Kama mashabiki wa Chelsea walitarajia mambo makubw akutoka kwa kocha wao kijana Frank Lampard sasa wanaweza kuona hali halisi kuwa mambo si mazuri kama wanavyodhani. Hadi kufika Januari 20 mwaka 2021 hakuna dalili kama mkongwe huyo wa zamani anaweza kupindua meza na kuibuka na taji la EPL msimu huu.
Msimu uliopita ulichukuliwa kama sehemu ya kujifunza kwa kocha huyo kijana, akiwa na miaka miwili katika kazi hiyo. Licha ya ugeni wake katika LiginKuu England, alifanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kumaliza nafasi nne za juu.
Msimu huu Lampard alianza kwa usajili wa nguvu baada ya kuwavua mastaa kama vile Thiago Silva, Timo Warner, Mendy na wengineo. Usajili wa mastaa bado haujampa uhakika wa kufanya vizuri msimu huu.
Mshambuliaji wake mpya Timo Warner alicheza mechi 14 na kutumbukiza wavuni bao moja pekee. Kwa mshambuliaji hiyo ni hatua mbaya lakini huwa inawakumba washambuliaji mara nyingi.
Katika msimu wa kwanza Lampard aliwategemea zaidi vijana ambao hawakumwangusha na walifanikiwa kufuzu Ligi ya Mabingwa. Mason Mount, Tomori, Kepa,Kurt Zouma ni baadhi ya vijana waliotegemewa kuifikisha mbali Chelsea.
Mabosi wa Chelsea wanafahamu kuwa wakati wanamwajiri Lampard kuwa kocha wao alikuwa na uzoefu wa mwaka mmoja pekee katika kazi hiyo. Klabu pekee aliyoiongoza ni Derby Country iliyopo daraja la kwanza. Mafanikio machache aliyopata akiwa Derby Country ndiyo yalimwezesha kukabidhiwa jukumu la kuinoa Chelsea.
Hivyo basi kwa matokeo ya sasa mabosi wa Chelsea bila shaka hawatoshangazwa. Chelsea wamechreza mechi 19 za Ligi Kuu England msimu huu na kujikusanyia pointi 29 wakiwa nafasi ya 8 katika msimamo wa Ligi hiyo.
Isivyo bahati Chelsea wanazidiwa pointi hata na klabu ya Leicester City ambao katika michezo hiyo hiyo 19 wamevuna pointin 38. Mbaya zaidi kwenye mchezo wao dhidi ya Chelsea katikati yawiki hii, Leicester City waliibuka washindi hivyo kupata pointi tatu muhimu.
Wikiendi iliyopita Chelsea walishinda bao 1 kwa nunge dhidi ya Fulham ikiwa ni ushindi wao wa pili katika mechi saba za hivi karibuni.
Wakati Lampard aliojiunga alikuta kikosi kidogo, kisha akampoteza mchezaji wa kutegemewa Eden Hazard na pia walikuwa wanatumikia adhabu ya kutofanya usajili.
Na sasa ili aweze kushindana vilivyo, walihitajika kuwekeza pesa zaidi katika kupata wachezaji wazuri. Lampard amefanya hivyo kama nilivyotaja hapo juu kw akununua mastaa kadhaa ambao wamekiimarisha kikosi hicho, lakini upande wa matokeo mambo hayajakaa vizuri.
Kocha yeyote anapopewa fedha kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya, anachotarajiwa kuipa matokeo mazuri timu yake.. Lakini matokeo yanayolengwa huwa hayatokei haraka kama ilivyo matumaini ya wengi.
Inafahamika kuwa mmiliki wa Chelsea Roman Abramovich hana uvumilivu kwa makocha ambao wameshindwa kuleta matokeo mazuri. Tajirihuyo huwa anatajwa kuwa na ‘kisu’ kikali kwaajili ya kuchinjilia mbali makocha wake kwa madaiya kuwa na matokeo mabovu zaidi. kwa maana hiyo hadi sasa swali kubwa linalobaki ni hilo iwapo Lampard anakikaribia kisu cha Abramovich ama atakwepa.
Msimu wa kwanza Lampard alikuwa na sababu nyingi za kueleza kwanini timu yake haijafanya vizuri. Kumpoteza nyota wake, klabu kufungiwa kuitosajili, kukosa wachezaji wenye viwango vya kimataifa ni miongoni mwa mambo yaliyokwaza ufanisi wake.
Hata kocha wa Manchester City Pep Guardiola alipojiunga na timu hiyo, alitumia fedha nyingi lakini hakushinda katika msimu wake wa kwanza. Hii inaonesha kwamba inachukua muda kuongeza thamani kwa kitu chochote kile.
Wachezaji ambao wameletwa na Lampard ni vijana wadogo kutoka nje ya nchi na wanahitaji muda kuzoea EPL ambayo inakabiliwa na wimbi la ugonjwa wa corona. Tunaweza kusema kwa upande mmoja ugonjwa wa corona umesababisha mazingira magumu ya kufanya kazi kwani wachezaji hawawezi kuziona familia zao kwa hofu ya kuambukizwa.
Lampard wakati akikabiliwa na kibarua kigumu kutokana na matokeo mabovu, huku kisu kikali cha Abramovich bila shaka kinanolewa. Kama sifa ya mchezaji mkongwe klabuni hapo kupewa nafasi ya kufundisha basi Lampard amefanikiwa. Chelsea naowamefanikiwa kudumisha utamaduni wa klabu kuwaamini wachezaji wao wa zamani, wakiwemo Peter Cech ambaye ni mkurugenzi wa michezo.
Kwa mantiki hiyo ukongwe wa Lampard na wenzake unawanusuru kuchinjwa na Abramovich, lakini tajiri huyo huwa hana subira mambo yakiwa magumu zaidi. bila shaka mwishoni mwa msimu huu Lampard atakuwa kikaangoni hususani akishindwa kufuzu kabisa kwa Ligi ya Mabingwa.
Lampard akipona kukatwa na kisu hiki basi msimu ujao ajiandae kufungashiwa virago kama atapata matokeo mabovu. Hapo ndipo linapoingia jina la Brendan Rodgers mmoja wa makocha mahiri ambaye alianzia kazi hiyo Chelsea, na bila shaka huyu anaweza kuwa kirusi kingine cha kumwondoa Lampard klabuni.