LICHA ya kuwa na msimu mgumu katika kazi yake, Olivier Giroud hakukata tamaa. Kwa miezi sita akiwa Chelsea chini ya kocha Frank Lampard, mshambuliaji huyo mkongwe alipata nafasi ya kuanza mechi mbili za Ligi Kuu. Kati ya Desemba 1 hadi Februari 16, hakucheza mechi yoyote. Alikalia benchi.
Giroud ni mkristu. Hakulazimisha kurejeshwa uwanjani haraka, lakini ametumia imani yake kuomba na kuwa mvumilivu katika kipindi kizuri na kigumu. Kwenye mkono wa kulia kwa mbele amechora tattoo kuonesha imani yake. kuna maandishi ya Kilatini aliyochukua kutoka kwenye biblia, “Bwana ndiye mlinzi wangu, kamwe sitaogopa,”
Ujumbe huo unaenda kokote aendako Giroud. Unamtuliza na kumpa amani. Lakini mambo yanapokuwa magumu amekuwa akizungumza na mchungaji wa Kanisa la Mtakatifu Barnabas lililopo Kensington kwa msaada zaidi.
Ratiba ngumu na mazoezi, hata kama akiachwa kwenye kikosi cha mechi, Giroud amekuwa yuleyule. Kila jumapili anahudhuria misa na kumtafuta mtu mwaminifu kwake kwa mazungumzo.
Itakuwa vigumu kupata muda wa kuzungumza naye wakati timu yake ya Chelsea inajiandaa kucheza fainali ya kombe la FA dhidi ya Arsenal jumamosi. Hii kwa kawaida ni wiki ngumu ya maandalizi, pamoja na mikutano mingi na vyombo vya habari.
Amefunga magoli 8 katika 11 alizocheza. Giroud amejiandaa kukabiliana na timu yake ya zamani Arsenal katika dimba la Wembley.
Ni tarehe 31 Januari mwaka 2018 siku ya makaubaliano ya uhamisho kati ya pande tatu; Arsenal,Chelsea na Giroud. Arsenal walizungumza na Borussia Dortmund kwa ajili ya kumsajili Pierre-Emerick Aubameyang, nao Borussia Dortmund walikuwa kwenye mazungumzo ya kumsajili kwa mkopo Michy Batshuayi, kisha Chelsea wakawa wanatafuta mbadala wa Mbelgiji huyo ndipo wakamsajili Giroud.
Klabu zote tatu zilikuwa kwenye presha kubwa kukamilisha mikataba kabla ya saa za mwisho za kufungwa dirisha la usajili.
Kama mfanyakazi wa zamani wa Arsenal alivyozungumzia mazingira hayo, “Ilikuwa mikataba ya pande tatu, kwa Batshuayi kwenda Dortmund na Aubameyang kuja kwetu Arsenal. Sio kila wakati soka limejengwa katika kuaminiana, lakini kwa mfano huo, timu zote tatu zilitakiwa kuaminiana hivyo hakuna iliyokuwa tayari kubadili mawazo au kuvunja mazungumzo. Chelsea walisema ikiwa watampa Giroud, watamtoa kwa mkopo Batshuayi kwenda Dortmund. Walisimamia kauli zao,”
Inaeleweka bosi wa usajili wa Arsenal, Dick Law ambaye alikuwa na uhusiano mzuri na Mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia, alimpigia simu siku ya kukamilisha dili la Giroud. Inasadikika ndiyo mshikamano uliofanikisha mengi.
Mchakato mzima ulienda kama ulivyopangwa. Giroud akasajiliwa Chelsea kwa pauni milioni 18, Aubameyang akaenda Arsenal kwa pauni milioni 56 na Batshuayi akaelekea Dortmund.
Kwa Giroud, ilikuwa na maana maisha yake ya miaka mitano na nusu kaskazini mwa London yalifika tamati. Ni kama alivyojaribu kutaka kuondoka Chelsea januari akihofia kuporwa namba katika kikosi cha Ufaransa kwenye michuano ya Euro mwaka huu.
Ukoefu wa mechi kwake ulikuwa na maana asingeitwa kikosi cha Ufaransa, hivyo kukosa mafanikio kama ya fainali za kombe la dunia za mwaka 2018 ambako waliibuka mabingwa.
Mfanyakazi wa zamani wa Arsenal alisema, “Olivier alitaka kuhama. Hakupenda kucheza mechi chache na alishakata tamaa, hakutaka tena kuwa mchezaji wa akiba.”
Ukweli, licha ya kufunga mabao 105 kwa Arsenal, bado alikabiliwa na changamoto ya kuthibitisha thamani yake na kuonesha ni mchezaji sahihi wa kuongoza safu ya ushambuliaji.
