Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema
litaifungia Tanzania iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia
shughuli za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia taarifa mbalimbali za vyombo vya
habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imeonesha
nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa
TFF, Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella
Mukangara) kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika
uchaguzi wakati tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa
uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa
Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda iwapo TFF haitatekeleza maagizo
yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa FIFA,
Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa na vyombo vya habari yatathibitika kuwa
kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha
shughuli zao kwa uhuru bila kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa
katika ibara za 13 na 17 za Katiba ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali yatatekelezwa,
suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua zaidi
ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na
uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya athari ambazo Tanzania itakumbana nazo
endapo itasimamishwa ni timu za taifa pamoja na klabu kutoshiriki mechi za
kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine watakaoweza kunufaika
na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na
Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA ilishatangaza
itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa
mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje
kuchunguza (suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu
kushughulikia tatizo hili kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa mamlaka
zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania
utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua
inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.