Menu
in , , ,

Fifa: Warner afungiwa maisha

 
Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), Jack Warner amefungiwa kujihusisha na masuala ya soka kwa maisha yake yote.

Kamati ya Maadili ya Fifa imetoa uamuzi huo baada ya uchunguzi wake ndani ya Fifa, ambapo uamuzi huo umetokana na matendo yake yanayoonekana kwamba yalikwenda kinyume cha maadili na kanuni za soka.

Warner, 72, anatoka Trinidadian & Tobago na alipata kuwa Mkuu wa Shirikisho la Soka la Caribbean na Amerika Kaskazini na Kati (Concacaf), lakini aliondoka Fifa 2011. Kwa sasa anachunguzwa na wapelelezi wa Marekani, wanaotaka apelekwe nchini humo kukabiliana na kesi za wizi wa fedha, rushwa na utakatishaji wa fedha.

Hata hivyo, anachuana kisheria na mamlaka za Marekani, akikataa kupelekwa Marekani, akitaka aachwe akae nchini mwake kwa sababu hajafanya kosa lolote. Anakana kupokea mamilioni ya dola kama hongo ili kufanikisha matakwa ya watoaji.

“Warner alijihusisha na matendo mbalimbali ya utovu wa nidhamu kwa kujirudia rudia, kinyume cha maadili ya vyombo vya soka. Katika nafasi yake kama ofisa wa soka, alikuwa mhusika muhimu katika mipango iliyohusisha utoaji ofa.

Advertisement
Advertisement

“Amehusika pia katika upokeaji na maandalizi ya upokewaji wa malipo batili pamoja na kuandaa miradi ya kutengeneza fedha isiyo na maelezo ya kuridhisha,” ilisema sehemu ya uamuzi wa kamati hiyo, iliyochunguza zaidi mchakato wa kuwania kandarasi ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia 2018 na 2022.

Uamuzi huo unakuja siku moja tu baada ya Kamati ya Maadili ya Fifa kuanzisha uchunguzi dhidi ya Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya (Uefa), Michel Platini, akidaiwa kupokea pauni milioni 1.35 kutoka kwa Rais wa Fifa, Sepp Blatter.

Malipo hayo yalifanyika muda mfupi tu kabla ya uchaguzi wa Fifa miaka minne iliyopita, kisha Platini akajitoa kuchuana na Blatter. Platini anadai kwamba yalikuwa malipo halali kwa kazi aliyoifanyia Fifa kama mshauri wa ufundi wa Rais Blatter, lakini malipo yalifanywa miaka tisa baadaye.

Kadhalika tukio hili limekuja baada ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu (AG) wa Uswisi kufungua jalada na kuanza uchunguzi dhidi ya bosi wa Fifa, Blatter, akidaiwa kujihusisha na matendo ya jinai na uchunguzi bado unaendelea.

Maofisa saba wa Fifa walikamatwa jijini Zurich Mei mwaka huu kabla ya mkutano wa uchaguzi mkuu wa Fifa wakaunganishwa na wengine saba wanaohusiana na dili chafu zinazodaiwa kufanywa ndani ya Fifa kwa miongo kadhaa, mashauri yao yakiwa nchini Marekani wanakotakiwa.

Written by Israel Saria

For the last 20 years I have been working as a football pundit. This experience has provided me with a very useful insight into football and the opportunity to carry out extensive research into the game including its players, the stadiums, the rules and tactics and I have also been grateful to meet a wide range of people connected to football in the UK, Tanzania, Germany .....

Exit mobile version