Maisha chini ya Gennaro Gattuso pale AC Milan yamebadilika sana. Matokeo yanaonekana kuja upande wao vizuri sana tofauti kabisa na matarajio akiwa ameiongoza timu hiyo mara 13 na kushinda 9 na sare 4 huku akiwa amekwenda zaidi ya dakika 500 bila kuishuhudia timu yake ikiruhusu bao pia.
Lakini Kama kuna kitu ambacho kinamsaidia mbabe huyo wa soka kwenye uongozi wake pale AC Milan basi ni utu ama “Personality” yake kwa kimombo.
Ni kweli alikuwa mkorofi enzi za uchezaji wake lakini ile picha imejenga heshima kubwa kutoka kwa wachezaji wake.
Sio kwamba atampiga mtu kichwa pale atakapokosea! lakini anaondoa ile hali ya kujisikia na timu inacheza kwa ajili ya kulinda na pengine kurudisha sura ya timu yenyewe. Hata hamasa inakuwa kubwa na matokeo huwa yanatafutwa kibabe sana.
Ignazio Abate sasa hivi hapati namba kisa ufaza. Kocha haitumi nafsi kufanya vile isivoweza lakini bidii iwepo na ujue mwalimu anataka nini.
Hata Antoinne Griezmann mwanzoni aliona mambo magumu pale Atletico Madrid lakini alipojua mahitaji ya Diego Simeone ni nini basi akajitoa mazima. Mwenyewe amekiri hivyo kwa kauli yake.
Wakati mwengine utu na mtiririko wa sifa za aina fulani za mtu huwa zinamjengea hata sifa fulani kutokana na tabia hizo hata hapo baadae hasa kwenye swala zima la uongozi.
Akiwa kama kocha zile sifa na tabia zake kiuchezaji zimeleta nguvu kubwa hasa kwenye swala la nidhamu na kuwa na nguvu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo pia. Ushawishi wa Gattuso kuanzia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo hadi uwanjani umekuwa ni mkubwa. Ukorofi wake umemsaidia akiwa mchezaji kwani sasa unampa heshima kubwa kama kocha.