ALIYEWAHI kuwa kocha mkuu wa klabu ya Simba, Goran Kopunovic anadaiwa kukaribia kurudi tena klabu hapo kwa mara nyingine kurithi mikoba ya kocha aliyetimuliwa Dylan Kerr raia wa Uingereza.
Goran raia wa Croatia anakaribia kujiunga na klabu hiyo ambayo iliwahi kumtupia virago mapema mwezi Mei mwaka 2015 baada ya kushindwa kumlipa dau alilohitaji ili aendelee kuinoa timu hiyo.
Uamuzi wa Simba kumgeukia Goran Kopunovic umekuja baada ya uongozi wa klabu hiyo kushindwa kufika bei katika dau la kocha wa zamani wa ‘Taifa Stars’ Kim Poulsen raia wa Denmark.
Kigogo mmoja wa klabu ya Simba alifichua kuwa wameanza mazungumzo na Goran Kopunovic ili kumshawishi arejee nchini kukinoa kikosi cha timu hiyo akisaidiana na Jackson Mayanja raia wa Uganda.
Taarifa zinasema kuwa Kamati ya Utendaji ya Simba imelazimika kumpa jukumu kigogo huyo(jina tunalo) ili kumshawishi Goran kutokana na maelewano yake tangu alipokuwa hapa nchini.
“ Goran Kopunovic ni kocha mzuri na katika muda aliofanya kazi Simba tulianza kuiona timu ikipata mwelekeo, hivyo kigogo huyo anajitahidi kumshawishi kama atakubali huenda msimu ujao akakabidhiwa timu kuchukua mikoba Kerr,” alisema.
Goran alitua nchini mwanzoni mwa mwaka 2015 na kukiongoza kikosi cha SImba kwenye mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambacho alikisaidia kutwaa taji hilo.
“Huyo kocha hakuondoka kama ilivyo kwa makocha wengine waliopita Simba, aliamua kutimka mara baada ya kushindwa kukubali ofa yetu, hivyo ushawishi unaofanyika sasa tunaamini utafanikiwa kwani jamaa ni mtu wake wa karibu na hata muda wote huu walikua bado wana mawasiliano,” kilieleza chanzo hicho.
Hata hivyo Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba Haji Manara, hakuwa tayari kukubali wala kukanusha taarifa hizo akidai uongozi upo kwenye mchakato wa kutafuta, na washabiki watamfahamu mara baada ya kupatikana.