Ghana wamekata tiketi kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) katika mazingira magumu, baada ya washabiki wa wenyeji Guinea ya Ikweta kuwashambulia wachezaji na maofisa, kwa madai ya kutoridhishwa na mwamuzi.
Black Stars walishinda 3-0 na kukatisha ndoto za alinacha za wenyeji kufika fainali, baadaya kuwa wametinga nusu fainali kiutata kwa ushindi dhidi ya Tunisia wa 2-1, ambapo mwamuzi aliyechezesha amefungiwa miezi sita.
Vurugu zilianza kwa washabiki kurusha chupa za maji uwanjani, lakini pia vitu kama sahani na mawe viliokotwa dimbani baadaye, ikabidi mchezo usitishwe kwa muda, wachezaji wakingwe kwenda vyumbani na polisi watumie mabomu ya kutoza machozi dhidi ya washabiki wakorofi, huku helikopta ya polisi ikirandaranda juu ya dimba kuhakikisha usalama.
Wachezaji wa Guinea ya Ikweta nao waliathiriwana vurugu hizo mjini Malabo, waliokuwapo wakielezea kwamba ilikuwa kama hali ya kivita, washabiki wa Ghana wakakimbia kujificha nyuma ya lango lao ili kuepuka kupigwa na wale wa wapinzani wao. Mashabiki kadhaa wamedakwa na polisi, na wapo waliomsogelea mwamuzi kumchapa.
Mechi hiyo iliyosimamishwa kwa dakika 30 ilirejea baada ya polisi kufanikiwa kutuliza ghasia na kuimarisha ulinzi kila upande, na sasa Ghana watacheza dhidi ya Ivory Coast katika mechi inayotarajiwa kuwa tamu Jumapili hii. Ivory Coast waliwatoa Kongo Kinshasa kwa mabao 3-1 Jumatano.
Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilitumia vipaza sauti kutishia kufutilia mbali mechi hiyo iwapo washabiki wangeendeleza fujo lakini Rais wa Chama cha Soka cha Ghana, Kwesi Nyantakyi baada ya mechi alisema halikuwa tukio kubwa kihivyo, bali palikuwapo njama za kuitia doa Afrika kwa kulikuza.
Mabao ya Ghana yalifungwa na Jordan Ayew katika dakika ya 42 baadaya Kwesi Appiah kuchezewa visivyo na kipa Felipe Ovono. Dakika tatu tu baadaye waliongeza bao la pili kupitia kwa Mubarak Wakaso baada ya shambulizi la kushitukiza.
Ni baada ya mabao hayo na wakati wa mapumziko ndipo washabiki walianza vurugu, pengine wakitaka yatokee ya kwenye mchezo wao na Tunisia uliopita ambapo walipewa penati isiyokuwa halali dakika ya 90 na hatimaye kuja kuibuka na ushindi.
Bao la tatu na lililotia msumari wa mwisho kwenye jeneza la wenyeji lilifungwa na Andre Ayew katika dakika ya 75 na baada ya hapo, washabiki walianza kutafuta pa kujificha.