Nyota wa Ufaransa, Frank Ribery ameondolewa
kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Ufaransa kitakachoshiriki kwenye fainali za Kombe la Dunia.
Ribery (31) aliumia vibaya mgongo akiwa mazoezini na hivyo Kocha Didier Deschamps kukosa jingine la kufanya zaidi ya kumwondosha kikosini.
Kocha huyo wa Les Bleus amesema kwamba Ribery aliumia Ijumaa na hataweza kufanya mazoezi wala kucheza soka kwa majuma kadhaa.
Ribery alikuwa tegemeo kubwa, akiwa mahiri katika kuambaa na mpira kwenye wingi na kumimina majalo, ambapo angeshirikiana vyema na Olivier Giroud wa Arsenal.
Ribery anayechezea Bayern Munich amekipiga katika timu ya taifa mara 81 na kushiriki michuano ya Kombe la Dunia 2006 na 2010 na kuifungia timu hiyo mabao 16.
Mchezaji wa Lyon, Clement Grenier pia ameondolewa kwenye kikosi hicho baada ya kuumia hivyo mchezaji wa Southampton, Morgan Schneiderlin na Remy Cabella wa Montpellier wameitwa kuziba mapengo hayo.
Ribery amekuwa mchezaji bora wa Ufaransa kwa miaka mitatu na alichangia kwa kiasi kikubwa Ufaransa kufuzu kwa fainali hizi ambapo alifunga mabao matano.
Ribery mwaka jana alipigiwa kura na kushika nafasi ya tatu kwa uchezaji bora duniani, nyuma ya Cristiano Ronaldo wa Real Madrid na Lionel Messi wa Barcelona.