|
||||
Kiungo wa timu ya Yanga na Taifa Stars Athuman Idd(Chuji) ambaye ameangukiwa na dhahama ya kutocheza mechi za ligi kuu kwa muda wa miezi mitatu kutokana na utovu wa nidhamu uwanjani | ||||
WAKATI machungu ya kuchapwa bao 1-0 na Majimaji ya Songea juzi hayajapoa, Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania, TFF limewafungia, kocha wa Yanga, Dusan Kondic na kiungo wake, Athumani Idd ëChujií kwa kile kilichoelezwa kuwa ni utovu wa nidhamu.
Yanga ilichapwa bao 1-0 na timu hiyo ya Songea katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Majimaji na kuifanya timu hiyo ya Songea kuvuna pointi tatu za kwanza za ligi.
Taarifa ya TFF jana ilisema kuwa Kamati ya Mashindano ya shirikisho hilo, imewafungia Kondic na Chujií kutokana na utovu wa nidhamu waliouonyesha katika mechi dhidi ya African Lyon, siku ya uzinduzi wa Ligi Kuu ya Vodacom, kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Katika mchezo huo timu ulimalizika kwa sare bao 1-1.
Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema katika taarifa hiyo ya Kamati ya Mashindano iliyokutana katikati ya wiki iliyopita, ilifikia maamuzi ya kumsimamisha mechi tatu Kondic kutokana na kumtolea lugha chafu, mwamuzi msaidizi, Hamis Changíwalu katika mchezo huo.
Taarifa hiyo iliendelea kuwa Kondic atakosa mchezo namba 19 dhidi ya JKT Ruvu utakaopigwa Dar es Salaam, pia 25 dhidi ya Mtibwa Sugar na 35 dhidi ya Kagera Sugar. Mechi zote hizi zitakuwa nje ya Dar Salaam.
Alisema pia kuwa Chuji amesimamishwa miezi mitatu kwa kile kilichoelezwa kutaka kushambulia waamuzi katika mchezo huo. ìSiku ya mchezo alitaka kuwapiga waamuzi na walipoingia kwenye vyumba vyao, alionyesha dhamira ya wazi kutaka kufanya fujo ikiwemo kuwapiga kwani alibamiza mlango kwa mateke,î alisema Mwakalebela.
Mwakalebela alisema baada ya mchezo kumalizika aliingia uwanjani akitokea kwenye benchi la akiba na licha ya kuzuiwa na wachezaji wenzake wa akiba, aliendelea kufanya hivyo. Adhabu ya Chuji iliyoanza jana, itamalizika Desemba 6 na kumfanya akose mechi mbalimbali ikiwemo ya watani, Simba itakayochezwa Oktoba 31.
ìKwa mujibu wa Kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom, Kanuni ya 25 kifungu cha 1 g (iii) mchezaji huyo ameadhibiwa kutocheza mpira kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Septemba 6, 2009,î ilisema sehemu ya taarifa ya TFF.
Mbali na adhabu hizo za Kondic na Chuji, klabu ya Yanga imepigwa faini ya Sh500,000 kutokana na kushindwa kudhibiti mashabiki wake wakati wa mchezo huo kwa kuwarushia waamuzi mawe na chupa za maji, kitendo hicho ni hatari na kinaweza kuhatarisha amani. TFF imeitaka Yanga kulipa fedha hizo kabla ya mchezo unaofuata.
Mwakalebela alisema pia kuwa Kamati ya mashindano inazikumbusha klabu kuhakikisha zinadumisha amani na usalama katika viwanja wakati wote, ndani na nje ya uwanja.