*Ajivunia mataji 38 kwa miaka 26
*Maswali ya atakayemrithi yatanda
Mtikisiko umeukumba ulimwengu wa soka, baada ya tamko la kocha mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson kwamba ameamua kung’atuka.
Mwangwi wa uamuzi na tangazo la klabu hiyo kubwa haukuishia nchini tu, bali ulisambaa kwenye nchi nyingi za wapenda soka, ambao licha ya kushangazwa, wameanza tayari kujiuliza mrithi wake atakuwa nani.
Fergie anaachia ngazi baada ya miaka 26 na ushee wa utumishi uliotukuka mfululizo Old Trafford, akichukua nafasi ya Ron Atkinson.
Katika muda wake huo, Fergie aliyetunukiwa heshima ya ‘Sir’ na Malkia Elizabeth II 1999, alifanikiwa kutwaa mataji tofauti 38, ukiwamo ubingwa wa England mara 13, na wapo wanaoona kwamba ameshapata kila kitu kwenye soka, hivyo amechoka kushinda na anaamua kupumzika.
United wametwaa ubingwa waliopoteza mwaka jana kwa mahasimu wao wa Manchester – Manchester City, huku ligi ikiwa bado inaendelea, na hapakuwa na dalili zozote za Fergie (71) kuachia nafasi yake hiyo, kwani ni wiki hii tu alikuwa akisema kombe walilotwaa analiona kama mwanzo wa muongo mwingine wa mafanikio lukuki.
Hata hivyo, inaeleweka kwamba Fergie amekuwa akisumbuliwa na mguu, na anatarajiwa kufanyiwa upasuaji mwishoni mwa msimu huu, na wakubwa wa United walikuwa wamesema upasuaji haungeathiri programu zake wala za klabu, lakini sasa imetokezea kwamba atajiuzulu pia mwishoni mwa msimu na atakuwa mkurugenzi klabuni hapo na balozi.
Ferguson ndiye kocha mwenye mafanikio zaidi nchini Uingereza, na pia aliyeongoza klabu kwa muda mrefu zaidi, akifuatiwa na Arsene Wenger wa Arsenal na David Moyes wa Everton. Moyes anapigiwa chapuo kumrithi Fergie, lakini pia bado kuna tetesi za kwamba Jose Mourinho huenda asirudi Chelsea, bali aende Old Trafford.
Wiki iliyopita, hata hivyo, alikuwa akitajwa tajwa Jurgen Klopp, kocha wa Borussia Dortmund aliyewafikisha fainali watakayocheza dhidi ya Wajerumani wenzao, Bayern Munich, kwamba anaweza kumrithi Fergie siku akiondoka, ambapo wadadisi walidhani ni ‘miaka mingi’ ijayo.
Katika tamko lake, Ferguson anasema haikuwa rahisi kufikia uamuzi huo, alifikiria kwa muda mrefu na ameridhika kwamba huu ni wakati mwafaka kung’atuka. Mechi yake ya mwisho itakuwa dhidi ya West Bromwich Albion Mei 19, na kuanzia hapo ataingia kwenye bodi ya klabu kama mkurugenzi.
“Ilikuwa muhimu kwangu kuondoka katika taasisi hii ikiwa imara kwa kadiri ambavyo ingewezekana na naamini nimefanya hivyo. Kiwango cha kikosi hiki kilichotwaa kombe na uwiano wa umri ndani mwake vinashamirisha mafanikio kwenye ngazi za juu kabisa na mfumo wa timu ya vijana ni ashirio la uendelevu wa uimara wa klabu kwa muda mrefu ujao,” akasema Ferguson.
Akaongeza kwamba viwanja na vifaa vya mazoezi vya United ni kati ya vilivyo bora zaidi duniani na kwamba sasa anafurahia kuingia katika majukumu ya kuwa mkurugenzi na pia balozi wa klabu hiyo, na pia akiendelea na mambo mengine anayovutiwa nayo.
Makombe aliyotwaa Fergie akiwa Manchester United ni kubwa zaidi Ubingwa wa England (EPL) 1993, 1994, 1996, 1997, 1999, 2000, 2001, 2003, 2007, 2008, 2009, 2011 na 2013.
Pia alitwaa Kombe la FA miaka ya 1990, 1994, 1996, 1999 na 2004. Alitwaa Kombe la Ligi 1992, 2006, 2009 na 2010.
Kimataifa Fergie hajambo, kwani ametwaa Kombe la Mabingwa Ulaya 1999 na 2008; Kombe la Mabingwa (Cup Winners Cup) 1991; Kombe la Klabu la Dunia la FIFA 2008; UEFA Super Cup 1992; Kombe la Mabara 1999 na Ngao ya Jamii 1990, 1993, 1994, 1996, 1997, 2003, 2007, 2008, 2010 na 2011.
Ferguson alizaliwa Desemba 31, 1941 Scotland na mbali na Man U amezifundisha klabu za East Stirlingshire mwaka 1974 na mwaka huo huo alihamia St. Mirren hadi 1978 alipokwenda Aberdeen. Alifundisha timu ya taifa ya Scotland kuanzia 1985 hadi 1986 alipoanza kuwafundisha Manchester United.
Ferguson alianza soka kwa kucheza, ambapo kati ya 1957–1960 alikuwa Queen’s Park; 1960 –1964 akacheza St. Johnstone; 1964–1967 akakipiga Dunfermline Athletic. Alijiunga Rangers 1967 kwa miaka miwili na 1969 akaenda Falkirk hadi 1973 alipohamia Ayr United akacheza kwa mwaka mmoja tu akaanza ukocha. Amechezea pia timu ya taifa ya Scotland.