza bila hofu yoyote.

Amani ilimjaa moyoni, furaha ikatawala maisha yake ikawa rahisi kwake yeye kufunga na kutoa pasi za mwisho za magoli.

Kwa kifupi kiwango cha Emmanuel Okwi kilirudi katika kiwango cha juu, kiwango ambacho kilisababisha Simba wamuuze kwa pesa ndefu Tunisia.

Wengi tukajua huu ndiyo utakuwa mwisho wa Emmanuel Okwi kama mchezaji wa Simba.

Aliondoka, lakini alirudi nyumbani. Nyumbani ambapo anaamini kuna neema kubwa, neema ambayo ilimpa nafasi ya kwenda Ubelgiji.

Ubelgiji ambako hakucheza vizuri, na hakupata nafasi kubwa ya kucheza. Nafasi aliyoipata ni finyu.

Hakuwa na jinsi kurudi tena nyumbani, safari hii alirudi kwa kejeli kubwa sana kutoka kwa mashabiki wa Yanga.

Waliamini Simba wamemsajili “Mhenga” , waliamini umri wa Emmanuel Okwi ulikuwa mkubwa sana.

Waliamini kiwango chake kilikuwa kimepungua sana kutokana na umri wake.

Kejeli zilikuwa nyingi, na wengi waliamini kupitia kejeli kuwa Emmanuel Okwi hatocheza katika kiwango kikubwa kutokana na “Uhenga” wake.

Muda una majibu bora na sahihi siku zote, ndiyo maana muda wa ligi kuanza ulitupa majibu mengi ambayo yalikuwa tofauti na kejeli zetu.

Tulimkejeli Emmanuel Okwi kwa mdomo yeye alitukejeli kwa miguu. Miguu yake ilituadhibu sana.

Tulilia kilio kikubwa kila miguu ya Emmanuel Okwi ilipokuwa inapata mipira, alitusurubu haswaaa na sisi tukasurubika sana mpaka akawa mfungaji bora wa ligi kuu Tanzania bara.

Midomo yetu ilibaki kimya, hatukuwa na cha kusema kwa sababu Emmanuel Okwi alitujibu kuhusu “Uhenga” wake.

Ligi iliisha akawa shujaa dhidi ya midomo yetu. Kama ilivyo kazi ya midomo, imeumbiwa kuongea. Huwezi kuzuia midomo kuoongea hata siku moja.

Midomo huwa haijifunzi kutokana na makosa yake, ndiyo maana hata Simba ilipomsajili tena Meddie Kagere ndimi zetu zilipewa nafasi na midomo yetu kuongea.

Muda wa kumkejeli Meddie Kagere uliwadia tena, na kejeli zetu juu yake zilikuwa kama zile ambazo tulizitumia kipindi ambacho Emmanuel Okwi anasajiliwa na Simba msimu uliopita.

Tulimwiita Meddie Kagere “Mhenga”. Tulimkejeli tena kuwa hatofanya vizuri kwa sababu ya umri wake kuonekana mkubwa.

Lakini taratibu ameanza kutunyamazisha, mechi mbili ana magoli mawili tayari.

Taratibu midomo yetu imeanza kufunga kwa aibu. Inawezekana Meddie Kagere ni “Mhenga” kweli lakini ni “Mhenga” mwenye wepesi wa akili na mwili.

Ana ukomavu mkubwa kwenye maamuzi yake ndani ya uwanja, kitu hiki kinadhihirisha kuwa Meddie Kagere ni “Mhenga” haswaa tena “Mhenga” mwenye ukomavu mkubwa na anayejua kipi anachokifanya uwanjani.

Amewazidi wachezaji wetu wengi, na anapicha ya ufanisi kama ambayo Emmanuel Okwi.

Kikubwa ameongeza kitu kipya ambacho msimu jana hakikuwepo.

Msimu jana walipokuwa wanakosekana John Bocco na Emmanuel Okwi safu ya ushambuliaji ya Simba ulikuwa dhaifu sana.

Meddie Kagere ameleta ukomavu, uimara na upana wa kikosi hasa hasa eneo la mbele.

Written by Martin

Martin Kiyumbi ni mchambuzi wa habari za michezo na mbunifu wa maudhui.

Martin Kiyumbi amewahi kufanya kazi za uchambuzi kwenye vituo mbalimbali vya habari kama Tanzaniasports (tovuti ya habari za michezo ), Jembe FM , Radio Free Africa na TVE.
Martin Kiyumbi anapatikana kwenye e-mail ya martinkiyumbi@gmail.com

Exit mobile version