Hata kabla ya kusajiliwa akitokea Montpellier ada ya pauni milioni 13 mwaka 2012, msaka vipaji wa Arsenal Gilles Grimandi hakwenda uwanjani kumwangalia Giroud peke yake bali kumfuatilia kiungo . Remy Cabella. Inaaminika Aubameyang tangu alipokuwa kinda katika klabu ya Saint-Etienne alikuwa anafuatiliwa zaidi. Hata hivyo mabosi wa Arsenal walikuwa hawajaridhishwa na ubora wake.
Aubameyang alisajiliwa Arsenal kurithi nafasi ya Robin van Persie, ambaye alikuwa amejiunga na Manchester United. Walikuwa wamempata Lukas Podolski kutoka Cologne msimu huo kwa ada ya pauni milioni 10.9, huku Giroud akitakiwa kuwa mchezaji wa ‘plan B’.
Lakini Podolski hakufaa kucheza safu ya ushambuliaji wa kati, bali kucheza nyuma ya Giroud. Hapo ndipo Giroud akabadilishwa kuwa ‘Plan A’.
Wataalamu wa afya Asrenal walihangaika kuhakikisha Giroud ana stamina ya kutosha kwa sababu aliweza kucheza mechi vizuri mfululizo lakini zingine anaishia kuwa majeruhi.
Haikujalisha Giroud amefunga magoli mangapi, Arsenal walionekana kutoridhishwa na kiwango chake. Waliendelea kutafuta mshambuliaji mwingine.
Kiangazi 2013 walifanya jaribio la kumsajili Luiz Suarez na Gonzalo Higuan wa Real Madrid bila mafanikio. Walikaribia kumsajili Demba Ba kutoka Chelsea, lakini kocha Jose Mourinho aliharibu mpango huo kwani hakutaka kuwaimarisha wapinzani wake.
Walifanya jaribio lingine la kumsajili Jamie Vardy kutoka Leicester aliyesaidia klabu yake kutwaa taji la Ligi Kuu mwaka 2016. Kwa mara nyingine tena Arsenal walifeli kumsajili nyota huyo. Hadi hapo ujumbe ulikuwa wazi kwa Giroud, hivyo hata walipomsajili Alexandre Lacazette kutoka Olympique Lyon miezi 12 baadaye haikumshangaza
Kusajiliwa Aubameyang kulithibitisha kuwa Giroud hatakiwi, lakini yeye hakubadilika kitabia. Alisalia kuwa maarufu mazoezini na alifurahia urafiki na wachezaji wenzake akiwemo Laurent Koscielny. Muhimu zaidi, kocha wake Arsene Wenger alimwamini.
Giroud alizungumza na jarida la France Football mara baada ya kujiunga na Chelsea. Alisema, “Nilikwenda kuonana na Kocha (Wenger), lakini nilimkuta akiwa na Aubameyang. Nilisababisha awe na presha kidogo, kama nilivyoongea na wakala wangu mara kadhaa siku hiyo.
Sikulazimishwa kwenda Chelsea, ambako kulikuwa suluhisho kwangu kuliko kubaki Arsenal. Kocha aliniambia nisiwe na mashaka, atahakikisha nakuwa na furaha. Kwa upande mmoja ilikuwa kawaida, sikuomba kuhama Arsenal. Kwa upande mwingine nilifahamu hawezi kuniletea matatizo kutokana na maelewano yetu. Aliniambia itamuumiza mno akili kama nisingechaguliwa kikosi cha Ufaransa cha kwenda kushiriki fainali za Kombe la Dunia Urusi,”
Mtu anaweza kujiuliza kwanini Giroud alichagua kwenda Chelsea ambao ni wapinzani wa Arsenal badala ya timu nyingine au ligi tofauti. Klabu mbalimbali za Ufaransa zilimtaka Giroud lakini mkewe Jennifer alitaka wabakie England. Hiyo ikawa sababu yay eye kujiunga Chelsea. Inasemakana ni Jennifer pia ndiye aliyechangia nyota huyo kubaki Chelsea msimu ulioisha.
Tangu Giroud ajiunge Chelsea amesaidia kutwaa kombe la FA mwaka 2018, mfungaji bora kwenye Europa League akiwa na mabao 11. Lakini kwenye mchezo wa fainali ya Europa League alikabiliana na washambuliaji waliosajiliwa kuchukua nafasi yake pale Arsenal, yaani Aubameyang or Lacazette, ambao hawakuwa na madhara yoyote siku hiyo.
Baada ya ushindi huo Jorginho akiwa ndani ya Basi la klabu ya Chelsea aliimba kuwashukuru Arsenal kumuuza Giroud kwao. Alikuwa ameshika kombe la Europa League na kutamka “Asanteni sana Arsenal” kwa lengo la kumshukuru Giroud aliyepachika bao siku ya fainali.
Giroud ana kismati na kombe la FA. Endapo mashabiki wa Arsenal wataruhusiwa kuingia dimba la Wembley bila shaka watamhofia Giroud. Hata mashabiki wa Chelsea wataliimba jina lake kwani wanathamini mchango aliotoa kwenye klabu yao. Miaka mitatu iliyopita alitoa pasi ya bao kwa Aaron Ramsey na kumnyima ushindi kocha Antonio Conte alipokuwa Chelsea.
