*Wamtaka Fabregas, Arsenal njiapanda
Kiungo mahiri wa Chelsea, Frank Lampard anaondoka klabuni hapo baada ya kutoafikiana juu ya mkataba mpya.
Lampard (35) ambaye anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya Chelsea alipenda kubaki lakini mazingira hayaruhusu.
Lampard aliye na Timu ya Taifa ya England ameitumikia klabu kwa misimu 13, akafunga mabao 211 na kuwazidi hata waliokuwa washambuliaji mahiri wa zama zote.
Alijiunga Chelsea akitoka West Ham 2001 na anakiri kwamba klabu hiyo imekuwa sehemu ya maisha yake na sasa ana ofa kutoka klabu nyingine 16 lakini anafikiria pia kustaafu soka.
Hata hivyo, pamekuwapo taarifa kwamba atakwenda Marekani kuchezea klabu kubwa ya huko wakati mjomba wake, Harry Redknapp anayefundisha Queen Park Rangers (QPR) angependa kumsajili lakini ni vigumu.
Alisajiliwa Chelsea kwa pauni milioni 11, akacheza mechi 648, akiwa mchezaji wa tatu kwa kucheza mechi nyingi zaidi, nyuma ya Ron Harris (795) na Peter Bonetti aliyecheza mechi 729.
Anakuwa mchezaji mwandamizi wa pili kuondoka Stamford Bridge msimu huu baada ya beki wa kushoto, Ashley Cole (33) aliyecheza hapo kwa miaka minane.
CHELSEA WAMFUKUZIA FABREGAS
Kuondoka kwa mchezaji huyo kunawafanya Chelsea kutafuta kiungo mwingine, na wameanza mbio za kumsajili Cesc Fabregas anayeuzwa na Barcelona kwa pauni milioni 30.
Fabregas (27) anapenda kurudi Ligi Kuu ya England lakini ni tamaa yake kurudi Arsenal alikoanzia katika umri mdogo akitoka akademia ya La Masia ya Barcelona.
Arsenal wamekuwa wakipata ufufutende katika kumsajili, ambapo klabu nyingine inayosemwa kumhitaji ilikuwa Manchester United ambayo imeghairi na Man City wanasubiri kuona hatima ya Yaya Toure aliyetishia kuondoka.
Hata hivyo, baada ya habari kuwa Chelsea, wapinzani wa Arsenal jijini London, wanataka kumsajili Fabregas, inasemekana wakuu wa Emirates wanakaa kutafakari upya.
Tatizo lao ni kwamba tayari katika nafasi ya Fabregas wapo viungo mahiri katika Mesut Ozil, Aaron Ramsey, Jack Wilshere na Santi Cazorla.
Arsenal wanalindwa na kifungu cha mkataba wa nahodha wao huyo wa zamani kuambiwa ikiwa anauzwa na timu gani inatoa dau gani, wakiamua kulipandia watauziwa lakini sasa wanapenda zaidi kuimarisha timu kwenye eneo la ushambuliaji na kiungo wakabaji.
Viungo wengine ambao Chelsea wanaweza kusajili kuziba pengo la Lampard ni Koke wa Atletico Madrid, aliyewahangaisha sana Chelsea kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.