Berbatov kurudi Ligi Kuu EPL
*Chelsea, Man City wamgombea Koke
*Liverpool Aubameyang, Man U Clyne
Mshambuliaji mahiri wa zamani wa Manchester United na Tottenham Hotspur, Dimitar Berbatov huenda akarejea Ligi Kuu ya England (EPL).
Klabu iliyopanda daraja na itakayocheza EPL msimu ujao, Bournemouth, wanataka kumchukua Berbatov (34) kutoka Monaco, Ufaransa ili achangie uzoefu wake kwa vijana walio nao kwenye michuano hiyo mikubwa.
Monaco wanaweza kutaka kumuuza Bernatov ili wawe ndani ya kanuni za uungwana katika matumizi ya fedha, kwani ndio wametoka kupigwa faini ya pauni milioni 9.5 na Uefa kutokana na matumizi yao makubwa. Wanaruhusiwa kusajili kikosi chenye watu 22 tu kwa msimu ujao.
Berbatov aliyejiunga na Monaco akitoka Fulham Januari mwaka jana anapenda kurejea England kwenye ligi kuu maarufu kuliko zote duniani. Hata hivyo, bosi wa Bournemouth, Eddie Howe amesema hawatatumia fedha nyingi kwa ada za uhamisho lakini wanaweza pia kumpata Berbatov bure lakini watokwe jasho kwa kumlipa mshahara wa pauni 100,000 kwa wiki.
Chelsea wanachuana na Manchester City kumsajili kiungo wa Atletico Madrid, Koke, 23. Mchezaji huyo anawaniwa pia na Manchester City, kwani wanatafuta mrithi wa Yaya Toure anayetarajiwa kuondoka Etihad kiangazi hiki.
Kocha wa zamani wa City, Roberto Mancini anapenda kumsajili Toure na kuna habari kwamba Mancini anayefundisha Inter Milan yupo tayari kumlipa pauni milioni10 kwa msimu ili akipige San Siro.
Japokuwa Man City hawataweza kumuuza Toure kwa bei kubwa sana, wanao uwezo kifedha wa kuchuana na Chelsea kumpata Koke na inaelezwa kwamba kocha Manuel Pellegrini amemweka mchezaji huyo kuwa kipaumbele chake.
Koke amecheza mechi 51 kwa klabu na nchi yake msimu huu,ambapoa mefunga mabao manne lakini amelambwa kadi 14 za njano.
Chelsea na Liverpool zimeingia katika ushindani wa kutafuta saini ya kiungo wa Juventus, Andrea Pirlo, 35, wakiamini kwamba utimamu wake wa mwili na kutoyumba katika kiwango kwa muda mrefu vitawasaidia msimu ujao wa ligi.
Manchester United wanasemekana wameongeza dau la pauni milioni 18 kwa ajili ya kumnasa beki wa kulia wa Southampton na England, Nathaniel Clyne, 24.
Wolfsburg wa Ujerumani wamesema kwamba watataka walipwe pauni milioni 45 na klabu inayomtaka mshambuliaji wa zamani wa Chelsea anayewaniwa na Manchester City, Kevin De Bruyne, 23.
Queen Park Rangers (QPR) wanafikiria kumchukua kocha msaidizi wa Real Madrid, Paul Clement au bosi wa Brentford, Mark Warburton ili kuchukua nafasi ya kocha wa sasa, Chris Ramsey. QPR wanaelekea kushuka daraja.
Liverpool wameeleza nia yao ya kumsajili mshambuliaji wa Borussia Dortmund, Pierre-Emerick Aubameyang, 25. Mchezaji huyo wa Gabon alitamba kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka huu.
Liverpool pia wanataka kumsajili mlinzi wa Chelsea, Andreas Christensen na wapo tayari kutoa pauni milioni sita ili kumpata. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 anaweza kuchezea beki ya kulia au ya kati lakini amecheza mechi mbili tu chini ya Jose Mourinho.
Manchester United wanaelekea kumkosa mshambuliaji wa Paris St-Germain (PSG), Edinson Cavani, 28, kwani raia huyo wa Uruguayan anatarajiwa kujiunga na Juventus wa Italia.
Beki wa Liverpool, Martin Skrtel, 30, amesema anataka kubaki klabuni Anfield licha ya kushindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya. Klabu ya Wolfsburg, Napoli na Inter Milan zinafuatilia kwa karibu ili kumsajili ikiwa ataondoka.
Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho amesema itamuwia ngumu kuiga mkao katika klabu moja kwa muda mrefu kama walivyofanya Sir Alex Ferguson na Arsene Wenger.