Msimu wa mwaka juzi klabu ya DTB ndio klabu ambayo iliyokuwa inasumbua ligi ya soka ya daraja la kwanza (championship na ndio ilikuwa bingwa wa ligi hiyo. Walipata ubingwa kabla mechi za msimu hazijaisha na katika msimu huo walionyesha dhahiri kwamba wana kiu ya kufika mbali katika soka la Tanzania kwani katika msimu huo walikuwa wamemsajili mashambuliaji wa kimataifa kutoka Burundi namzungumzia hamisi Tambwe mchezaji ambaye alikuwa anacheza soka lake la kulipwa katika klabu ya Arta Solar ya nchini Djibouti.
Tambwe katika mechi zake tatu za mwanzo wa msimu huo alikuwa tayari ameshapata hat trick. Walikuwa wana wachezaji mahiri kama James Kotei ambaye aliwahi kutumikia wababe wa mtaa wa Msimbazi kariakoo yaani Simba. Tambwe hakuweza kumaliza kucheza mechi tano za awali za msimu huo kwani alipata majeraha ambayo yakamfanya akashindwa kucheza mechi kadhaa kutokana na kuumizwa katika mchezo dhidi ya klabu ya Green Warriors ambayo makazi yake ni Mwenge jijini Dar es salaam. Katika nyakati hizo klabu hiyo ilikuwa chini mtendaji mkuu wa klabu bwana Muhibu Kanu. Kwa wakati huo klabu hiyo makazi yake yalikuwa jijini Dar es salaam na msimu huo walitia fora kwa kuvifunga vilabu ambavyo vilikuwa vinashiriki ligi hiyo.
Hakika klabu hiyo ilianza kutengeneza galacticos ya namna yake katika soka la Tanzania. Galacticos ni msamiati ambao ulibuniwa na rais wa klabu ya Real Madrid ya uhispania baada ya kushinda uraisi wa klabu hiyo na kasha akaanza kufanya usajili wa wachezaji wakubwa wa nyakati hizo ambao walikuwa wanawika katika soka la ulaya. Aliwasajili wachezaji kama vile Luis figo, Zinedine Zidane, David Beckham, Ronaldo de Lima na Michael Owen.
Hakika kikosi hiki kilivutia sana na licha ya kwamba hakikushinda mataji mengi makubwa ila kilivutia mamilioni ya mashabiki kufuatilia mechi za Real Madrid na kukifanya kiwe ni klabu ya michezo yenye nembo kubwa duniani. Ukubwa huo ambao ulianzishwa ni zama hizo za galacticos umeendelea kuwa mpaka hivi leo.
Florentino Perez amepata heshima sana toka alipkuja na dhana hiyo ya Galacticos na hata bilionea wa kirusi bwana Roman Abramovich alipoinunua klabu ya Chelsea mwaka 2003 naye alitembelea dhana hiyo hiyo na akasajili wachezaji wakubwa na mashuhuri duniani na kuwahamishia makazi yao katika uwanja wa Stamford Bridge jijini London. Vilabu vya Manchester City na PSG navyo vimefuata muundo huo huo.
Dhana ya Galacticos ndio dhana ambayo klabu ya Singida illibeba na kuitumia.Msimu uliofuatia klabu hiyo ilihamia jijini Singida na kuamua kubadilisha jina la klabu hiyo na kujiita Singida Big Stars. Katika kuhamia huko nako walihamia kwa mbwembwe kwani walisajili wachezaji wakubwa na wenye uzoefu katika soka la Tanzania na hivyo kulibeba taswira ya jina la Big stars.
Wakamchukua mpachika mabao mzoefu kutoka Rwanda ambaye alikuwa anachezea klabu ya Simba bwana Meddie Kagere wakamchukua beki wa kimataifa wa Tanzania bwana Gadiel Michael beki wa kimataifa wa ivory coast bwana Pascal Wawa, beki wa kimataifa wa Kenya bwana Joash Onyango, kiungo wa kimataifa wa Tanzania Thomas Ulimwengu, wakasajili kiungo wa kimataifa wa Brazil bwana Bruno, kipa wa kimataifa wa Tanzania bwana Beno Kakolanya na wengineo wengi.
Kwenye benchi la ufundi wakamchukua kocha wa kimataifa toka uholanzi bwana Hans Van Pluijm ambaye ana uzoefu mkubwa sana na coka la Tanzania na Afrika kiujumla. Katika utendaji wa klabu hiyo wakamuajiri afisa mtendaji mkuu bwana Olebile Sikwane ambaye alitokea ukanda wa kusini mwa Afrika ili kuifanya klabu hiyo iweze kujitanua kimataifa na wakamuajiri afisa masoko mwanadada Nyaisa Kadenge ambaye alikuwa anatokea nchi ya Zimbabwe.
Katika msimu wake wa kwanza klabu hiyo ilifanikiwa kufuzu kushiriki katika mashindano ya shirikisho la barani Afrika. Katika kuingia kwake katika kombe la shirikisho klabu hiyo iliuza sehemu za hisa za klabu hiyo kwa taasisi ya Fountain Gate ambayo makao makuu yake Dodoma na ikabadilisha jina na kujiita Singida Fountain Gate. Walishiriki mashindano ya shirikisho na hawakuweza kufika hatua kubwa sana katika mashindano hayo. Katika msimu huu wamebadilisha makocha kwa mara kadhaa na sasa wanafundishwa na kocha mzawa bwana Jamhuri kihwelo maarufu kama Julio.
Bodi ya ligi ikawaamua kwamba wabadilishe uwanja wa kuchezea mechi zao za nyumbani kutokana na mapungufu kadhaa ambayo uwanja wa Singida ulikuwa nao na hii ikapelekea klabu hiyo kutumia uwanja wa Black Rhino Academy ambao upo Karatu mkoani Manyara. Siku si nyingi tukaona klabu hiyo ikahama na kwa sasa klabu hiyo inatumia uwanja wa Mwanza kama uwanja wake wa nyumbani.
Licha ya kuhamia Mwanza tumeona klabu hiyo iko katika changamoto ya kulipa faini kadhaa ambazo iliamrishwa na shirikisho la soka duniani FIFA kutokana na madai ambayo yalifunguliwa na baadhi ya wachezaji wake. Na bila ya shaka klabu hiyo ilitikisika kwa kiasi Fulani kwani ililazimika kuuza baadhi ya wachezaji wake ikiwemo Gadiel Michael kwenda vilabu kadha ikaachana na mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda bwana Meddie Kagere kwenda klabu ya Namungo ya mkoani Lindi.
Klabu hiyo kwa sasa imepungua kidogo msisimko kutokana na kutokuwa na matokeo mazuri sana na hali ya kuhama mikoa imepunguza mashabiki kwa kiasi Fulani. Msimu ndio unaelekea ukingoni na klabu ya Singida haina dalili ya kuwa klabu bingwa msimu huu na mashabiki wa soka wanasubiria kwa hamu klabu hiyo itafanya nini kwenye dirisha lijalo la usajili kwani klabu hiyo imejipambanua kuwa ni miongoni mwa vilabu ambavyo vyenye uwezo wa kusajili mastaa. Je itaweza kusajili mastaa tena wa kusisimua soka la afrika mashariki? Je itaendelea kutumia jina la singida licha ya kwamba imehama mkoa wa Singida? Je itafuzu tena kushiriki mashindano ya kimataifa?. Majibu ya maswali hayo yatajibiwa na muda.