Msimu wa 2019-2020 ulianza vibaya kwa Giroud. Amejikuta akiwa mshambuliaji wa akiba. Kwanza aliwekwa benchi na Alvaro Morata, kisha Gonzalo Higuan, na sasa kinda Tammy Abraham anaongoza safu ya ushambuliaji huku Giroud akiwa benchi. Kimahesabu Giroud ana uzoefu mkubwa kuliko Tammy Abraham.
Uzoefu huo ulionekana siku ya mchezo wa Super Cup dhidi ya Liverpool ambapo Lampard aliamua kumpanga Giroud kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza baada ya miezi mitatu chini ya kocha huyo.
Hata hivyo Giroud alitolewa na nafasi yake ikchukuliwa na Tammy Abraham ambaye alikosa penati ya mwisho ambayo ingewapatia ubingwa Chelsea. Hilo lilisababisha mashambulizi makali na ubaguzi dhidi ya Tammy kwenye mitandao ya kijamii, lakini Giroud alimtumia ujumbe wa kumtia moyo bila kujali tofauti za kiufundi kati yake na kocha Lampard. Giroud alituma ujumbe kutoka kwenye biblia, Isaya 10; 27-31.
Wakati akiwa ansikitishwa kuwa chaguo la tatu baada ya Abraham na Batshuayi, lakini hakuonesha hadharani huzuni yake. Wachezaji wenzake wanavutiwa na tabia yake kwa kipindi chote anachopuuzwa na kuwekwa benchi.
Jinsi anavyoongea nao. Jinsi anavyocheka nao. Jinsi anavyojinyima kulalamika. Jinsi anavyotulia licha ya kuachwa kikosini. Ni kivutio kwa wenzake.
Beki Antonio Rudiger anasema, “Kwanza, namheshimu sana Giroud. Ni mkimya, daima amekaa kiweledi, anafakazi sana, anapambana kureudisha nafasi yake. Amekuwa na msimu mgumu, kwa miezi sita ya kwanza hakuwa katika hali hii. Pakawa na tetesi anaondoka.
Sote ni binadamu, kuna wakati huwi kawaida hasa kama huchezi. Lakini wakati wote yuko kawaida, iwe anacheza au yuko jukwaani. Akiwa kwenye benchi anahamasisha timu nzima, hana chuki. Ni kiongozi mzuri. Ni mtu ambaye unaweza kuongea nae chochote mkaelewana. Ametwaa kombe la dunia. Anajiamini na kombe la dunia limemwongezea zaidi kujiamini. Ila hana majivuno,”
Lampard ni miongoni mwa wanaokiri hilo, anasema mshambuliaji huyo ana uwezo wa kuwatisha wapinzani na kuleta madhara langoni mwao, lakini hajaimarika kiuwezo.
Akizungumzia kuwekwa benchi, Giroud amewahi kusema, “kuna matendo mawili ya kuachwa kikosini. Kwanza ni kuinamisha kichwa chini na kuanza kulaumu kwanini huchezi. Nyingine ni kutumia mfadhaiko huo kwa njia chanya, kuboresha hisia zako na kurudisha namba kushindana na kufanya mazoezi kwa wingi,”
Januari Chelsea walizungumza na timu za Inter Milan na Tottenham, lakini dili lilivunjika, pale waliposhindwa kuwasajili Dries Mertens (Napoli) na Edinson Cavani(Paris Saint-Germain).
Lampard na Giroud walizungumza juu ya hali ya kuwekwa benchi. Lampard akaahidi mabadiliko na kumpa nafasi Giroud. Akafanikiwa kucheza mechi kadhaa tangu hapo. Hata kipindi cha mlipuko wa ugonjwa Corona, Giroud aliendelera kufanya mazoezi ya nguvu kujiweka katika hali nzuri.
Tukio la kukumbukwa zaidi ni pale Giroud alipofunga bao muhimu dhidi ya Wolves ambalo liliipa nafasi Chelsea ya kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao kwa kumaliza nafasi ya nne.
Lampard alizungumzia bao hilo na mchango wa Giroud kwa kusema, “Sitaki kuonekana nina busara, nataka kusema tangu januari sitakata Giroud aondoka, nafahamu nini anachokiongeza katika timu na mazoezini kila siku. Sio kwamba ni kiongozi mpendwa, lakini ana haiba yake na kipaji kizuri. Ameimarisha safu ya ushambuliaji akiwa na Mason Mount, Christian Pulisic na Willian,”
Hata hivyo, msimu wa 2020-2021 unaonekana utakuwa vilevile kama misimu mingine kwa Giroud. Chelsea wamemsajili Timo Werner kwa pauni milioni 47.
Hata hivyo fainali ya FA wikiendi hii itakuwa ni kama bustani mpya kwa Giroud kama atafanikiwa kunyakua taji ndani ya dimba la Wembley. Giroud hajawahi kukosa kombe hilo kila alipofika fainali.