Klabu ya Ligi Kuu ya England (EPL), Fulham imeuzwa kwa raia wa Marekani mwenye asili ya Pakistan, Shahid Khan.
Timu ya klabu hiyo inafundishwa na kocha Mholanzi Martin Jol, na imekuwa na kawaida ya kuwa katikati ya msimamo wa ligi, wakishindwa kutwaa vikombe lakini pia wakiepuka kushuka daraja.
Mmiliki wa klabu hiyo kwa miaka 16, Mohamed Al Fayed ameamua kuachana nayo, na sasa itakuwa chini ya bilionea mwenye umri wa miaka 62, anayemiliki pia klabu ya Jacksonville Jaguars inayoshiriki Ligi ya NFL.
Khan amewekeza zaidi kwenye biashara ya vipuri vya magari na anakuwa Mmarekani wa sita kumiliki klabu inayocheza EPL.
Al Fayed (84), raia wa Misri alifanikiwa kuwekeza kwenye soka, akawapandisha Fulham kutoka daraja la tatu hadi EPL, na anasema alifurahia muda wote akiwa mmiliki na mwenyekiti wa Fulham, lakini wakati wa kuondoka umewadia.
Haijawekwa wazi klabu hiyo yenye makazi yake Craven Cottage imeuzwa kwa bei gani, lakini tetesi zinasema dau lililotembea hapo ni kati ya pauni milioni 150 na 200.
Majina ya utani ya klabu hiyo ni The Lilywhites, The Cottagers au The Whites na ni moja ya timu zinazosumbua vigogo, hasa vinapokwenda kucheza katika dimba lao lililo kusini magharibi mwa London.
Msimu uliopita Fulham walimaliza katika nafasi ya 12, ambapo kundi linaloongoza kwa ushabiki katika klabu hiyo lilisema kuuzwa kwa klabu ni habari za kusisimua, lakini kuna sintofahamu katika hatima yao.
Mmiliki mpya, Khan aliondoka Pakistan kwenda Marekani akiwa na umri wa miaka 16, akasoma Chuo Kikuu cha Illinois katika fani ya uhandisi viwanda, utaalamu aliotumia kujenga kiwanda
kilichoajiri watu 16,000.
Akizungumzia uwapowake Fulham baada ya kuinunua, Khan alisema:
“Fulham ni klabu sahihi kwa wakati mwafaka. Nataka nieleweke, sijichukulii kama mmiliki wa Fulham, bali mtu anayeitunza kwa niaba ya washabiki.
“Kipaumbele change ni kuhakikisha klabu inakuwa na uendelevu na uthabiti katika Ligi Kuu, hivyo kwamba washabiki wa sasa na wajao waijivunie.
“Tutasimamia masuala ya fedha na operesheni ya klabu hii kwa uaminifu na uangalifu mkubwa, ikiwa ni pamoja na kuendeleza timu za vijana na kuendesha miradi ya jamii,” akasema Khan.
Khan aliinunua Jacksonville Jaguars Desemba 2011.